WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa, amemwagiza Katibu Mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera na Bunge), Uledi Mussa, kufuatilia malipo ya kiwanja kilichouzwa na Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu Dadoma (CDA) kwa Sh milioni 240, lakini fedha iliyoingia serikalini ni Sh milioni 6 tu.
“Katibu Mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu, ninataka ufuatilie mauzo ya kiwanja namba 26 block AA eneo la Kikuyu East ambacho kimeuzwa kwa Sh milioni 240, lakini fedha iliyoingia CDA ni milioni 6 tu. Nataka kujua nani ameingiza kiasi hiki, na nani kachukua hizo Sh milioni 234,” alisema.
Waziri Mkuu alitoa agizo hilo jana, wakati akizungumza na watumishi na viongozi wa mamlaka hiyo kwenye ukumbi wa Hazina ndogo mjini Dodoma.
Bila kutoa ufafanuzi zaidi, Waziri Mkuu alisema eneo hilo lilipaswa kuwa na kituo cha mafuta na akataka apatiwe taarifa mapema iwezekanavyo.
Pia amemwagiza Katibu Mkuu, afuatilie mkataba wa upangishaji wa jengo la CDA ambalo wamepangishwa taasisi ya Tunakopesha Limited kwa madai kuwa mhusika alipewa bure na sasa anataka kulipangisha tena ili apate cha juu.
Waziri Mkuu amewaonya watumishi hao pamoja na viongozi wao, waache tabia ya kushirikiana na madalali kuuza viwanja na akawataka wachape kazi wakijielekeza na kasi ya Serikali kuhamia Dodoma.
“Tabia ya watumishi kushirikiana na madalali kuuza ardhi sasa basi. Hata hivyo, nimefarijika kukuta mmeanza kuweka mfumo wa kielektoniki katika baadhi ya huduma. Lazima mauzo ya viwanja sasa hivi yafanyike kwa njia ya kieletroniki, madalali hawana nafasi,” alisema.
Ameutaka uongozi wa CDA uongeze kasi ya upimaji viwanja kwa sababu mahitaji ni makubwa, lakini akaonya wakati kazi hiyo ikifanyika, wananchi walionunua viwanja na bado hawajamalizia kuvilipia, wasinyang’anywe kwa kigezo cha kutaka kuwauzia wengine.
“Mimi nataka idadi ya viwanja vilivyopimwa iongezeke. Lakini pia msitumie fursa hii kuwanyang’anya watu wenye umiliki halali eti kwa sababu Serikali inataka idadi ya viwanja vilivyopimwa iongezeke,” amesema.
“Kama mtu amepewa offer au hati yake asinyang’anywe hata kama amelipia nusu. Ahimizwe kumalizia hilo deni na nyinyi kazi yenu ni kupima viwanja vingine.
“Natambua mnayo benki ya viwanja, inabidi mwongeze idadi ya viwanja vingi zaidi. Tumeita wawekezaji waje kujenga nyumba za kuishi watumishi, mahoteli na viwanda na maeneo yote haya inabidi yatengwe rasmi,” amesema.
Alisema viwanja 70,000 vimepimwa tangu CDA ianzishwe mwaka 1973. Alisema kama wataendelea na kasi hiyo, wakati mahitaji yameongezeka, itawachukua zaidi ya miaka 40 kukamilisha mahitaji ya viwanja 100,000 ambavyo vinatarajiwa kuanza kupimwa hivi karibuni.
Akitoa taarifa kwa Waziri Mkuu, Mkurugenzi Mkuu wa CDA, Mhandisi Paskasi Muragili alisema usanifu wa upimaji viwanja 20,000 umekamilika na kwamba wana lengo la kupima viwanja vingine 100,000 ifikapo Juni 2017.
Waziri Mkuu alitembelea Ofisi ya CDA na kukagua mfumo wa utunzaji mafaili wa zamani pamoja na uhamishaji wa taarifa za wenye viwanja kwenye mfumo wa kompyuta. Pia alikagua mifumo ya uuzaji viwanja kwa njia ya mtandao ambayo hata hivyo bado haijakamilika.