>>Magufuli asema yeye ndiye mshindi
>> Lowassa atamba kupata ushindi mnono
NA FREDY AZZAH, HANDENI
MGOMBEA urais wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Edward Lowassa, amesema ana uhakika wa kushinda kwa asilimia 80, na kwamba atakuwa rais wa mabadiliko na si maneno.
Lowassa ambaye anaungwa mkono na Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), aliyasema hayo jana katika mkutano wa kampeni uliofanyika kwenye Uwanja wa Kigoda CCM, Wilaya ya Handeni mkoani Tanga.
“Kuna watu wanasema nitapita kwa asilimia 50 au 60 hivi, lakini kwa hali niliyoiona vijijini na mijini, naona nitapata asilimia 80.
Naomba mfanye kweli nipate hizo asilimia kwa sababu nitakuwa rais, si rais wa maneno, nitakuwa rais wa
mabadiliko.
“Nimeongoza haya mabadiliko kwa heshima, nataka niongoze taifa hili kwa heshima pia, ili wajue tunaweza kuwa bora kuliko mataifa mengi duniani na hatimaye tuachane na umasikini ambao mimi nauchukia,” alisema Lowassa.
Ili kuhalalisha ushindi wake huo, aliwataka wafuasi wake kumpigia kura kwa wingi ili hata kama baadhi zitaibwa, aweze kushinda.
“Tumechoka na miaka 54 ya CCM, Tanzania bila CCM inawezekana, tuonyeshe kazi,” alisema Lowassa. Kuhusu Jeshi la Polisi, alisema kwa sasa wanawakamata ovyo vijana wanaoonyesha mapenzi kwa Chadema, jambo ambalo alisema
linaweza kusababisha vurugu nchini.
“Nimeona jana Tanga na maeneo mengine kuna tabia imeanza ya kukamata vijana wa Chadema. Nawaambia Serikali waache, wanachochea fujo, vijana hawa ukiwachokoza utaanzisha fujo.
“Sisi tuna hakika ya kushinda asubuhi kweupe, kwahiyo, hatuna sababu ya kufanya fujo, na waache vitisho vya aina yoyote,” alitahadharisha Lowassa.
SUMAYE
Waziri Mkuu wa zamani, Fredrick Sumaye, akizungumzia suala la polisi, alisema vijana wanaobeba bendera za Chadema wakionekana wakiwa wamefuatana hata kama ni watatu, wanakamatwa, lakini wanaobeba bendera za CCM, hata wakiwa wengi kiasi gani hawaguswi.
“CCM hata wakiwa 50 hawakamatwi, waendelee tu kuwapiga, lakini kwenye kura watapiga bomu la machozi?
“Jumapili ndiyo siku ya sisi kuamua kujikomboa na matatizo ama kuendelea nayo maisha yetu yote, hii ndiyo nafasi Mungu aliyotupa, tuitumie vizuri,” alisema Sumaye.
Msafara wa Lowassa ulipokuwa Kilindi, mkoani Tanga, Meneja Kampeni wa Chadema, John Mrema, aliwataka wanawake wasimchague mgombea urais wa CCM, Dk John Magufuli kwa sababu hajui matatizo yao.
Alimshangaa Dk. Magufuli kutomtumia mkewe majukwaani kama ambavyo mke wa Lowassa, Regina Lowassa anavyopanda majukwaani kumwombea kura mumewe,” alisema Mrema.
MSAFARA WASIMAMISHWA
Awali wakati magari ya msafara wa Lowassa yakitoka Tanga Mjini kuelekea Handeni, yalisimamishwa na mamia ya wananchi waliokuwa wamesimama eneo la Muheza.
Wananchi hao walisimamisha magari hayo wakidhani yumo Lowassa ambaye alikuwa ametangulia Handeni kwa kutumia helkopta.
Wakati Lowassa akitoka Tanga Mjini kwenye mkutano wa kampeni uliovunjika hivi karibuni kutokana na uwanja kuzidiwa na watu, alifanya mikutano ya kampeni kwenye eneo hilo na kumnadi mgombea ubunge na madiwani.