26.9 C
Dar es Salaam
Wednesday, December 6, 2023

Contact us: [email protected]

MLALAMIKAJI AANGUA KILIO MBELE YA TUME

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Bonaventura Mushongi
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Bonaventura Mushongi

CHRISTINA GAULUHANGA -DAR ES SALAAM

MLALAMIKAJI Jimmy Sandy (60), ameangua kilio mbele ya Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB), wakati akielezea jinsi Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Bonaventura Mushongi na maofisa wenzake saba walivyoinyanyasa na kuidhalilisha familia yake.

Akitoa ushahidi dhidi ya malalamiko yake aliyoyafikisha mbele ya tume hiyo jana, Sandy alidai familia yake ilidhalilishwa kwa sababu ya kushindwa kuwapa polisi Sh 300,000 ambazo wafanyabiashara wa Pwani hutoa kwa kamanda wa polisi kwa ulinzi.

Shauri hilo linasikilizwa chini ya Mwenyekiti wa tume hiyo, Bahame Nyanduga.

Walalamikiwa ni Kamanda Mushongi, Mkuu wa Polisi Wilaya ya Mkuranga, Edson Kasekwa, aliyekuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Japhary Ibrahim na aliyekuwa Mkuu wa Polisi Wilaya ya Mkuranga, OCD Mayenga Mapalala.

Wengine ni G.7429 Konstebo Swalehe, Mkaguzi Msaidizi wa Polisi, Janeth Thobias, E.99272 D/Koplo Trano Peter na G.8941 Konstebo Nuhu.

Akitoa ushahidi wake, Sandy ambaye ni mmiliki wa kiwanda cha kutengeneza juisi aina ya Sophy, huku akiangua kilio alidai kuwa Juni 8, 2015 baadhi ya askari walifika nyumbani kwake Kiparang’anda, Mkuranga na kumkuta mkewe, wakataka awape fedha za ulinzi Sh 300,000 kwa madai wametumwa na OCD wa wilaya hiyo.

“Siku hiyo walikuja askari polisi wawili, wakajitambulisha kuwa ni Nuhu na Swalehe na kudai wametumwa na Mkuu wa Polisi Wilaya, waje wachukue Sh 300,000. Mke wangu aliwajibu sipo, waliondoka na kuacha namba zao ili niwasiliane nao,” alidai Sandy.

Sandy aliongeza kuwa walalamikiwa walidai utaratibu huo ni wa kawaida, kwamba wafanyabiashara wa Pwani hutoa kiasi hicho ili waweze kupewa ulinzi.

“Baada ya kupokea taarifa hizo kutoka kwa mke wangu, alinipa namba hiyo. Niliipiga na ilipokewa na mtu aliyejitambulisha kuwa ni Nuhu, nikamwambia siwezi kutoa kiasi hicho cha fedha,” alisema.

Pia alidai kuwa Juni 10, 2015, alipigiwa simu na dereva wake, Mohamed Ally ambaye alimweleza  nyumbani kwake wamevamia askari kama 20 wakiwa na silaha.

Aliendelea kudai kuwa baada ya kuendelea kuhoji kilichotokea nyumbani na kama viongozi wa mtaa wake wapo, aliambiwa hawapo na afanye jitihada aiokoe familia yake kwani watoto, mke wake na wafanyakazi wake wa kiwandani wanateswa na polisi.

“Roho iliniuma sana siku hiyo kwa sababu aliyenipigia aliniambia nyumba yangu imegeuka bwawa la juisi, polisi wamechukua juisi yote iliyokuwa ikitengenezwa kiwandani kwangu na kuimwaga,” alidai Sandy.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
580,000SubscribersSubscribe

Latest Articles