28.2 C
Dar es Salaam
Sunday, December 1, 2024

Contact us: [email protected]

Magufuli azidi kuandamwa

Waziri John Magufuli
Waziri John Magufuli

Na Aziza Masoud, Dar es Salaam.

CHAMA cha Alliance for Democratic Change (ADC), kimemtaka Rais Jakaya Kikwete kumfukuza kazi Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli kwa kuisababishia hasara Serikali baada ya kushindwa kesi ya uvuvi haramu wa samaki katika Ukanda wa kiuchumi wa Bahari ya Hindi bila kibali.

Kauli hiyo imekuja siku chache baada ya Serikali kubwagwa katika kesi hiyo maarufu kama kesi ya ‘samaki wa Magufuli’ iliyofungulia mwaka 2012 wakati Dk. Magufuli akiwa Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam.

Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa ADC Taifa, Said Miraji alisema chama hicho kimepokea taarifa ya hukumu hiyo kwa mshtuko mkubwa kwa kuwa mazingira ya kesi yalikuwa hayaonyeshi kuwa watuhumiwa hao wanaweza kushinda na kuibwaga Serikali.

“Tunamtaka Rais Kikwete amfute kazi Waziri Magufuli kwa kulitia Taifa hasara na kupoteza kodi za wananchi, kwa sababu kama Magufuli alikuwa anajua idadi ya samaki hadi dagaa, hesabu ya samaki katika meli ile ilimshindwaje mpaka akashindwa ile kesi,” alisema Miraji.

Alisema chama kinatambua kazi anayoifanya Dk. Magufuli katika wizara zote lakini kwa hili suala kuna haja ya kumwajibisha ili iwe fundisho kwa wengine.

Alisema pamoja na kumfuta kazi Magufuli, Rais Kikwete pia aangalie uaminifu kwa umakini ofisi ya Mwanasheria Mkuu pamoja na wanasheria wa Serikali kutokana na kushindwa kwa kesi mara kwa mara.

“Ofisi ya Mwanasheria Mkuu badala ya kusimama na kuwaita watu tumbili, asafishe msitu katika ofisi yake, awachunguze kwa kina na kuwaangalia wanasheria wake ili wafanye kazi kwa uadilifu, kuna uwezekano baadhi vijana wake watakuwa wanachukua rushwa kukwamisha baadhi ya kesi kwa kuandaa maelezo yasiyojitosheleza,” alisema Miraji.

Mwishoni mwa wiki iliyopita, Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imewaachia huru Wachina wa ‘samaki wa Magufuli’ na kuamuru Jamhuri iwarejeshee vitu vyao ikiwemo meli ya Tawaliq 1.

Wachina hao nahodha wa meli, Hsu Chin Tai na Wakala wa Meli ya Tawaliq 1, Zhao Hanquing, waliachiwa kupitia hati ya Nole ya kuwaondolea mashitaka.

Hii ni mara ya pili kwa Wachina hao kuachiwa kwani mara ya kwanza waliachiwa na Mahakama ya Rufaa Machi 28 mwaka huu, walikamatwa tena na kushtakiwa upya kwa mashtaka hayo hayo yaliyofutwa.

Washtakiwa hao walikuwa wakikabiliwa na mashtaka ya uvuvi haramu katika Ukanda wa Uchumi wa Tanzania.

Hakimu Harufani alisema mahakama imekubaliana na maombi ya Jamhuri hivyo inawaachia huru washtakiwa wote na kuamuru warejeshewe vitu vyao vilivyokuwa vinashikiliwa.

Wakati mawakili wa pande zote mbili wakikubaliana vitu vyote vya washtakiwa hao virudishwe, Meli ya Tawaliq 1 maarufu kama ‘Meli ya Magufuli’ ilizama baharini wakati kesi ikiwa bado inaendelea.

Kuzama kwa meli hiyo kunatokana na Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi kushindwa kuitunza tangu ilipokamatwa Machi 8, 2009 ikiwa na tani 293 za samaki aina ya Jodari iliyowavua katika Bahari ya Hindi ukanda wa kiuchumi wa Tanzania (EPZ) bila kibali.

Mbali na meli hiyo ambayo ina uwezo wa kuvua samaki kwenye kina kirefu baharini kuzama baada ya wajanja wachache kukata vyuma vyake na kuviuza, samaki waliokutwa ndani ya meli hiyo wanaokadiriwa kuwa na thamani ya zaidi ya shilingi bilioni mbili wote waligawiwa katika taasisi mbalimbali baada ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi wa wakati huo, John Magufuli kudai kuwa Serikali haiwezi kufanya biashara.

Inaelezwa kuwa sehemu kubwa ya meli hiyo ambayo imetengenezwa kwa malighafi aina ya Brass ambayo kilo moja kwa sasa inauzwa kwa Sh 5,200, vyuma vyake karibu vyote vimekwisha uzwa na wajanja wachache waliokuwa wakipenya baharini kwa ajili ya kuvikata.

Washtakiwa hao walikamatwa mwaka 2009 na boti ya askari wa doria wa nchi za Tanzania, Afrika Kusini, Botswana na ilibainika kuwa leseni waliyokuwa nayo ilikuwa imemaliza muda wake Desemba mosi, 2008.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles