27.7 C
Dar es Salaam
Monday, February 26, 2024

Contact us: [email protected]

Magufuli atema wakuu wa mikoa 12

Adeo pg 1 14 FEB 2016.indd*Paul Makonda kuongoza Dar, Wamo makamanda wa JWTZ

* Kilango, Zambi, Mwanry, Dk. Kebwe, Shingela wakumbukwa

Na Kulwa Mzee, Dar es Salaam

RAIS Dk. John Magufuli, amefanya uteuzi wa  wakuu wa mikoa wapya huku akiwatema 12 wa zamani.

Katika uteuzi huo Rais Magufuli ameteuwa majenerali wa wanne wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) na kuwapangia kazi katika mikoa ya mipakani.

Taarifa ya Ikulu iliyotolewa jijini Dar es Salaam jana na Kaimu Katibu Mkuu Kiongozi, Mhandisi Mussa Iyombe ilieeleza kwamba wakuu hao wa mikoa wataapishwa kesho Ikulu.

Katika uteuzi huo wakuu wa mikoa 26 walioteuliwa kati yao 13 ni wapya, saba  wamebakizwa katika vituo vyao vya kazi, watano wamehamishwa vituo vya kazi, huku wengine wakipandishwa akiwemo Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Paul Makonda.

Februari 13, mwaka huu Rais Dk. John Magufuli, alilitaja hadharani jina la Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Paul Makonda kuwa mmoja wa watu waliojihakikishia nafasi katika Serikali yake kutokana na utendaji kazi wake.

Rais Magufuli aliyasema hayo alipokuwa akizungumza na wazee wa Dar es Salaam ambapo pamoja na kusifia utendaji kazi wa Makonda, alisema umma usishangae iwapo atampandisha cheo.

Makonda alitajwa kwa kiwango kikubwa kuhamasisha uchangiaji wa elimu na kusimamia shughuli za maendeleo.

“Najua watu wanauliza sana ni lini nitateua wakuu wa mikoa na wilaya. Wala hawatajua, lakini ninaendelea kuwachambua, angalau mheshimiwa Makonda umeshajihakikishia angalau kupata. Lakini na wewe sasa usianze kulala,” alisema Rais Magufuli katika mkutano huo na wazee.

Kauli hiyo ya Magufuli imeonekana kuwaibua baadhi ya wakuu wa wilaya ambao kwa zaidi ya wiki moja sasa wamekuwa wakisambaza wenyewe au mawakala wao picha za utendaji kazi wao kupitia mitandao mbalimbali ya kijamii.

Walioteuliwa

Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Paul Makonda, ameteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Meja Jenerali Mstaafu Ezekiel Kyunga (Geita), Meja Jenerali Mstaafu Salum Kijuu (Kagera).

Wengine ni Meja Jenerali Mstaafu Raphael Muhuga aliyekuwa Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) ameteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Brigedia Jeneral Mstaafu Emmanuel Maganga (Kigoma) na Godfrey Zambi (Lindi).

Wengine ni Dk. Kebwe Steven Kebwe (Morogoro), Kamishna Mstaafu wa Polisi, Zelothe Stephen (Rukwa), Anna Kilango Malecela ( Shinyanga) na Mhandisi Methew Mtigumwe (Singida).

Wengine walioteuliwa ni aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro, Antony Mataka (Simiyu), aliyekuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Aggrey Mwanri (Tabora), huku aliyekuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana wa CCM na badaye kuwa mshauri wa Rais Jakaya Kikwete wa mambo ya siasa, Martine Shigela akiteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Tanga.

Katika uteuzi huo, Rais Magufuli amewakumbuka na kuwafuta machozi baadhi ya wabunge walioanguka majimboni mwaka jana, ambao walikumbana na upepo wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).

Wabunge hao na majimbo yao katika mabano ni Agrey Mwanry (Siha), Anne Kilango (Same Mashariki), Godfrey Zambi (Mbozi Mashariki) na Dk. Kebwe Steven Kebwe (Serengeti).

Waliohamishwa ni aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Jordan Rugimbana kapelekwa Mkoa wa Dodoma, Said Meck Sadick (Kilimanjaro), Magesa Mulongo (Mara), Amos Makalla ( Mbeya) na John Mongella (Mwanza).

 

Waliobaki vituoni

 Rais pia amewateua na kuwabakisha katika vituo vyao vya kazi Amina Masenza (Iringa), Daudi Ntibenda (Arusha),

Dk. Joel Bendera (Manyara), Halima Dendegu (Mtwara), Dk. Rehema Nchimbi (Njombe), Evarist Ndikilo (Pwani), Said Mwambungu (Ruvuma) na Luteni Mstaafu Chiku Galawa ambaye amepelekwa Mkoa mpya wa Songwe ulioanzishwa baada ya kugawanywa Mkoa wa Mbeya.

 

Kiapo

Taarifa hiyo ya Ikulu ilieleza kwamba wakuu wote wa mikoa walioteuliwa wataapishwa kesho saa tatu na nusu asubuhi Ikulu, jijini Dar es salaam.

Waliotemwa

Wakuu wa mikoa waliotemwa na mikoa yao katika mabano ni Dk. Parseko Kone (Singida), Fatma Mwasa (Geita), Ludovick Mwananzila (Tabora), Ally Rufunga (Shinyanga), Eraston Mbwilo (Simiyu), Abas Kandoro (Mbeya), Dk. Rajabu Rutengwe (Morogoro), Mwantumu Mahiza (Tanga).

Wengine ni Asery Msangi (Mara) Kanali Mstaafu Issa Machibya (Kigoma), Dk. Ibrahim Msengi (Katavi) na Magalula Said Magalula (Rukwa).

Chekeche kwa Ma-DC

Pamoja na Rais Magufuli kakamilisha kazi ya uteuzi wa wakuu wa mikoa hivi sasa presha imebaki kwa wakuu wa wilaya, huku taarifa za ndani zikieleza kwamba wengi wao hawapewi nafasi ya kurejea katika nafasi zao.

Tangu Rais Magufuli alipotangaza Baraza la Mawaziri Desemba mwaka jana, baadhi ya wakuu wa mikoa  pamoja na wilaya wameripotiwa kuishi kwa hofu ya kutemwa katika nafasi zao.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
583,000SubscribersSubscribe

Latest Articles