22.5 C
Dar es Salaam
Saturday, May 11, 2024

Contact us: [email protected]

MAHAKAMA ZAONGOZA KWA RUSHWA-TWAWEZA

Na NORA DAMIAN-DAR ES SALAAM



UTAFITI uliofanywa na Shirika Lisilo la Kiserikali la Twaweza unaonyesha kuwa bado kuna tatizo kubwa la rushwa katika Jeshi la Polisi na Idara ya Mahakama.

Utafiti huo unaoitwa ‘Hawashikiki’ ulijumuisha wananchi 1,705 wa Tanzania Bara ambao walipigiwa simu kati ya Julai 27 na Agosti 14 mwaka huu.

Katika utafiti huo sekta nyingine iliyotajwa kuongoza kwa rushwa ni ile ya ajira hasa kwa watu wanaotafuta kazi.
Akitangaza matokeo hayo jana, Mkurugenzi Mtendaji wa Twaweza, Aidan Eyakuze, alisema asilimia 60 ya wananchi walisema rushwa ipo katika Jeshi la Polisi wakati asilimia 56 walisema ipo mahakamani.
Utafiti huo ulibainisha kuwa asilimia 39 ya wananchi waliokutana na polisi waliombwa rushwa na asilimia 30 walitoa.

“Aina nyingine ya rushwa iliyoshamiri ni ile inayotolewa wakati wa kutafuta kazi, idadi ya wananchi walioombwa rushwa ni asilimia 36 ambayo imepanda kutoka asilimia 34 mwaka 2014,” alisema Eyakuze.
Alisema pia asilimia 51 ya wananchi walisema posho za vikao kwa watumishi wa umma ni rushwa.

Hata hivyo alisema licha ya serikali kujikita kushughulikia suala la rushwa imeonekana kurudi nyuma katika kuweka mikakati ya kuhakikisha watu hawafanyi vitendo vya rushwa hasa kwa kubana uhuru wa vyombo vya habari na kukataza shughuli za wanasiasa wa upinzani.

“Serikali inafanya vitu vingine vinavyotishia kuathiri jitihada za kupambana na rushwa kama vile kuminya uhuru wa vyombo vya habari, mijadala ya umma na kuiondoa Tanzania kwenye Mpango wa Uendeshaji wa Shughuli za Serikali kwa Uwazi,” alisema.

Mkurugenzi huyo alisema asilimia 85 ya wananchi walisema rushwa imepungua kulinganisha na miaka mitano iliyopita.
“Wananchi wanasema kwa sasa hawakutani sana na vitendo vya rushwa tofauti na ilivyokuwa mwaka 2013, haya ni mafanikio makubwa lakini yanapaswa kwenda sambamba na tahadhari kadhaa.

“Watu wanaweza kudhani rushwa imepungua wanapoona mapambano ya rushwa yamejipatia umaarufu mkubwa na kutawala vyombo vya habari…ni vigumu sana kupima viwango halisi vya rushwa kwa usahihi,” alisema.
Alisema pia wananchi wengi wanaunga mkono mapambano dhidi ya rushwa lakini wanatofautiana kwenye namna ya kuendesha mapambano hayo.

“Asilimia kubwa wanasema ni muhimu haki za msingi za watuhumiwa zikaheshimiwa…kupambana na rushwa kwa kumtafuta mchawi na hukumu za kujionesha ni dalili za serikali ya mabavu,” alisema.
Mkurugenzi huyo alisema asilimia 59 ya wananchi walisema iwapo ushahidi utapatikana utakaomuhusisha rais wa zamani na rushwa asiwekewe kinga au upendeleo wowote.

“Asilimia 49 ya Watanzania wanapenda mwanasiasa mkubwa aadhibiwe kwa kufungwa gerezani iwapo amegundulika kuwa ameiibia serikali Sh milioni 100.

“Hukumu kama hiyo inaungwa mkono kwa askari wa barabarani anayepokea rushwa ya Sh 20,000,” alisema.
Mkurugenzi wa Mipango na Utafiti kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Sabina Seja, alisema bado vitendo vya rushwa vipo kwani wanaendelea kupokea malalamiko.

Alisema mwaka 2014 walipokea malalamiko 5,000 lakini kwa mwaka wa 2016/2017 wameshapokea malalamiko 7,000.
“Kwa mwaka 2017 malalamiko yameonekana kuongezeka lakini pengine ni uelewa wa wananchi kuhusu rushwa au ujasiri wa kuleta taarifa,” alisema Seja.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles