25.6 C
Dar es Salaam
Monday, November 25, 2024

Contact us: [email protected]

Majaliwa ashtushwa DART kutoanza kazi

kasimNa Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa, ameitisha kikao ofisini kwake na kutaka apewe taarifa ambayo amehoji ni kwanini mradi wa mabasi yaendayo kasi (DART) haujaanza kazi hadi sasa.

Pamoja na hali hiyo, amewataka wakurugenzi wa vitengo na wakuu wa taasisi katika Ofisi ya Waziri Mkuu (TAMISEMI), kuhakikisha wanapata nakala ya hotuba ya Rais Dk. John Magufuli ya uzinduzi wa Bunge kwa kuisoma na kuifanyia kazi.

Kauli hiyo aliitoa jijini Dar es Salaam jana alipokuwa akizungumza na  wakuu wa taasisi, wakurugenzi na watumishi wa Ofisi ya Waziri Mkuu (TAMISEMI).

Alisema leo anahitaji taarifa ya kutoanza kazi kwa mradi wa DART kama ilivyopangwa.

“Kesho (leo) saa 4 asubuhi Katibu Mkuu, Mkurugenzi Mkuu DART na watendaji wako mje ofisini. Nataka kupata maelezo ni kwanini mabasi hayajaanza kazi hadi leo. Je, ni lini yataanza kazi? Je, ni nani anakwamisha? Na hata kama ni sheria, ni kwanini tusizi-harmonise ili kuondoa hivyo vikwazo?”

“Ninataka kupata haya maelezo kwa sababu Watanzania na hasa wana-Dar es Salaam, wamesubiri kwa muda kuona mradi ukianza kazi ili uondoe kero ya usafiri. Wao wanajua anayehusika ni TAMISEMI,” alisema.

Akizungumzia utendaji wa taasisi zilizo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu, alisema anatamani kuona mabadiliko ya utendaji kazi serikalini katika kipindi kifupi.

“Natamani kila mmoja asiridhike na uzembe unaofanywa huku chini. Nyote ni wataalamu, kwahiyo mnapaswa kudhihirisha elimu yenu na ujuzi mlionao,” alisema.

Alisema kila mkurugenzi na mkuu wa taasisi anapaswa kuongeza usimamizi na ufuatiliaji wa kazi kwenye sekta yake, kwani hilo litasaidia kukidhi matarajio ya Watanzania ya kuona mabadiliko ya utendaji kazi kwenye Serikali ya awamu ya tano.

“Ninyi wakurugenzi siyo desk officers bali ni field officers. Nataka muweke utaratibu wa kwenda vijijini mkasimamie watu wenu, pia mhimize uadilifu, uaminifu na weledi wa kazi, mambo ninayotaka mhimize watendaji waliopo chini yenu ni muda wa kuripoti kazini uzingatiwe, muda wa kukaa kazini uzingatiwe,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles