25.2 C
Dar es Salaam
Sunday, December 1, 2024

Contact us: [email protected]

Magufuli atoa maagizo mazito kwa wakandarasi

Nora Damian -Dar es salaam

RAIS Dk. John Magufuli ameagiza kufukuzwa kazi kwa watendaji watakaobainika kuwapa kazi wakandarasi wa nje kwa miradi ambayo thamani yake haizidi Sh bilioni 10.

Serikali ilielekeza miradi yote isiyozidi Sh bilioni 10 wapewe wakandarasi wa ndani ili kuongeza fursa za ajira na uwekezaji ndani ya nchi.

Akizungumza jana wakati akifungua mkutano wa mwaka wa mashauriano uliohusisha Bodi ya Usajili wa Makandarasi (CRB), Bodi ya Usajili wa Wahandisi (ERB) na Bodi ya Usajili wa Wabunifu Majengo na Wakadiriaji Majenzi (AQRB), Rais Magufuli alisema hata akiletewa mapendekezo na waziri atatengua nafasi ya mtendaji husika.

“Hizi fedha za Road Fund (Mfuko wa Barabara) zinakusanywa na Serikali na ni za walipakodi, sasa kwenye miradi hata midogo midogo mnawapa watu wengine, mradi wa kuchimba choo unampa mtu wa nje…

“Tanroads, Tarura, Waziri wa Ujenzi, Waziri wa Maji ama Waziri wa Mifugo huyo haitaji kuwa mhandisi wa mkoa mfukuze, kama ni ofisa mifugo fukuza ni lazima tufike mahali tuamue.

“Katibu Mkuu Kiongozi au Katibu Mkuu ukiletewa mapendekezo na waziri lete kwangu mimi nitatengua,” alisema Rais Magufuli.

Pia alisema kutokana na gharama kubwa za ukandarasi Serikali imelazimika kutumia nguvu kazi (Force Account) kutekeleza baadhi ya miradi na matokeo yamekuwa mazuri.

Alitoa mfano wa ujenzi wa vituo vya afya 352 vilivyojengwa kwa Sh bilioni 184 ambapo kama wangetumia wakandarasi vingegharimu zaidi ya Sh trilioni moja.

Mifano mingine aliyotoa kwa kutumia nguvu kazi ni ya ujenzi wa darasa moja kwa Sh milioni 20 wakati mkandarasi ni kati ya Sh milioni 50 – 60, bweni moja na vitanda 80 Sh milioni 75 ambapo angejenga mkandarasi bila kuweka vitanda lingegharimu Sh milioni 170.

“Tujiulize sisi watu wa ujenzi wapi tunakosea, kwanini wakijenga watu wengine wa kawaida ni nafuu kuliko kuwahusisha wataalamu waliosomeshwa na Serikali?

“Mfano ungekuwa wewe ndiyo kiongozi wa Serikali ungechagua njia ipi, fedha umezipata kwa shida, changamoto ni nyingi…ungechagua kutumia Force Account ili fedha zingine zitumike kwa shughuli nyingine,” alisema.

Kuhusu madeni ya wakandarasi alisema mwaka 2016/17 zililipwa Sh bilioni 557, 2017/18 zililipwa Sh bilioni 833.645 na kuahidi kuwa 2019/20 wataongeza fedha zaidi kuwawezesha makandarasi kufanya kazi zao kwa ufanisi.

Rais Magufuli alitoa mfano wa mmoja wa wakandarasi aliyefukuzwa kisha kupewa kazi ya kujenga Uwanja wa Ndege Songwe aliyoifanya chini ya kiwango na kuilazimu Serikali kutumia tena Sh bilioni 18 kuukarabati.

“Mbeya kuna bwawa limechimbwa kwa zaidi ya miaka 12 lakini halijaisha hadi leo na kuna kisima kimoja kimetumia zaidi ya Sh milioni 400 na hadi leo hakijaisha.

“Mtu akifukuzwa afukuzwe moja kwa moja akavue hata samaki, hata kama ana GPA ya 4 ‘practical’ imemshinda alikuwa anadesa tu. Ni heri tuwe na wataalamu wachache badala ya kuwa na kampuni nyingi ambazo hazi–perform,” alisema Rais Magufuli.

WENYEVITI WA BODI

Mwenyekiti wa CRB, Consolata Ngimbwa, alisema hadi sasa makandarasi waliosajiliwa ni 10,794, wahandisi 25,812, wabunifu majengo 1,898, kampuni za ushauri wa wabunifu majengo 418 na kampuni za ushauri wa kihandisi 348.

Hata hivyo alisema kutokana na kukiuka sheria mbambali wamewafutia usajili makandarasi 4,558, wahandisi 450, wabunifu majengo 117, kampuni za ushauri wa wabunifu majengo 47 na kampuni za ushauri wa kihandisi 87.

Consolata aliiomba Serikali kujenga mazingira wezeshi ya kisheria yatakayohakikisha ushiriki wa wataalamu wa ndani katika miradi mikubwa unakuwa ni wa lazima.

Mwenyekiti wa ERB, Profesa Ninatubu Lema, alisema Tanzania ni ya pili kwa kuwa na wahandisi wengi ikitanguliwa na Afrika Kusini yenye wahandisi 110,000 na kwamba wakijipanga vizuri wanaweza kuyatumia masoko ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) yenye watu milioni 470.

“Tusijidharau sisi ni jeshi kubwa hivyo tufanye kazi kwa bidii, uaminifu, uadilifu na uzalendo wa hali ya juu katika Taifa letu,” alisema Profesa Lema.

Alisema pia wanatarajia kujenga kituo cha ushauri jijini Dodoma na tayari wamepata eneo la mita za mraba 60,000 ambalo litatumiwa na wahandisi wazalendo kujifunza na kujenga viwanda.

Mwenyekiti wa AQRB, Dk. Ludigija Bulamile, aliiomba Serikali kutoa kipaumbele cha ajira kwa wataalamu hao kwa sababu bado hawaajiriki kirahisi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles