Anna Potinus, Dar es Salaam
Rais John Magufuli amemzuia Waziri wa Madini, Dotto Biteko, kuzungumza katika Mkutano wa Kisekta wa Wizara ya Madini na kisha kuwapa nafasi wadau na wachimbaji wa madini wadogo kuzungumzia changamoto zao.
Hali hiyo imejitokeza leo Jumanne Januari 22, katika mkutano huo baada ya wasemaji mbalimbali kuzungumza akiwamo Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, na wa mwisho alikuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini Dunstan Kitandula.
Baada ya mwenyekiti huyo kuzungumza, Rais Magufuli alisema anatoa nafasi kwa wadau wa madini badala ya serikali kutoa nasaha zake na kisha baada ya wadau hao serikali ije na majibu badala ya mapendekezo.
“Nawapa nafasi ya kuzungumza na nawataka mzungumze kwa uwazi bila kuogopa chochote.
“Kama tunahitaji suluhisho tusije na maneno ya jumla jumla, tunataka tujue kwanini Tanzania hainufaiki na madini wakati tunayo mengi, kwanini yanatoroshwa na juzi polisi walisindikiza.
“Kwanini TRA (Mamalaka ya Mapato Tanzania) hawakusanyi kodi, kwanini Makamishna waliopo mikoani wanalipwa mishahara lakini madini yanatoroshwa kwenye maeneo yao, je tume ya madini inafanya nini katika kudhibiti jambo hili.
“Kwanini Tanzanite pamoja na kujenga ukuta bado inatoroshwa, kwanini hatuna maeneo ya soko la madini kama dhahabu wakati BOT (Benki Kuu ya Tanzania) wapo, mawaziri wapo, makatibu wakuu wapo, hujawaeleza soko liko wapi inabidi watoroshe, hata kama tutakaa siku tatu ni lazima tutoke na majibu.
“Kwanini wachimbaji wadogo wanashawishika kuuza nje badala ya huku ndani, mimi kwa mawazo yangu nilifikiri haya ndiyo ya kujadili bila hivyo tutawaeleza yetu tutapiga picha tutaondoka na hatutapata suluhisho,” amesema Rais Magufuli.
Baada ya kusema hayo, Rais Magufuli aliwaambia wadau hao kama wanamkubalia suala hilo anaomba kuchukua uenyekiti aanze kuchagua wazungumzaji huku akiwahoji wanakubali waseme ndiyo na wasiokubali waseme siyo, waliokubali waliitikia kwa nguvu na kumfanya Rais Magufuli kusema waliosema ndiyo wameshinda jambo lililoshangiliwa na watu wengi.