31.2 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

Mbunge amwomba Spika asilipwe posho

4.Elibariki-akisoma-taarifa-yake-aliyokuwa-ameiandaa-kwa-wanahabari.NA SHABANI MATUTU, DAR ES SALAAM

MBUNGE wa Singida Magharibi, Elibariki Kingu (CCM), amemwandikia barua Spika wa Bunge, Job Ndugai,  akimwomba kumsitishia malipo ya posho ya vikao  vya Bunge kwa muda wa miaka mitano ya uhai wa Bunge la 11.

Alisema badala yake fedha hizo zielekezwe kwenye huduma za elimu, afya na huduma za maji.

Kutokana na uamuzi wake huo, amemwomba Spika Ndugai, kuridhia suala hilo na fedha hizo ziingizwe kwenye akaunti maalumu ambayo itakuwa chini ya mkuu wa wilaya pamoja na wajumbe wake.

Akitangaza uamuzi huo jana mbele ya waandishi wa habari, Kingu, alisema ameshawasilisha barua hiyo na anaamini itafanyiwa kazi kwa uzito unaostahili na ofisi ya Spika.

“Nimewasilisha barua jana (juzi), ambayo ni hatua ya kwanza ya kutekeleza dhamira yangu hii ya kutaka miaka mitano nitakayokuwa nikiwatumikia wananchi wangu katika shughuli mbalimbali za kibunge, sitapokea pesa za posho zenye nia ya kunufaisha tumbo langu, huku watu wangu wakiendelea kutaabika kwa kukosa huduma muhimu za elimu, afya na maji katika jimbo langu,” alisema Kingu.

Mbunge huyo mpya wa Singida Magharibi, ambaye pia aliwahi kuwa Mkuu wa Wilaya ya Igunga mkoani Tabora, alisema kwa sasa Bunge linapaswa liwe na wabunge 394 na vikao vya Bunge kisheria kwa muda wa mwaka mmoja ni siku 182  ambapo kila mbunge hulipwa Sh 220,000  kwa kushiriki kikao kwa siku.

“Fedha hizi kama zitaondolewa au wabunge wenzangu wataridhia kutokuchukua, basi tutakuwa tumeokoa zaidi ya shilingi bilioni 15.7 mwaka mmoja wa Bunge,” alisema Kingu.

Alisema ili apate uhalali wa kuikemea Serikali katika matumizi yasiyo ya lazima, ameona aanze kujiwajibisha kwa kuanza kukataa kuchukua malipo ya vikao, kwa kipindi chake chote cha miaka yake mitano bungeni, ili pesa hizo zielekezwe katika shughuli za maendeleo.

“Kwa kuwa fedha hizo za posho ya vikao zipo kikanuni, nimeomba sehemu yangu ielekezwe kutatua huduma mbalimbali katika Jimbo la Singida Magharibi, na tayari hatua ya kwanza ya utekelezaji imeshafanyika kwa fedha hizo kuweza kununua zaidi ya mifuko 100 ya sementi ya ujenzi wa zahanati katika Kijiji cha Mpetu, Kata ya Muhintiri, Tarafa ya Ihanja,” alisema Kingu.

Alisema uamuzi huo ameuchukua kama changamoto kwa wengine wenye nafasi ya kuchukua posho ya vikao, huku wakiwa wanapokea mishahara kutokana na vikao hivyo ambavyo ni sehemu ya kazi yao.

“Ninatambua jambo hili linawezekana na wala Kingu sitokuwa wa kwanza kupinga uchukuaji wa posho hizi, kwani katika Bunge la kumi lililomalizika, Zitto Kabwe aliweza kusimamia hili na kufanikiwa kwa sababu ya dhamira safi ya kuwatumikia wananchi,” alisema Kingu.

Mbunge huyo kijana alisema atafungua akaunti maalumu ya kusimamia maendeleo kwa kushirikisha mkuu wa wilaya, Sheikh wa Wilaya ya Ikungi, mchungaji mmoja kutoka Kanisa la Wasabato, Mchungaji kutoka CCT, Pentecostal, padri mmoja kutoka Kanisa la Romani Katoliki na Ofisa Mipango wa Wilaya.

Kingu alionyesha waandishi wa habari barua hiyo ambayo ilimtaka Katibu wa Bunge kuheshimu uamuzi wake huo wa kutokubali kupokea fedha ya kujikimu wakati huo huo akiongezwa posho ya vikao.

Katika mkutano wake huo, alitumia fursa hiyo kumuunga mkono Rais Dk. John Magufuli kwa kufuta safari za nje ya nchi, akiitaja hatua hiyo kama sehemu itakayoleta nidhamu ya uwajibikaji katika maeneo mbalimbali ya kazi.

MTANZANIA ilimtafuta Kaimu Katibu wa Bunge, John Joel ili kujua kama barua hiyo imefika, ambapo alisema hadi kufikia jana walikuwa bado hawajaipokea.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles