AMINA OMARI -TANGA
SERIKALI imesema haitaagiza nguzo za umeme nje ya nchi kwa sababu wazalishaji wa ndani wamezalisha za kutosha.
Kauli hiyo, imetolewa na Waziri Mkuu Majaliwa Kassim Majaliwa alipozindua kiwanda cha kuzalisha nguzo za umeme Muha Traders kilichopo Pongwe.
Alisema wakati wa utekelezaji wa miradi ya umeme vijijini, Serikali itatumia nguzo ambazo zinazolishwa nchini.
“Tunanguzo nyingi,hatuagizi kutoka nje kwani zamani Serikali ilikuwa inapata hasara kuagiza nguzo nje ya nchi,”alisema Waziri Mkuu.
Aliwataka watendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), kuhakikisha wanawasimamia kwa ukaribu wakandarasi wanaosimamia miradi ya REA ili kuhakikisha wanafanyakazi kwa ufanisi.
Alisema nia ya Serikali, ni kufikisha umeme maeneo yote ya vijijini na vitongoji ili kutoa fursa kwa wananchi kuitumia huduma hiyo.
Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Martin Shigela alisema Serikali imepata Sh milioni 45 kutokana na kodi ya mazao ya nguzo.
“Baada ya agizo ulilolitoa la kukusanya kodi katika viwanda vya uzalishaji wa nguzo, tumebaini deni la Sh milioni 162, tumewekeana utaratibu wa kulipa na mwekezaji,”alisema.