28.2 C
Dar es Salaam
Thursday, January 2, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

Majaliwa aagiza vyoo, mifumo ya maji viwandani ikaguliwe

Na Mwandishi Wetu, Dodoma

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa, ameiagiza Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, ishirikiane na Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi na Ajira, kufanya ukaguzi wa vyoo na mifumo ya kutiririsha maji katika viwanda vyote na vitakavyobainika na makosa hatua kali zichukuliwe.

Pia amewaagiza maofisa afya na mazingira katika mikoa yote nchini badala ya kuzingatia maeneo ya hoteli, mabucha na migahawa waende kwa jamii na kutoa elimu ya matumizi ya vyoo bora na umuhimu wa usafi wa mazingira.

Agizo hilo alilitoa jijini hapa jana katika kilele cha Maadhimisho ya Wiki ya Usafi wa Mazingira Kitaifa na mkutano wa maofisa afya wa mikoa, halmashauri na wadau wa afya na mazingira.

Alisema viwanda vina jukumu la kuhakikisha vinatunza afya za wafanyakazi wake kwa kufuata taratibu na sheria za afya kazini.

“Ni jukumu la kila kiwanda kuhakikisha kinadhibiti uchafuzi wa hewa ili tuweze kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi,” alisema.

Pia alisema kwa sasa madhara ya mabadiliko ya tabianchi yameanza kushuhudiwa nchini na endapo jitihada za makusudi zisipochukuliwa ipo hatari ya kufifisha matarajio ya kesho ya watoto.

Aliwataka wakuu wote wa mikoa, wilaya, wakurugenzi wa halmashauri na maofisa watendaji wa kata, mitaa na vijiji kusimamia vizuri kampeni ya usafi wa mazingira na matumizi ya choo bora.

“Hakikisheni kuwa lengo la kila kaya nchini kupata choo bora kabla ya tarehe 31 Desemba, mwaka huu linafikiwa. Waziri mwenye dhamana, tambua kwamba baada ya tarehe husika kupita nitahitaji kupata taarifa kuhusu utekelezaji wa agizo hilo kutoka kila mkoa na halmashauri nchini,” alisema.

Pia alisema ameelezwa kuwa hadi kufikia Septemba 30, mwaka huu kaya zenye vyoo bora zimefikia asilimia 51.4 kutoka asilimia 46.6 Julai, mwaka jana na katika kipindi hicho kaya zisizokuwa na vyoo kabisa zimepungua kutoa asilimia 5.4 hadi asilimia 3.8.

Alisema iwapo watazidisha kasi katika utoaji wa elimu, usimamizi wa sheria na kuongeza ufuatiliaji, kaya zote zitakuwa na vyoo bora ndani ya muda mfupi ujao.

“Nimedokezwa hapa kwamba, Halmashauri ya Wilaya ya Njombe wamefanikiwa kwa kiasi kikubwa katika hilo. Sasa nitashangaa kwanini wengine mshindwe?

Pia alisisitiza uwapo wa huduma za vyoo bora kwa taasisi zote za umma na binafsi. “Ninaagiza shule zote, vituo vyote vya tiba, vituo vya abiria, masoko na nyumba zote za ibada ziwe na miundombinu bora ya vyoo na sehemu za kunawa mikono,” alisema.

Aliwaagiza wakurugenzi wa halmashauri wahakikishe maeneo yote yanakuwa na huduma hizo muhimu kabla ya Aprili 30, mwakani na itasaidia kuondokana na aibu ya kukosa miundombinu ya usafi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles