29.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

…Magufuli, Dau siri nzito

dauNA MWANDIASHI WETU, DAR ES SALAAM

RAIS John Magufuli anaonekana kuwa na siri nzito dhidi ya aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Hifadhi ya Jamii (NSSF), Dk. Ramadhan Dau.

Katika siku za karibuni, Dk. Dau amekuwa akituhumiwa kutumia vibaya ofisi yake na kulisababisha hasara ya mamilioni ya fedha shirika hilo kutokana na kuingia mikataba ya miradi mingi.

Kutokana na hali hiyo, wiki kadhaa zilizopita, taarifa zilizagaa mitaani kuwa Dk. Dau alihojiwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), japo si yeye wala kiongozi wa taasisi hiyo aliyekuwa tayari kuthibitisha taarifa hiyo.

Februari 15, mwaka huu, Rais Magufuli alitengua uteuzi wa Dk. Dau kisha akamteua kuwa balozi, ingawa hadi sasa hajampangia nchi ya kwenda.

Lakini jana, wakati wa ufunguzi wa daraja la Kigamboni, Rais Magufuli alimwita Dk. Dau na kumpa nafasi kuelezea mradi huo, licha ya kutowekwa kwenye ratiba ya wazungumzaji.

Jambo hilo liliibua hisia za aina yake kwa watu waliohudhuria ufunguzi wa daraja hilo.

Rais Magufuli alisema Dk. Dau ni miongoni mwa watu muhimu ambao wamefanikisha ujenzi wa daraja hilo ambalo mchakato wake ulianza akiwa mkurugenzi wa shirika hilo.

“Wakati fulani alikuja kwangu akiwa ‘flatrated’, wakati ule nikiwa Waziri wa Ujenzi nikamwambia ‘endelea nimeweka kifua mbele’. Watanzania huwa tunasahau, lakini ukweli mnyonge mnyongeni, haki yake mpeni,” alisema Rais Magufuli.

Kitendo hicho kinaonyesha Rais Magufuli ana siri nzito kwa Dk. Dau, kwani ni jambo ambalo halikutegemewa kwa kuwa alitengua uteuzi wake kwa madai ya kuisababishia NSSF hasara ya mabilioni ya fedha tangu alipoteuliwa kuongoza shirika hilo 1997.

Alipopewa nafasi ya kuzungumza na Rais Magufuli, Dk. Dau alisema: “Nashukuru kwa fursa hii kwa sababu sikupangwa kwenye ratiba kuwa mmoja wa wazungumzaji leo (jana), umetambua mchango tulioutoa ukanipa nafasi.

“Sikujipanga kuzungumza lolote, kwa ufupi ni kwamba NSSF tulidhamiria kujenga daraja hili mwaka 2012 tulipokwenda Mkuranga na Rais mstaafu Benjamin Mkapa, ambako tulizindua hospitali ambayo tuliijenga.”

Alisema anashukuru kupata nafasi ya kuhitimisha ndoto iliyokuwapo tangu enzi za mkoloni ya kujengwa kwa daraja hilo.

“Hivyo ni vyema daraja hili liwe chachu kwa mifuko mingine ya hifadhi ya jamii kujenga miradi mingine ya uwekezaji ambayo itaigusa jamii moja kwa moja na hatimaye kukuza pato la Taifa.

“Hata kitabu kitakatifu cha Quran kimeandikwa katika mambo ya kheri washindane wanaoweza kushindana, tujielekeze huko katika kushindana ili kusukuma mbele maendeleo ya Taifa,” alisema.

Baada ya Dk. Dau kumaliza kuzungumza, Rais Magufuli aliendelea na hotuba yake ambapo alisema awali Serikali ya Uingereza ilitaka kujenga daraja hilo, wakati Tanzania ilipokuwa koloni lake mwaka 1933, lakini walishindwa kutokana na kukosa fedha.

“Mwaka 1976, Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere katika awamu yake ya kwanza walianza kupanga mikakati ya ujenzi wa daraja hili, pia walishindwa kwa kukosa fedha, palikuwa na juhudi za makusudi za kulijenga katika awamu zote tangu wakati ule wa mkoloni.

“Nimebahatika kujua historia hii kwa sababu kwa miaka 20 nimekuwa serikalini na kwa miaka 15 nimekuwa waziri. Hata katika ‘master plan’ ya Jiji la Dar es Salaam mji wa Kigamboni umewekwa ‘mastered’, kama si kujengwa daraja hili basi hata stendi mpya ya Mtwara inayotarajiwa kujengwa isingejengwa kabisa,” alisema.

 

LIITWE DARAJA LA NYERERE

Rais Magufuli alisema ni vyema daraja hilo likaitwa Daraja la Nyerere ili kumpa heshima kiongozi huyo.

“Kuna madaraja mengi yamejengwa, lipo la Mkapa, Kikwete, Umoja na mengine yanazidi kujengwa. Waziri wa Ujenzi (Profesa Makame Mbarawa) alinifuata na kuniomba daraja hili liitwe kwa jina langu, nikakataa.

“Kwa sababu mawazo ya kujenga daraja hili yalianza tangu enzi ya mkoloni, sistahili sifa yoyote kwa sababu mimi nilitimiza wajibu wangu kama mtumishi wenu (wananchi). Sikupenda liitwe jina langu, si zuri (Magufuli) halileti raha,” alisema Rais Magufuli jambo ambalo lilisababisha watu waliokuwapo kuangua kicheko.

“Ni vyema liitwe Daraja la Nyerere, nina uhakika wizara itafanya utaratibu kwa heshima kubwa ya Hayati Baba wa Taifa.”

 

LILIVYOPATIKANA ENEO LA MRADI

Akikumbushia namna walivyopata eneo hilo, Rais Magufuli alisema walilazimika kuwaondoa wananchi ambao walikuwa wamejenga makazi yao.

“Tulitenga Sh bilioni 13 kwa ajili ya fidia, tulipowapa walidai fidia ilikuwa ndogo, ilifika mahali tulilazimika kuwaondoa kwa nguvu na wakakubali kuchukua fedha zile, hii ina maana ili kupata maendeleo ni lazima pawe na kutoka jasho,” alisema.

 

MATUMIZI

Alisema ni vyema NSSF ikakaa na kupanga kiasi watakachokuwa wakiwatoza wananchi wanaotumia vyombo vya usafiri kuvuka katika daraja hilo.

“Watembea kwa miguu waruhusiwe kupita bure katika hatua hii ya awali hadi hapo mtakapokaa na kutafakari vingine, magari, pikipiki, baiskeli, guta hizo zilipie gharama. Lazima watu walipie maana mradi huu umejengwa kwa ushirikiano na sekta binafsi (PPP).

“Hata maharusi ambao watahitaji kupiga picha za kumbukumbu katika daraja walipie, watakaokuwa wanasimama simama nao watozwe fedha. Mzee bure alishakufa, hizi fedha lazima zirudi ziende zikajenge miradi mingine, hata wenzetu Wachina walifanya hivyo na wakafanikiwa,” alisema.

 

KUAJIRI WAFANYAKAZI 300

Rais Magufuli alisema kuzinduliwa kwa daraja hilo kunatoa fursa ya ajira kwa watu wapatao 300 hatua ambayo inatimiza ahadi yake ya kutengeneza fursa za ajira kwa Watanzania.

“Kuna kamera zimefungwa hapa kwa ajili ya usalama, na usafi lazima uendelezwe katika eneo lote,” alisema.

 

ULINZI

Rais Magufuli alitaka kila mwananchi kuwa mlinzi wa mwenzake, huku akivitaka vyombo vya usalama kuweka adhabu kali kwa mtu atakayebainika kuharibu miundombinu ya daraja hilo.

“Kamera zilindwe, vyombo vya ulinzi viweke adhabu kali ili mtu akigonga hata nguzo moja aadhibiwe maana vinginevyo zitapoteza ‘stability’ na ile ‘central gravity’, watu waheshimu, tunahitaji maendeleo na daraja hili limejengwa kwa gharama kubwa,” alisema.

 

MACHINGA

Rais Magufuli aliwapiga marufuku vijana wanaopenda kupanga bidhaa zao barabarani au kutembeza maarufu kama machinga kufanya hivyo katika daraja hilo.

“Niliona mmeanza kupanga bidhaa, ni marufuku, aidha mpange kule mwanzo wa daraja au mwisho, si katikati ya daraja, matokeo yake watajaa vibaka kama kule Manzese,” alisema.

 

VIVUKO

Alisema wakati umefika wa vivuko vya Mv Kigamboni na Mv Magogoni kupumua kwa kupumzishwa ili vifanyiwe matengenezo.

“Ni wakati vivuko kupumua… pandisheni hata bei kule ili wananchi wahamie huku, naamini mtajenga vituo vya daladala karibu ili watu wasitembee sana, lifanikisheni mapema maana viongozi wote mpo hapa,” alisema.

 

UVUMILIVU

Rais Magufuli aliwashukuru wakazi wa Kigamboni kwa uvumilivu wao kwa sababu muda mrefu wamekuwa wakipata tabu ya usafiri.

Alisema pamoja na matatizo yote, wameweza kuleta maendeleo na kumpigia kura zilizochangia kushinda Uchaguzi Mkuu kwa kishindo mwaka jana.

“Nawashukuru mno wakazi wa Kigamboni kwa uvumilivu wenu, hii ni wilaya mpya na jimbo jipya, wakati wa kampeni niliwaahidi sitawaangusha na leo narudia tena sitawaangusha, nilifurahi nilipokaribishwa kuja kuzindua daraja hili na kuambiwa kuwa sherehe hizi zitafanyika hapa.

“Kwa muda mrefu mlikuwa mkipata shida ya usafiri na wengine (wanasiasa) walitaka kuitumia nafasi hiyo kupata kura, lakini bado mliniamini mkanipa, tena za kutosha. Asanteni… lengo la Serikali ya awamu ya tano kama zile zilizopita ni kutatua kero za wananchi ingawa najua haziwezi kuisha, tutajitahidi kuzitatua kama si kuzimaliza kabisa,” alisema.

 

AMPONGEZA MKANDARASI

Katika hatua nyingine, Rais Magufuli alimpongeza mkandarasi wa daraja hilo ambayo ni Kampuni ya  China Railway Construction Engineering Group, iliyotekeleza mradi huo kwa kushirikiana na Kampuni ya China Railway Major Bridge Group kutoka nchini China kwa kukamilisha mradi huo kwa ubora na viwango.

“Kufuatia kazi nzuri iliyofanywa na wenzetu hawa kutoka nchini China, napenda kutumia fursa hii kuahidi kwa niaba ya Serikali kuwa tutaendeleza ushirikiano wetu katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ikiwemo kumalizia kipande cha barabara kinachounganisha daraja hili kutoka upande wa Kigamboni,” alisema.

Alisema kampuni hiyo imefanikisha ujenzi huo wa daraja lenye urefu wa mita 360, na barabara zenye urefu wa kilometa 2.5 kila upande pamoja na ‘fly-over’ ndogo, na naamini hata ile ya kilometa 1.5 wataimaliza kwa wakati.

“Naamini hawatashindwa kwa sababu wameweza kumaliza kunyoa kichwa watashindwaje kunyoa ndevu? Watamaliza na Kigamboni utakuwa mji wa kisasa,” alisema.

 

UJENZI WA BARABARA                

Katika hatua nyingine, Rais Magufuli aliagiza kupanuliwa haraka barabara ya Mbagala Rangitatu hadi Gerezani na kwamba pawe na mpango wa haraka wa ujenzi wa barabara itakayoweza kupitia bandarini kutokea Kituo Kikuu cha Polisi ili watu wafike haraka katika vituo vyao vya kazi.

 

APIGA VIJEMBE

Rais Magufuli hakuacha kuwatupia vijembe wapinzani wake, ambapo alisema ingawa jitihada zimefanyika kukamilisha ujenzi huo, wapo watakaojitokeza na kuzipinga, japo hakuwataja.

“Niliona mtu mmoja anaongea na kusema eti halijajengwa vizuri…. si ukajenge la kwako, daraja hili ni ukombozi kwa wananchi na litakaa kwa muda wa miaka 100, hivyo vizazi vitanufaika nalo,” alisema.

 

WAZIRI NGONYANI

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Edwin Ngonyani, alisema katika mwaka wa fedha 2016/17, Serikali imedhamiria kujenga barabara nyingi zaidi.

“Katika mwaka huo wa fedha Serikali imeongeza bajeti kutoka kati ya asilimia 26 au  27 hadi asilimia 40 katika miradi mbalimbali ya maendeleo, hasa ujenzi wa barabara ambapo kuanzia Mei, mwaka huu tutaanza na ‘fly-over’ ya kutoka Kibada hadi Feri,” alisema.

Alisema pia mchakato wa ujenzi wa barabara ya aina kama hiyo kutoka Dar es Salaam hadi Chalinze mkoani Pwani unaendelea vizuri.

“Barabara hiyo itatoka Dar es Salaam kupitia Tuangoma, Mbagala, Kisarawe, Mlandizi hadi Chalinze na itakuwa na umbali wa kilomita 128. Tutajenga pia barabara ya kutoka Uhasibu, Kawawa hadi Nyerere kwa ushirikiano na Benki ya Maendeleo ya Afrika,” alisema.

Alisema fly-over ya Ubungo itajengwa na Serikali kwa kushirikiana na Benki ya Dunia, daraja la Salender litajengwa kwa kushirikiana na Korea Kaskazini na kwamba upembuzi yakinifu unaendelea kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya Mwenge (fly-over), Magomeni, Kamata na Buguruni.

 

KIJANA AKAMATWA

Wakati Rais Magufuli akielekea kukata utepe, kijana mmoja ambaye jina lake halikufahamika mara moja alijikuta matatani na kushikiliwa na watu wa usalama baada ya kutaka kumkabidhi Rais karatasi aliyokuwa ameibeba akidai kuwa ni barua ambayo angependa akaisome.

 

MEYA WA JIJI

Awali kabla ya hotuba ya Rais, Makonda alimkaribisha Meya wa Jiji, Isaya Mwita (Chadema) ambaye naye alihudhuria sherehe hizo kuzungumza na wananchi jambo ambalo liliamsha shangwe katika eneo hilo.

Akizungumza, Meya Mwita alisema Rais Magufuli alimtendea haki kwa kumpatia nafasi hiyo ya kuzungumza kwani alipopata nafasi ya kugombea alisema nchi inahitaji umoja.

“Baada ya kampeni za mwaka jana, siasa zilisimama, sasa ni kipindi cha kufanya kazi na kujenga Taifa. Lakini tukienda na mtindo wa kugombania mbao hatufiki, ni lazima tumsaidie Rais Magufuli, lakini hatuwezi kujenga Dar es Salaam kama hatuna pato la ndani ambalo linatokana na kodi zinazokusanywa,” alisema.

Alisema mara nyingi watu wanaomiliki majengo wamekuwa wakikwepa kulipa kodi jambo ambalo linachelewesha maendeleo ya jiji hilo.

 

MEYA WA TEMEKE

Kwa upande wake, Meya wa Temeke, Abdallah Chaulembo, alisema: “Ni vyema mameya wote tukaungana ili kusaidiana na Rais katika kuleta maendeleo kwa wananchi wetu.”

mwisho

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles