31.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, December 11, 2024

Contact us: [email protected]

Mbunge: Zanzibar si shwari

Mwinyi_AbdullahNA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM

MWENYEKITI wa Kamati ya Usuluhishi na Migogoro wa Bunge la Jumuiya la Afrika Mashariki (EALA), Abdullah Ali Mwinyi, amesema hali ya kisiasa Zanzibar si shwari, hivyo ni vema viongozi wa pande zote kukutana pamoja na kutafuta suluhisho kwa njia ya mazungumzo

Amesema pamoja na kumalizika kwa uchaguzi wa marudio uliofanyika Machi 20, mwaka huu  na Dk. Ali Mohamed Shein, alitangazwa mshindi kwa kupata asilimia 91.4 ya kura zilizopigwa, bado kuna ulazima wa kutafuta mwafaka.

Kauli hiyo aliitoa jana Dar es Salaam baada ya wabunge wa EAC kutoka Tanzania, kutembelea ofisi za Kampuni ya New Habari (2006) Ltd zilizopo Sinza Kijiweni, ambapo pamoja na kuelezea mafanikio kadhaa ya jumuiya hiyo, waliulizwa kuhusu hatima ya hali ya kisiasa Zanzibar.

Akijibu swali hilo, Mwinyi alisema suala la hali ya kisiasa Zanzibar lipo bayana na kila mtu anajua, kinachotakiwa ni kutatuliwa kwa njia ya mazungumzo, hasa baada ya kukamilika kwa uchaguzi huo ambao CCM wameshinda nafasi zote.

“Ni lazima tukiri Zanzibar si shwari, hilo liko bayana. Tatizo la Zanzibar ni la kisiasa na mazungumzo japo sina shaka uchaguzi umemalizika, tunaamini viongozi wa juu wataliangalia hili kwa ngazi yao pamoja na kuchukua hatua za pamoja.

“CUF walisusia uchaguzi kama tunavyojua, na CCM pamoja na baadhi ya vyama vilishiriki na hatimaye Rais amepatikana. Kwa mantiki hiyo ilikuwa ni ngumu kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) kama Katiba inavyotaka, maana kama angefanya hivyo Rais Dk. Shein, pia ungeibuka mjadala wa kuvunja katiba.

“Na pia hakuna chama kilichofisha asilimia 10 ya kura, kwa maana hata Hamad Rashid amepata asilimia tatu tu na alichokifanya Rais Dk. Shein si kibaya kuwashirikisha baadhi ya waliokuwa wagombea urais kuingia katika Serikali,” alisema Mwinyi.

Alisema pamoja na Katiba ya Zanzibar kuweka vigezo katika uundaji wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK), ilimlazimu Dk. Shein kufanya hivyo kwa kuwa na Serikali ya upande mmoja pekee.

“Nina imani mazungumzo yataendelea, hasa kwa viongozi wa juu kwa kuangalia mazingira ya Zanzibar,” alisema.

 

KIMBISA

Akizungumzia hali hiyo kwa upande wake, Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA), Adam Kimbisa, alisema CCM ilishinda kwa kishindo na kilichobaki ni kujenga nchi.

“CCM ilishinda kwa kishindo na kilichobaki ni kujenga nchi maana hawa wengine wanachokifanya sasa ni kuleta fujo,” alisema Kimbisa ambaye ni pia Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM

 

MAAMUZI YA MCC

Bodi ya Shirika la Changamoto za Milenia (MCC) la Marekani ilitangaza Machi 28, mwaka huu kwamba inasitisha msaada wa dola milioni 473, karibu sawa na Sh trilioni moja kwa Tanzania kutokana na kutoridhishwa na uchaguzi wa marudio wa Machi 20 visiwani Zanzibar pamoja na utekelezaji wa Sheria ya Mtandao.

Fedha hizo zililenga kupanua upatikanaji wa umeme wa uhakika na kuisaidia Tanzania itekeleze mpango kabambe wa mageuzi ya sekta ya nishati.

Aprili 4, mwaka huu, taarifa ya shirika hilo ikaeleza kuwa Tanzania ndiyo itakayoamua hatua za kuchukua ili kuiwezesha irudishiwe msaada huo ulioondolewa kuishinikiza kushughulikia mambo hayo.

“Serikali ya Tanzania inahitaji kuamua namna itakavyoshughulikia masuala ya wasiwasi yaliyoifanya iondolewe katika mpango wa kuisaidia,” Renee Kelly, msemaji wa MCC alisema kupitia ujumbe wa barua pepe.

“Ni juu ya Bodi ya MCC pia kuamua iwapo hatua hizo zitakazochukuliwa na Serikali ya Tanzania zitatosha kuirudisha katika mpango wa shirika hilo.”

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles