29.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 26, 2024

Contact us: [email protected]

Magufuli atumbua Majipu 23

John+Magufuli+PHOTO*Atengua uteuzi wa katibu Mkuu Uchukuzi, bosi Bandari
*Vigogo TPA wasimamishwa kazi, wawekwa chini ya ulinzi

Na Fredy Azzah, Dar es Salaam

MPANGO wa Rais Dk. John Magufuli wa kutumbua majipu, safari hii umegeuka na kung’oa vigogo 23 wa Mamkala ya Bandari (TPA) pamoja na kuvunja Bodi ya Wakurugenzi ya mamlaka hiyo.

Bodi hiyo ilikuwa na vigogo kadhaa akiwamo Naibu Spika wa Bunge, Dk. Tulia Ackson na Mkurugenzi wa zamani wa Mamlaka ya Udhibiti ya Nishati na Maji (Ewura), Haruna Masebu.

Hatua ya kuvunjwa kwa bodi hiyo, imetokana na kushindwa kuisimamia vema Bandari, hali iliyosababisha makontena 2,716 kutolewa bandarani bila kulipia kodi na kuisababishia Serikali hasara ya mabilioni ya shilingi.

Akitangaza uamuzi huo jijini Dar es Salaam jana, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alisema Rais Magufuli, ametengua uteuzi wa Mwenyekiti wa bodi hiyo, Profesa Joseph Msambichaka kutokana na uzembe huo, huku Mkurugenzi wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Awadhi Massawe naye uteuzi wake ukifutwa.

Majaliwa alisema, Rais Magufuli pia ametengua uteuzi wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi, Dk. Shaban Mwinjaka kutokana na ubadhirifu wa Sh bilioni 16 ndani ya Shirika la Reli Tanzania (TRL).

Maofisa wa Bandari Kavu

Akifafanua juu ya waliosimamishwa kazi TPA kutokana na makontena kutolewa bandarini bila kulipiwa kodi, Waziri Mkuu Majaliwa alisema maofisa 12 wa mamkala hiyo wamesimamishwa kazi na kuamuru wawekwe chini ya ulinzi ili wasaidie kujua wamiliki wa makontena hayo na gharama yake.

Alisema kati ya maofisa waliosimamishwa, wapo wasimamizi wanane wa Bandari Kavu (ICD), waliohusika kutoa makontena hayo bandari kavu kwenda kwa wateja na wanne waliohusika kutoa makontena hayo bandarini kwenda ICD.

Alisema waliohusika kutoa makontena hayo bandarini ni Shaban Mngazija, aliyekuwa Meneja Mapato na kwa sasa amehamishiwa Makao Makuu Kitengo cha fedha.

Waziri Mkuu Majalia aliwataja maofisa mwingine ni Rajab Mdoe, aliyekuwa Mkurugenzi wa Fedha na Mkuu wa Bandari Kavu (ICD), ambaye amehamishiwa Makao Makuu kwa Naibu Mkurugenzi Co- Operate Service, Ibin Masoud, ambaye ni Kaimu Mkurugenzi wa Fedha, Apolonia Mosha, Meneja Bandari Msaidizi wa Fedha.

Alisema maofisa wa TPA waliokuwa wakifanya kazi bandari kavu na kuruhusu makontena hayo kutoka na kwenda kwa wateja bila kulipiwa kodi ni Happygod Naftari, Juma Zaar, Steven Naftari Mtui, Titi Ligalwike, Lydia Prosper Kimaro, Mkango Alli, John Elisante na James Kimwona ambaye kwa sasa amehamishiwa jijini Mwanza.

Alisema hatua hizo kwa upande wa TPA zimechukuliwa kutokana na madudu yaliyobainika baada ya ziara alizofanya kwenye taasisi hiyo Novemba 27mwaka huu ambapo alibaini upotevu wa kontena 329 na ile ya Desemba 4, mwaka huu iliyobaini upotevu wa kontena 2,387.

“Ziara yangu ilinipitisha hatua zote za upitishaji mizigo ambazo pia kwa mujibu wa taarifa ya uchunguzi wa ndani wa Julai 30, mwaka huu TPA niligundua kuwepo kwa mianya mingi ya ukwepaji wa kodi ikiwamo na makontena 2387 yaliyopitishwa kati ya Machi na Septemba mwaka jana kinyume cha taratibu.

“Vitendo hivi vinaonesha kuwa bandari yetu hupitisha makontena mengi bila ya kulipiwa kodi na hakuna hatua zozote zinazochukuliwa. Upotevu huo unakwenda sambamba na mfumo usiokidhi wa kupokea malipo ambao unatoa mwanya mkubwa wa kupoteza mapoto ya Serikali,” alisema Majaliwa.

Ripoti ya Bandari

Alisema katika ripoti ya Bandari iliadhibu watu wa ICD tu lakini yeye amesimamisha na wale viongozi wa sekta iliyoruhusu makontena kwenda bandari kavu kwa kuwa ufisadi huo ulifanywa kwa maofisa hao kushirikiana.

Alisema wakuu hao wa vitengo wamechukuliwa kwa kuwa wao ndiyo wahusika wakubwa wa kutoa makontena hayo bandarini na walikuwa na nafasi ya kujua kila kitu kilichokuwa kikiendela ICD, lakini walishindwa kubaini kilichotokea na hawakuchukua hatua yoyote baada ya upotevu huo.

“Wote hawa, wawe chini ya ulinzi wahojiwe na wasaidie kubaini makontena haya yametokaje, ni ya nani na yana thamani gani na lazima kodi zile zilipwe ili TPA na TRA waweze kupata kodi yao,” alisema Majaliwa.
Waziri Mkuu Majaliwa, alisema kutokana na ziara hiyo, aliamuru TPA ikamilishe mfumo mpya wa uulipaji mpaka kufika Desemba 11, mwaka huu.

Akifafanua juu ya kutenguliwa uteuzi wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi, Dk. Shaban Mwinjaka, alisema hatua hiyo imechukuliwa kutokana na ziara aliyofanya katika Shirika la Reli Tanzania (TRL) ambapo alibaini ubadhirifu wa Sh bilioni 16.

“Tarehe nne (Desemba), nilifanya ziara TRL, nikaenda kujifunza mwenendo mzima lakini nikiwa na taarifa za matumizi mabaya ya fedha Sh bilioni 16.5, kati yake Sh bilioni 13.5 zilitolewa na Serikali kwa ajili miradi ya TRL ili iweze kujiendesha.

“…. na Shilingi bilioni tatu TRL ilipata mkopo kutoka TIB ili kuendesha miradi yake, fedha zote hizi zilitumika visivyo na uchunguzi bado unaendelea.

“Kwa kuwa TPA na TRL yote ni mashirika yanayoshindwa kujiendesha vizuri, Rais Dk. Magufuli ametengua uteuzi wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi, wote hawa wataendelea kusaidia uchunguzi ili kupata taarifa ya kina,” alisema Majaliwa.

Bodi iliyovunjwa

Kwa mujibu wa taarifa zilizopo katika tovuti ya TPA, Bodi ya Wakurugenzi iliyovunjwa na Dk. Magufuli, iliteuliwa na aliyekuwa Waziri wa Uchukuzi, Samuel Sitta, ambapo wakati akiitangaza alieleza namna bodi hiyo ilivyosheheni wajumbe mahiri wenye fani ya sheria, manunuzi, masoko, uhandisi wa kielektroniki na ujenzi.

“Lengo la uteuzi huu ni kuleta tija na ufanisi wa utendaji kazi wa mamlaka ya usimamizi wa Bandari Tanzania,” alisema Sitta wakati akiitangaza.

Wajumbe wa bodi hiyo walioteuliwa na kuanza kazi Juni mwaka huu ni pamoja na Dk. Tulia Ackson, ambaye kwa sasa ni Naibu Spika wa Bunge ambaye kwa wakati huo alikuwa Mhandhiri Mwandamizi, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Kitengo cha Sheria.
Wengine ni Mhandisi Mussa Ally Nyamsingwa, Mhandisi wa Ujenzi, Norplan Consultants, Donata Mugassa ambaye ni mtaalam wa manunuzi na Mjumbe wa Bodi ya PSPTA.

Wengine ni Mkurugenzi wa zamani wa Ewura Haruna Masebu, Mhandisi Gema Modu, ambaye ni Mhandisi wa Elekroniki wa Bodi ya Wahandisi Tanzania, Dk. Francis Michael, Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuuu cha Dar es Salaam, Crescentius Magori ambaye ni Mkurugenzi wa Mipango NSSF na Flavian Kinunda, Mkurugenzi wa Masoko Mstaafu wa Mamlaka hiyo.

Dk. Michael na Tulia walikuwa wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba, ambalo Sitta alikuwa mwenyekiti wake.
Kabla ya uteuzi wa bodi hiyo, Sitta alivunja bodi ya awali iliyoteuliwa na mtangulizi wake katika wizara hiyo, Dk. Harrison Mwakyembe, ambaye alikuwa Waziri wa Uchukuzi kabla ya kuhamishwa kwenda Wizara ya Afrika Mashariki.

Bodi ya Mwakyembe

Dk. Mwakyembe aliteua bodi ya TPA Novemba 6, 2012 ambayo wajumbe wake walikuwa ni John Ulanga, Caroline Temu, Jaffer Machano, Dk. Hildebrand Shayo, Said Salum Sauko, Mhandisi Julius Mamiro na Asha Nasoro.

Bunge lafafanua

MTANZANIA ilimtafuta Msemaji wa Bunge, Owen Mwandumbya, alithibitisha kuwa Naibu Spika wa Bunge, Dk. Tulia Ackson, alikuwa mjumbe wa bodi ya mamlaka hiyo, ingawa tangu alipochaguliwa kushika wadhifa mpya hajawahi kushiriki kikao chochote cha bodi hiyo.

Alisema hatua ya Serikali kuivunja bodi hiyo itamfanya Naibu Spika Dk. Tulia kuweka nguvu zake katika shughuli za Bunge.

“Ni kweli alikuwa mjumbe wa bodi hiyo, lakini kwa muda sasa hajashughulika na shughuli za bodi hiyo kwa sababu ya majukumu ya unaibu spika.

“Kwa sasa yupo kwenye mkutano wa mabunge ya Ulaya na Karibibian na Afrika, haya ndiyo majukumu yake mapya,” alisema Mwandumbya.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles