23.3 C
Dar es Salaam
Sunday, June 16, 2024

Contact us: [email protected]

MAHAKAMA YA HAKI ZA BINADAMU YAIBUKA NA BABU SEYA

Na Eliya Mbonea, Arusha

Wakati mwanamuziki Nguza Viking (Babu Seya) na mwanawe Johnson Nguza (Papii Kocha) wakiwa nje kwa msamaha wa rais, Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu (AfCHPR), imeahirisha kutoa hukumu ya maombi waliyofungua kupinga kifungo cha maisha jela.

Babu Seya na Papii Kocha waliachiwa kwa msamaha wa rais Desemba 9, mwaka jana kutokana na kifungo cha maisha jela walichohukumiwa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam Juni mwaka 2004 baada ya kumkuta na hatia ya kunajisi na kulawiti watoto 10 ambapo walikata rufaa Mahakama za juu na kugonga mwamba na hivyo kulazimika kukimbilia AfCHPR wakidai haki zao zilivunjwa.

Akiahirisha kesi hiyo Rais wa AfCHPR, Jaji Sylvaine Ore kutoka nchini Ivory Cost, amesema wamelazimika kuahirisha kusoma hukumu hiyo hadi Ijumaa Machi 23, kutokana na upande wa waomba maombi kutofika mahakamani.

Katika shauri hilo Jamhuri iliwakilishwa na Mwanasheria wa Serikali Mkuu Sara Mwaipopo akisaidiana na Mwanasheria wa Serikali Mkuu Nkasori Sarakikya.

Hata hivyo, mwanasheria Daniel Kalasha akitoa maoni yake kuhusiana na hukumu hiyo amesema vyovyote itakavyokuwa hukumu hiyo haiwezi kuathiri msamaha wa rais waliopata waomba maombi hao lakini walipaswa kuitaarifu mahakama kuachana na kesi hiyo kutokana na sababu hizo.

Amesema utaratibu ulivyo wao ndiyo walifungua hiyo kesi baada ya kuona wamepata msamaha wa rais walikuwa wanapaswa waiandikie barua mahakama kwamba wameshapata msamaha huo hivyo wanaomba mahakama isitoe hukumu.

“Lakini kama hawakufanya hivyo mahakama itaendelea na kazi yake kama kawaida na aidha itawakuta na hatia au isiwakute na hatia kwamba jambo lao limeshapata msamaha na msamaha wa rais huwezi kuuhoji popote, hakuna mwenye mamlaka ya kuhoji kwa sababu kile kifungo kimeshabatilishwa tayari.

“Kesi ingekuwa bado inaendelea msamaha ukatoka basi wakili ndiyo alikuwa na wajibu wa kuiambia mahakama hatuna nia tena ya kuendelea na rufaa yetu kwa hiyo kesi inakuwa imekufa.

“Lakini hata hivyo halina uzito tena hata kama wakikutwa na hatia tayari wameshapata msamaha wa rais ambao uko kwa mujibu wa katiba,” amesema Kalasha.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
588,000SubscribersSubscribe

Latest Articles