Na PATRICIA KIMELEMETA
-DAR ES SALAAM
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, imeahirisha kesi ya uhujumu uchumi namba 87 inayowahusu wakurugenzi wa kampuni ya Rifaro Africa Limited, Jones Moshi(42) na James Gathonjia(35).
Washtakiwa hao walipandishwa kizimbani na kusomewa mashtaka matatu ikiwamo kuendesha biashara ya upatu na utakatishaji wa fedha Sh bilioni 1.022.
Wakili wa Serikali Neema Mbwana, aliieleza mahakama hiyo mbele ya Hakimu Mfawidhi, Salum Ally kuwa kesi hiyo imekuja kwa ajili ya kutajwa na upelelezi bado haujakamilika na kuiomba kupanga tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.
Hakimu Ally aliahirisha kesi hiyo hadi Januari 10, mwaka huu kwa ajili ya kutajwa.
Washtakiwa hao wanadaiwa kuwa, kati ya Julai 14,2014 na Julai 31, 2016 ndani ya jiji la Dar es Salaam na maeneo mbali mbali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania washtakiwa hao walipanga njama ya kuendesha biashara ya upatu.
Wanadaiwa kuwa katika kipindi hicho na maeneo hayo washtakiwa hao wanadaiwa kuwa waliendesha biashara ya upatu kwa kukusanya fedha kutoka kwa mwananchi kwa ahadi kuwa fedha hizo zitazaa.
Katika shtaka la tatu la utakatishaji wa fedha, washtakiwa hao wanadaiwa kujihusisha na miamala ya Fedha moja kwa moja ya Sh 1,022, 560, 854 kupitia akaunti namba 3301106013 iliyopo katika benki ya Kenya Commercial (T) Ltd (KCB) yenye jina la Rifaro Africa Limited wakati wakijua fedha hizo ni zao la makosa ya kuendesha biashara ya upatu.