NA MAGRETH KINABO-DAR ES SALAAM
MAHAKAMA ya Tanzania kupitia mpango mkakati wake wa miaka mitano wa 2015- 2020, inatarajia kujenga kituo maalumu ikiwa ni hatua ya kupanua wigo wa huduma kwa watu wenye mahitaji maalumu.
Kuanzishwa kwa kituo ni hatua ya kuwapunguzia wananchi gharama za fedha wanazozitumia, muda wanaoutumia na utoaji wa haki kwa wakati.
Kauli hiyo ilitolewa hivi karibuni na Mwenyekiti wa Mkutano wa Mashauriano kuhusu uanzishaji Kituo Maalumu cha kushughulikia masuala ya mirathi ambaye ni Msajili ya Mahakama Kuu ya Tanzania, Ilvin Mugeta.
“Tuna mpango wa kuanzisha kituo hicho cha huduma za mahakama kuhusiana na masuala ya mirathi, ambacho kitakuwa na wadau mbalimbali wa Mahakama ya Tanzania kuhakikisha huduma za mirathi zinatolewa kwa wakati bila kupoteza muda na gharama,” alisema.
Alisema kituo hicho pia kitasaidia kupunguza mlundikano wa kesi zilizokaa muda mrefu mahakamani, ikiwa ni moja ya mkakati wa mahakama wa kupitia mpango huo.
“Katika mpango huo mahakama inatarajia kujenga kituo cha pamoja kitakachoshughulikia masuala ya mirathi.
“Hivyo huduma hizo zitakuwa zinapatikana kwenye jengo moja kuwaondolea usumbufu watu wanaohitaji huduma za mahakama,” alisema Mugeta.
Alisema kituo hicho kitakuwa na huduma za Mahakama ya Mwanzo, Mahakama ya Wilaya na Mahakama Kuu na kusaidia watu wanaohitaji huduma hiyo kupatiwa haki zao kwa wakati.
Kituo hicho cha pamoja kinatarajiwa kuanza kufanya kazi Dar es Salaam mwaka 2019 katika Wilaya ya Temeke karibu na Kituo cha Polisi Chang’ombe , eneo ilipo Mahakama ya Mwanzo Temeke.