25.3 C
Dar es Salaam
Friday, January 3, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

Majaliwa amkabidhi Jafo majina ya watumishi waliogoma kuhama

Na Mwandishi Wetu, Dodoma



WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa, amemkabidhi Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Tamisemi), Selemani Jafo, orodha ya watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Bahi ili awachukulie hatua baada ya kugoma kuhamia katika kituo chao cha kazi na kuendelea kuishi jijini Dodoma.

Orodha hiyo alimkabidhi jana baada ya Mkuu wa Wilaya ya Bahi, Mwanahamisi Mukunda, kusoma taarifa iliyoeleza kuwa watumishi wote wameshahamia katika kituo chao cha kazi na wanaishi.

Waziri Mkuu alikuwa katika kikao na watumishi wa halmashauri hiyo.

Hata hivyo, Majaliwa, alimwambia Mwanahamisi kwamba amedanganywa.

“Mkuu wa wilaya umedanganywa, watumishi bado wanaishi jijini Dodoma, walichokifanya baadhi wamejiunga watatu na wamekodi chumba kimoja. Namkabidhi Waziri wa Tamisemi orodha ya watumishi ambao wamegoma kuishi katika kituo chao cha kazi ili uwashughulikie,” alisema.

Majaliwa alisema watumishi hao wamegoma kuhamia katika kituo chao cha kazi licha ya kutakiwa kufanya hivyo.

“Maelekezo hatuyatoi kwa ajili ya kujifurahisha, bali tunataka utekelezaji ufanyike ili wananchi wahudumiwe ipasavyo,” alisema.

Juni 27, mwaka huu, Majaliwa, akizindua vituo 51 vya kufuatilia taarifa za hali ya hewa, vituo 15 vya haidrolojia, kanzidata ya taarifa za hali ya hewa na kituo cha operesheni na mawasiliano ya dharura Bahi, aliwaagiza watumishi wa halmashauri hiyo wanaoishi nje ya kituo chao cha kazi wahamie kituoni kwao.

Alisema Serikali inataka watumishi wa umma wawajibike na waishi katika vituo vyao vya kazi.

“Nawataka watumishi wote wa wilaya hii wanaoishi jijini Dodoma wawe wamehamia hapa ifikapo Julai 30 mwaka huu na wasiohamia nipewe majina yao,” alisema.

Pia Majaliwa aliwataka viongozi na watumishi wa Bahi wakiwamo madiwani na wakuu wa idara wahakikishe wanamaliza tofauti zao na washirikiane kufanya kazi kwa lengo la kuboresha maendeleo ya wananchi.

Awali, alikagua mradi wa ujenzi wa nyumba ya walimu katika Shule ya Sekondari ya Mpalanga yenye uwezo wa kukaliwa na walimu sita na alisema ameridhishwa na ujenzi huo uliogharimu zaidi ya Sh milioni 140.

Pia alizindua Daraja la Chipanga ambalo ujenzi wake umegharimu Sh bilioni 2.18 na kisha alitembelea Kituo cha Afya cha Bahi alikokagua wodi ya wazazi na kuzungumza na akina mama walioishukuru Serikali kwa kuboresha huduma za afya.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles