29.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

Serikali yasisitiza kunyang’anya viwanda visivyoendelezwa

Na Amina Omari, TANGA

SERIKALI imesema haitasita kuwanyanganya viwanda wawekezaji walioshindwa kuviendeleza na kugeuka magofu jambo linalorudisha nyuma juhudi za uchumi wa viwanda.

Kauli hiyo ilitolewa mjini hapa jana na Naibu Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Stella Manyanya, alipofungua maonyesho ya wajasiriamali Kanda ya Kaskazini yaliyoandaliwa na Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO).

Alisema haiwezekani wawekezaji hao kupewa viwanda halafu wanashindwa kuviendeleza na wanaacha mzigo wa madeni unaolipwa na Serikali pekee.

Alisema viwanda vingine vimejengwa kwa njia ya mikopo huku nia ya Serikali ilikuwa ni kutoa fursa ya ajira na kulipa madeni lakini imekuwa tofauti kwa sababu wawekezaji wameshindwa kuviendeleza huku wakiwa bado wameving’ang’ania.

“Safari hii hatutakuwa na majadiliano. tunawapokonya viwanda hivyo kwa aibu kama umeshindwa kuendeleza ni heri uvirudishe serikalini kimya kimya lakini ukisubiri tutakichukua kwa aibu,” alisema.

Pia alisema viwanda vingi vilichukuliwa kwa uchoyo wakati wa ubinafsishaji lakini watu hawakuwa na uwezo wa kuviendeleza.

“Ukiona ulichukuwa kiwanda kwa hila halafu huna mtaji wa kukiendeleza rejesha ili Serikali iweze kuona namna bora ya kuendesha kiwanda hicho na kusaidia Watanzania kupata ajira,” alisema.

Naye Kaimu Mkurugenzi wa Sido, Joyce Meru, alisema katika kutekeleza sera ya viwanda tayari wametengeneza mashine 1,808 zinazosaidia kuongeza thamani bidhaa zinazozalishwa na wajasiriamali.

Pia walitoa mikopo yenye masharti nafuu ya thamani ya Sh bilioni 1.7 kwa wajasiriamali zaidi ya 2,071 nchini katika kipindi cha mwaka 2017/2018.

Pia alisema kwa sasa wanahitaji wawekezaji katika sekta ya vifungashio ili kuwawezesha wajasiriamali kupata fursa ya kununua vifungashio hivyo hapa nchini badala ya kusubiri hadi kuagiza nje ya nchi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles