Na Mwandishi Wetu – Dar es Salaam
WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa, ametembelea mradi ya kuzalisha umeme wa Kinyerezi II na kusema ameridhishwa na maendeleo ya ujenzi wake.
Kauli hiyo aliitoa jana alipotembelea mradi huo wa kuzalisha umeme kwa kutumia gesi asilia unaojengwa Kinyerezi, Dar es Salaam.
Pia alisema kukamilika kwa mradi huo kutaliwezesha taifa kuwa na umeme wa uhakika, utakaowezesha kuendesha viwanda.
Alisema mkakati wa Serikali ni kuongeza kiwango cha uzalishaji ili Watanzania wapate umeme mwingi utakaosambazwa hadi vijijini kwa gharama nafuu.
“Tunataka tupate umeme wa kutosha ili viwanda vitakavyojengwa viwe na nishati ya uhakika na ya gharama nafuu. Ni wajibu wetu kuendelea kuimarisha utekelezaji wa miradi hii,” alisema.
Naye, Meneja Mradi wa Umeme wa Kinyerezi, Stephen Manda, alisema gharama za mradi wa Kinyerezi II ni Dola za Marekani milioni 344.
Alisema tayari mradi huo umefikia asilimia 66.32 ya ujenzi wake na sasa wako katika hatua mbalimbali za kukamilisha, ikiwamo ujenzi wa misingi ya mitambo na jengo la kuiendeshea.
“Tunaendelea na ujenzi wa nguzo za kupokea laini ya msongo wa kilovoti 220 kutoka Kinyerezi I hadi Kinyerezi II… mtambo wa kwanza wa megawati 30 utawashwa ifikapo Desemba, mwaka huu na kila mwezi tutaingiza megawati 30 katika gridi ya taifa,” alisema Manda.
Pia alisema miradi iliyoko eneo hilo ambayo iko katika hatua mbalimbali za utekelezaji ni Kinyerezi I (megawati 150), Kinyerezi I Extension (megawati 185) na Kinyerezi II (megawati 240).
Manda alisema mradi wa Kinyerezi I ulikamilika Machi, mwaka juzi na miradi miwili ya Kinyerezi I – extension na Kinyerezi II inatarajiwa kukamilika mwakani.
Alisema miradi mingine inayotarajiwa kujengwa katika eneo hilo ni wa Kinyerezi III utakaozalisha megawati 600 na Kinyerezi IV utakaozalisha megawati 450.
Awali, Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Sophia Mjema, alisema mradi huo umewanufaisha wananchi wengi wa eneo hilo.
Alisema hadi sasa wananchi 100 wameajiriwa katika miradi hiyo ambayo ni sawa na asilimia 40 ya watumishi wote.
Mbali na ajira, pia alisema wananchi wa Kinyerezi watanufaika kwa kuboreshewa huduma mbalimbali za kijamii katika eneo hilo zikiwamo za maji na elimu na wameahidiwa kupewa madawati ya shule tano.