30.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

WATANZANIA MILIONI 3 WATUMIA UZAZI WA MPANGO

NA VERONICA ROMWALD – DAR ES SALAAM

IDADI ya Watanzania wanaotumia njia za uzazi wa mpango imeongezeka kutoka watu milioni 2.1 mwaka 2010 hadi kufikia watu milioni 3.48 mwaka huu.

Kauli hiyo ilitolewa Dar es Salaam jana na Meneja Utetezi wa Shirika la Advance Family Planning (AFP), James Mlali, alipozungumza katika semina ya kuwajengea uwezo waandishi wa afya na masuala ya jamii kuelekea maadhimisho ya Siku ya Idadi ya Watu Duniani yatakayofanyika Julai 11.

“Ongezeko hilo la watumiaji wa njia za uzazi wa mpango limesaidia kupunguza mimba milioni moja zisizotarajiwa, pia limepunguza kiwango cha utoaji mimba 32,000 zisizotarajiwa na kumeepusha vifo 3,300 vitokanavyo na uzazi,” alisema.

Alisema bado jamii inahitaji elimu ya kutosha kwa sababu Tanzania inatajwa kuwa ni miongoni mwa nchi ambazo watu wake wanazaliana kwa kasi kubwa.

“Takwimu zinaonyesha ongezeko la watu ni kubwa kuliko miundombinu na rasilimali zilizopo, inakadiriwa ifikapo mwaka 2025 kama hatua hazitachukuliwa, idadi ya huduma za kijamii zilizopo itahitajika kuongezeka mara tatu zaidi.

“Kwa mfano kama tuna vituo 7,000 vya kutolea huduma za afya, maana yake tutahitaji kuwa na mara tatu yake ambavyo ni vituo 21,000,” alisema.

Alisema endapo hali hiyo haitadhibitiwa, itasababisha pia ongezeko kubwa la ukosefu wa ajira kuliko inavyoshuhudiwa hivi sasa.

Kwa upande wake, Ofisa Habari wa Tume ya Mipango Tanzania, Adili Mhina, alisema licha ya Serikali kuelimisha jamii juu ya umuhimu wa kupanga uzazi, lakini bado kuna changamoto.

“Tunaongezeka kwa kasi kubwa, katika sensa ya mwaka 1967 idadi ya watu iliongezeka kutoka milioni tisa mwaka 1961 hadi milioni 12.3. Katika sensa ya 2012 tuliongezeka hadi kufikia watu milioni 45,” alisema.

Kutokana na hali hiyo, alisema ipo changamoto ya upungufu wa miundombinu na huduma kutosheleza mahitaji.

“Mahitaji yameongezeka kwa sababu ya shinikizo la ongezeko la idadi ya watu. Kila mwaka vijana milioni 1.2 wanaofikia umri wa kuajiriwa, vijana 300,000 pekee ndio wanaoajiriwa,” alisema.

Pia alisema hali hiyo imesababisha wimbi kubwa la ujenzi wa makazi holela na kuzuka kwa maeneo ya biashara yasiyo rasmi na yasiyoendana na taratibu za ustawi wa jamii.

Naye Ofisa Habari wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Idadi ya Watu (UNFPA), Wallen Bright, alisema kwa mwaka huu maadhimisho hayo yatafanyika Temeke Mwembe Yanga, Dar es Salaam.

“Katika maadhimisho hayo, tunatarajia mgeni rasmi atakuwa Naibu Waziri wa Afya, Dk. Hamis Kigwangwalla,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles