31.2 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

Yanga yamnyima usingizi Kerr

kerr kazini simba 34JUDITH PETER NA ABDUCADO EMMANUEL DAR ES SALAAM

KOCHA Mkuu wa timu ya Simba, Dylan Kerr, amesema bado ana wakati mgumu wa kupanga kikosi cha kwanza kutokana na ubora na viwango vya wachezaji wake.

Kerr amekiri kuwa pambano la Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya watani wake Yanga litakalofanyika Uwanja wa Taifa,
Dar es Salaam Jumamosi hii litakuwa na upinzani tofauti na mechi ambazo tayari wamecheza.

Kuelekea mchezo huo wa aina yake, Simba itaingia uwanjani ikiwa imeshinda mechi zake tatu za awali walipozivaa African Sports (1-0), Mgambo JKT (2-0) zote Uwanja wa Mkwakwani, Tanga na Kagera Sugar (3-1) iliyofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Ili kujiandaa na pambano hilo la kukata na shoka, Simba wamelazimika kusafiri kwenda Unguja, visiwani Zanzibar
jana kuwafuata Yanga ambao walikwenda kujichimbia kambini huko kisiwani Pemba tokea juzi.

Akizungumza jijini Dar es Salaam mara baada ya mchezo dhidi ya Kagera, Kerr alisema hawezi kujisifia kuwa tayari
amepata kikosi cha kwanza chenye ushindani kwani viwango vya nyota wake vinabadilika mara kwa mara kutokana kila mchezaji kutambua nafasi yake
ndani ya timu hiyo.

Alisema anataka kuona Simba inacheza soka la uhakika lenye muonekano wa kimataifa ili kuendana na viwango vya
uchezaji wa Bara la Afrika na kufikia malengo waliyojiwekea ikiwemo kutimiza ndoto za kutwaa ubingwa msimu huu.

Mwingereza huyo alimsifia kiungo wake Simon Sserunkuma na beki Hassan Ramadhan ‘Kessy’ kwa kuonyesha juhudi na kucheza kwa kujituma huku akimwelezea Msenegal Pape Nd’aw kuwa bado hayupo fiti, hivyo anahitaji muda zaidi wa mazoezi ili aweze kuendana na viwango vya wachezaji wengine.

“Tutakapocheza na Yanga mechi itakuwa tofauti kabisa na zile tulizocheza awali, lakini cha msingi ni kwamba tunaweza kujihamasisha wenyewe na kucheza soka la uhakika lenye ushindani wa hali ya juu mbele ya wapinzani wetu,” alisema.

Kerr pia alilalamikia ubovu wa viwanja na ukosefu wa sehemu za kufanyia mazoezi wakati wakijiandaa na Ligi
Kuu huku akidai amekutana na changamoto kubwa ya kuwaandaa wachezaji wake hasa walipokuwa mkoani Tanga.

Akizungumzia mechi ya juzi dhidi ya Kagera, Kerr alikiri kuzidiwa kipindi cha pili na kudai tatizo halikuwa uchovu wala kutokuwa fiti kwa wachezaji wake, bali ni makosa madogo madogo yaliyojitokeza na hata kuwapa nafasi wapinzani wao kuwafunga.

“Haikuwa kazi rahisi kwetu kucheza mechi tatu za Ligi Kuu ndani ya wiki moja na kufanikiwa kushinda zote, bali
tulikuwa na changamoto kubwa ambapo tulijitahidi kufanya kazi ya ziada ili kupata matokeo mazuri ya kujivunia,” alisema.

Alisema hakumchezesha mshambuliaji Mussa Hassan ‘Mgosi’ dhidi ya Kagera kwa kuwa ana kadi ya njano, huku akiwa na mpango wa kumtumia kwenye mechi ngumu watakapokutana na watani wao wa jadi Yanga Jumamosi.

Wakati huo huo, Yanga imeanza jana kujifua ikiwa kisiwani Pemba kwenye Uwanja wa Gombani huku ikidaiwa kuwa wamewawekea ulinzi mkali nyota wake ili kukwepa hujuma za watani zao Simba.

Huku ikidaiwa kufikia katika Hoteli ya Pemba Misali Sunset Beach, inaelezwa hivi sasa hoteli hiyo haiingiliki hovyo
hovyo kama awali yote hayo ni kuzuia mwingiliano wa watu wa timu hiyo na wengine ambao isiowajua.

“Tumepania sana kuifunga Simba safari hii na tunataka kuwaweka wachezaji wetu kwenye hali nzuri kiakili na kisaikolojia na hatutakua na muingiliano wowote siunajua hii ni mechi kubwa na tunatambua hujuma zote za wapinzani wetu,” kilieleza chanzo chetu kutoka visiwani humo.

Tayari Kocha wa Yanga, Hans van Pluijm, ameshaweka wazi kuwa haihofii Simba na katika maandalizi yake atakayofanya Pemba, ataiandaa timu yake kawaida kama anavyowanoa vijana wake kwenye mechi nyingine.

Yanga nayo imeanza vema ligi ikiwa imeshinda mechi tatu kwa kuzichapa Coastal Union (2-0), Tanzania Prisons (3-0) na JKT Ruvu (4-1), hivyo wadau wengi wanasubiria kuona kama Wanajangwani hao wataweza kulipa kisasi cha kufungwa bao 1-0 dhidi ya Simba msimu uliopita.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles