20.9 C
Dar es Salaam
Saturday, June 15, 2024

Contact us: [email protected]

Magufuli, Lowassa wakwepana tena

1Na Veronica Romwald, Dar es Salaam

WAZIRI Mkuu mstaafu Edward Lowassa, kwa mara nyingine tena amekwepa kukutana ana kwa ana na Rais Dk. John Magufuli.

Tukio hilo linatokea ikiwa ni mara ya pili tangu ulipomalizika Uchaguzi Mkuu Oktoba 25, mwaka jana.

Kwa mara ya kwanza, Lowassa ambaye ni kada wa zamani wa CCM, alikwepa kuonana na Rais Magufuli katika ibada ya Sikukuu ya Pasaka iliyofanyika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Azania Front, Machi 27, mwaka huu.

Hali hiyo ni kinyume cha matarajio ya watu wengi ambao walisubiri kwa hamu kuwaona mafahari hao wawili wa kisiasa wakikutana kwa mara ya kwanza tangu ulipomalizika mchakato wa kumpata mgombea urais ndani ya CCM mjini Dodoma.

Jana, wakati watu wakitarajia tena kuwaona wakikutana kwenye shughuli ya kuaga mwili wa marehemu Christina Lissu, aliyekuwa mbunge wa Chadema katika Bunge la 10, Lowassa hakuhudhuria na kumwacha Rais Magufuli akiwaongoza waombelezaji kuaga mwili huo.

Shughuli hiyo ilifanyika katika Ukumbi wa Karimjee, Dar es Salaam ambapo mbali na Rais Magufuli, viongozi wengine waliohudhuria ni pamoja na Waziri Mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye, Naibu Spika wa Bunge, Dk. Tulia Akson pamoja na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), George Simbachawene.

Msafara wa Rais Magufuli uliwasili katika viwanja vya Karimjee saa 7:30 mchana na kupokewa na viongozi mbalimbali wa Chadema waliokuwa wakiongozwa na Mwenyekiti Freeman Mbowe ambaye pia ni Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni.

MTANZANIA ilipomtafuta msaidizi wa Lowassa, Abubakary Liongo kwa simu yake ya kiganjani, hakupatikana hadi tunakwenda mitamboni.

 

MBOWE

Akizungumza wakati wa shughuli hiyo ya kuuaga mwili wa Christina, Mbowe alisema ingawa marehemu ambaye ni dada wa mwanasheria mkuu wa Chadema na Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu alikitumikia chama kwa muda mfupi, lakini amefanya kazi njema.

“Sijui nitumie maneno gani kumshukuru Mungu kwa ajili ya Christina ambaye leo hii amempenda zaidi… hajakitumikia chama sana, lakini ametenda vyema. Nilishangaa amefanya kazi bila kulalamika ingawa alikuwa mgonjwa, hii inamaanisha alikuwa mvumilivu. Hivyo tujiulize sisi tuliobaki tunaacha alama ipi ya kujenga umoja kama Taifa na viongozi,” alisema Mbowe.

 

SIMBACHAWENE

Akitoa salamu za rambirambi za Serikali kwa niaba ya Rais Magufuli, Waziri Simbachawene alisema Serikali ilishtushwa na taarifa za kifo hicho, na kwamba ipo bega kwa bega na familia ya marehemu katika kipindi hicho cha majonzi.

“Tulishtushwa na taarifa hizi… Christina tunautambua uwezo wake, alikuwa mtendaji, tena mwenye uwezo mkubwa wa kusimamia kile anachokifanya, tutaendelea kukumbuka utendaji kazi wake. Hii iwe nafasi kwa kila mmoja wetu kutafakari utendaji kazi wake,” alisema.

 

  1. TULIA

Kwa upande wake, Naibu Spika wa Bunge, Dk. Tulia Akson alisema: “Ingawa sijawahi kufanya naye kazi na hakuweza kurudi katika Bunge la 11, lakini nimepata kusoma habari zake na hata nyingine zimezungumzwa hapa, ni wazi kwamba tumempoteza mtu muhimu ambaye alikuwa na uwezo wa kujenga hoja na kuisimamia.”

 

LISSU

Awali akisoma wasifu wa marehemu, Tundu Lissu alisema kuwa alizaliwa Juni 26, 1969 katika Kijiji cha Ikungi mkoani Singida, lakini imempendeza Mungu kumchukua katika wiki ile ile ambayo pia alimchukua mama pamoja na mjomba wao Aprili, 4.

“Katika taarifa zilizoandikwa kwenye kitabu cha kumbukumbu ya historia ya familia yetu, Christina alizaliwa saa 10 jioni, ilikuwa kijijini na kwa kuzingatia hali za huduma za afya wakati huo, ni muujiza kuwa naye kwani alizaliwa miezi mitatu kabla ya muda wake… mama alikuwa akimuanika juani na zoezi hilo liliendelea kwa miezi kadhaa hadi alipopata nguvu, kila familia kubwa ina mgonjwa wake.

“Pengine kwa sababu ya mazingira ya kuzaliwa kwake alikuwa akiugua kila mara, alikuwa na tatizo la sikio na akafanyiwa upasuaji, alikuwa akisumbuliwa na kikohozi kisichoisha kwa muda mrefu, lakini bado alikuwa na dhamira kubwa ya kufanikiwa maisha na alikuwa mshindani mkubwa darasani,” alisema.

Akiendelea kusoma wasifu huo, Lissu alisema Christina alikuwa mwanasiasa mashuhuri na kielelezo cha kuwakomboa wakina mama kutoka kwenye mila na desturi kandamizi, alikuwa akilea mtoto wake peke yake baada ya mumewe kufariki, alikuwa mfano wa ujasiri wa wanawake akikabiliana na magumu yote.

“Ugonjwa wa saratani umemwangusha, lakini imedhihirisha pia ujasiri wake maana alipambana kwa kila hali,” alisema.

Alisema Christina alisoma katika Shule ya Msingi Mahabe 1978 hadi 1984, alijiunga Sekondari ya Weruweru 1985 hadi 1988, Masomo ya juu ya sekondari ya Kilakala 1989 na 1991, mafunzo ya kijeshi kwa mujibu wa sheria 1991 hadi 1992 na 1993 alijiunga na Kitivo cha Sanaa na Sayansi Jamii Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Lissu alisema kuwa Christina aliajiriwa katika Benki ya Posta 1998, baadae alihamishiwa Mwanza kama meneja wa ghala la kampuni hiyo, 2004 aliajiriwa na Serikali katika Bohari Kuu ya Dawa (MSD) kama ofisa mauzo na baada ya miaka mitatu alihamia kwenye mradi wa kuchangia sekta ya afya (bima) uliokuwa unafadhiliwa na USAID hadi Septemba, mwaka 2010 alipoingia kwenye siasa.

Alisema kuwa mwili wa marehemu unatarajiwa kuzikwa leo katika Kijiji cha Mahambe mkoani Singida.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
588,000SubscribersSubscribe

Latest Articles