Mahakama ya Juu nchini Uganda imekubaliana na uamuzi wa kuondosha ukomo wa umri wa mgombea urais, na hivyo kumsafishia njia Rais Yoweri Museveni mwenye umri wa miaka 74 kuwania kwa muhula mwengine wa sita.
Mahakama hiyo ilitupilia mbali zuio la wapinzani, ambao waliukatia rufaa uamuzi wa mahakama ya katiba ulioridhia mabadiliko ya katiba yaliyofanywa na bunge.
Katika uamuzi wake hapo jana, Jaji Mkuu Bart Katureebe alitangaza kwamba rufaa hiyo imeshindwa, baada ya majaji wanne kuitupilia mbali dhidi ya watatu walioiunga mkono. Mwezi Disemba 2017, Rais Museveni – ambaye amekuwa madarakani tangu mwaka 1986 – aliusaini muswaada wa sheria kuondosha ukomo wa umri kwa wagombea urais, na hivyo kuashiria kuwa angeliwania tena mwaka 2021