33.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 19, 2024

Contact us: [email protected]

Magufuli atoa neno mali za waislamu

Na ANDREW MSECHU

RAIS Dk. John Magufuli, ameamua kutumia mamlaka yake ya kikatiba kuhakikisha kuwa mali zote za Waislamu zilizochukuliwa isivyo halali zinarejeshwa.

Akizungumza katika maadhimisho ya Miaka 50 ya Baraza Kuu la Waislamu nchini (Bakwata) jijini Dar es Salaam jana, Rais Magufuli alisema alichukua uamuzi huo baada ya kupata ombi kutoka kwa Mufti, Sheikh Abubakar Zuberi, ambaye alimweleza namna mali hizo zilivyochukuliwa na kumwomba asimamie zirejeshwe.

“Kwa jinsi Mufti alivyozungumza kupigania maslahi ya Waislamu, aliniambia kwamba awali nilipokuwa waziri (wa Ardhi) nilishindwa kuzisimamia, lakini sasa mimi ni Rais na ninapewa mamlaka ya kisheria kupitia Katiba katika masuala ya ardhi.

“Aliniambia kwa kuwa wewe sasa ni Rais tusaidie hizi mali ziweze kurudi. Tena aliniambia akiwa amenikazi jicho, na kwa mcha Mungu unapoambiwa na kiongozi wa juu wa kidini kama Mufti ni kwamba umeambiwa na Mungu kwa hiyo ni lazima utekeleze,” alisema

Alisema baada ya ombi hilo alimwita waziri wa ardhi na wakuu wa mikoa akiwamo, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda na kutoa maagizo kwa viongozi wote aliowateua katika mikoa na wilaya akiwataka waangalie namna ya kufuatilia mali za Waislamu na kusaidia kuzirejesha, suala ambalo kwa kiasi kikubwa linafanikiwa.

Alisema katika mali ambazo zilikuwa na ugumu wa urejeshaji wake kutokana na mazingira na mikataba migumu aliamua kutumia mamlaka yake kuzifutia umiliki wake kutoka kwa waliokuwa wamejimilikisha au kumilikishwa.

Rais Magufuli alisema awali aliwahi kupelekewa suala hilo alipokuwa waziri wa ardhi ambapo alibaini kwamba ni kweli mali hizo za Waislamu zipo zilizokuwa zimechukuliwa, ila alibaini Waislamu wenyewe ndio waliohusika katika kuzihujumu.

“Niliwahi kufuatili kwa undani ni kwa namna gani mali za Waislamu zilichukuliwa au kupokonywa. Baada ya kufuatilia nilibaini waliohusika kuzigawa ni Waislamu wenyewe kwa kuingia katika mikataba migumu ambayo walishindwa kuisimamia na kuitekeleza,” alisema.

Ombi                                    

Baada ya kueleza hayo, Rais Magufuli aliwaomba Waislamu kuwa mali zote ambazo zimeanza kurejeshwa mikononi mwa Bakwata hazirudi tena huko zinakotolewa.

“Ninaomba muhakikishe mali hizi ambazo zimeanza kurejea hazirudi tena kule zilikotolewa. Nimefanya haya kwa mapenzi makubwa kwa Waislamu, kikubwa zaidi mjue kuwa unapofanya jambo kubwa kwa maslahi ya wengi kuna watu ambao wanaguswa na hawawezi kufurahi, hivyo ninaomba muniombee,” alisema.

Alisema kwa wakati huu ni vyema wajiepushe na migogoro kwa kuwa migogoro wakati wote huletwa na shetani na ndiyo inayowachelewesha watu.

Alisema wakati Waislamu wakiadhimisha miaka 50 ya kuanzishwa kwa Bakwata wamepitia changamoto nyingi, lakini suala la kujivunia ni suala la kuendelea kuwa wamoja kwa kudumisha amani na amali zao.

Alisema miongoni mwamambo muhimu anayoweza kufanya katika maadhimisho hayo ni kuwashukuru kwa kura nyingi walizompa zilizomwezesha kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, suala mbalo atakuwa anatenda dhambi iwapo hatalitekeleza.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles