Na Veronica Romwald, Dar es Salaam
MAHAKAMA ya Wilaya ya Ilala imemwachia huru mfanyabiashara na mwimbaji wa muziki wa injili, Emmanuel Mbasha aliyekuwa akikabiliwa na kesi ya ubakaji.
Baada ya Hakimu Flora Mjaya kumaliza kusoma hukumu jana, Mbasha alitoka nje ya mahakama hiyo na kupiga magoti na kunyanyua mikono juu akimshukuru Mungu huku akibubujikwa na machozi.
“Namshukuru Mungu ni mwema amenitetea maisha yangu,” alisema Mbasha huku akirudia maneno hayo mara kwa mara.
Hakimu Mjaya alisema mahakama inamwachia huru mshtakiwa kutokana na kukosekana kwa ushahidi wa kutosha dhidi yake kutoka upande wa mlalamikaji.
Katika kesi hiyo, Mbasha ambaye pia ni mume wa mwimbaji maarufu wa muziki wa injili, Flora Mbasha, alidaiwa kumbaka binti mwenye umri wa miaka 17 (jina linahifadhiwa) ambaye ni shemeji yake.
Alidaiwa kumbaka shemeji yake huyo kati ya Mei 23 na 25 mwaka 2013 maeneo ya Tabata, Dar es Salaam ambako alikuwa akiishi naye.
Kesi hiyo ilianza kusikilizwa mahakamani hapo Septemba 5, 2013 ambapo binti huyo aliieleza kuwa alibakwa na shemeji yake (Mbasha) kwa awamu mbili tofauti kabla ya kufanikiwa kukimbia.
Kesi hiyo ilikuwa ikisikilizwa mahakama ya chemba ili kulinda haki ya binti huyo kwa mujibu wa sheria ya mwenendo wa makosa ya jinai ya mwaka 2003 sura ya 20 kifungu cha 186, kifungu kidogo cha tatu.