MGHWIRA ANG’OLEWA UENYEKITI ACT

0
413
Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Anna Elisha Mghwira akila kiapo cha Uadilifu kwa Viongozi Ikulu jijini Dar es Salaam.

 

 

Na ELIZABETH HOMBO-DAR ES SALAAM

CHAMA cha ACT-Wazalendo, kimemvua uongozi Mwenyekiti wake, Anna Mghwira kwa kile kilichodai kuwa hawezi kutekeleza majukumu yake ya chama kwa ufanisi.

Chama hicho kimesema, kimefikia uamuzi huo baada ya kushauriana na Mghwira pamoja na viongozi wenzake wakuu wa chama.

Juni 3 mwaka huu, Rais Magufuli alimteua Mghwira kuwa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, uteuzi ambao ulizua maswali na kuleta mshtuko kutokana na cheo alichopewa tofauti na ubunge.

Kutokana na uamuzi huo, gazeti hili lilimtafuta RC Mghwira kupitia simu yake ya kiganjani, ambapo ilipokelewa na mmoja wa wasaidizi wake huku akisema apigiwe baadaye.

Hata hivyo hadi gazeti hili linakwenda mtamboni simu ya RC Mghwira haikupatikana tena hewani.

Juzi, RC Mghwira aliliambia MTANZANIA kuwa hana mpango wa kuachia nafasi yake ya uenyekiti wa ACT na kwamba anachoangalia kwa sasa ni kusimamia shughuli za maendeleo kwa faida ya Watanzania.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Kaimu Kiongozi Mkuu wa chama hicho, Samson Mwigamba alisema kwa mujibu wa katiba ya ACT- Wazalendo, Mghwira amekoma kuwa mwenyekiti wa chama hicho.

 “Kwa mujibu wa ibara ya 17(1)(iii) ya katiba ya ACT na kutokana na mashauriano kati ya mama Anna Mghwira na viongozi wenzake wakuu wa chama, amekoma kuwa mwenyekiti wa chama chetu.

“Ibara hii inasema iwapo kiongozi wa chama atashindwa kutekeleza majukumu yake atakoma kushika nafasi yake. Ni dhahiri kuwa kuteuliwa kwake kuwa Mkuu wa Mkoa, hawezi tena kutekeleza kwa ufanisi wajibu wake,” alisema Mwigamba.

Kwa mujibu wa ibara ya 29 (24) ya katiba ya ACT, Kamati ya Uongozi  imemteua Yeremia Kulwa Maganja kuwa kaimu mwenyekiti wa chama hicho hadi Uchaguzi Mkuu utakapoitishwa Machi mwaka 2018.

Mwigamba alisema kamati hiyo imemshauri Rais Dk. John Magufuli, kuweka mfumo bora wa kuazima watu kutoka vyama vingine kwa kufanya mashauriano na vyama husika, ili kuepuka migongano isiyo ya lazima.

“Pamoja na kwamba Rais kama mkuu wa nchi anayo mamlaka ya kumteua yeyote amtakaye, lakini afya na hekima ni vema teuzi hizo kufanywa kwa kushauriana na viongozi wa vyama husika ambavyo anachukua wanachama wake.

“Hii haitakuwa kuingilia mamlaka yake ya kikatiba bali kuimarisha umoja wa kitaifa na hata mfumo wa vyama vingi nchini.

“Kuteua bila ya mashauriano kunaleta wasiwasi wa dhamira mbaya na kuathiri taswira ya vyama vya upinzani ambavyo Rais anachukua wanachama wake,”alisema.

Pia alimpongeza Rais Magufuli kwa kuvunja miiko ya siasa za hapa nchini, kwa kuanza kuteua wapinzani na kuwaingiza katika utumishi wa umma (Serikali).

Alisema uteuzi wa mara ya pili wa Rais kwa wanachama na viongozi wa ACT ni uthibitisho kuwa chama hicho kinapaswa kupewa nafasi ya kuongoza nchi katika uchaguzi ujao.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here