Anna Potinus – Dar es salaam
Rais John Magufuli amesisitiza wananchi kupiga vita suala la rushwa kwa lengo la kukuza maendeleo ya nchi huku akiwataka wafanyakazi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kutumia chombo hicho vizuri na kufanya utafiti wa haki usio wa kuwaonea watu bali kuwatendea haki.
Rais Mgufuli ametoa kauli hiyo leo Alhamisi Machi 28, Ikulu jijini Dar es salaam baada ya kumuapisha Balozi wa Tanzania nchini Cuba, Valentino Mlowola na kupokea taarifa ya Takukuru ambapo amesema kuwa rushwa haina chama na kwamba hata ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ipo.
“Rushwa ni ugonjwa kuliko hata saratani na ndiyo maana ninawaomba Watanzania kwa ujumla tupambane na rushwa na ninapongeza juhudi ambazo zinaendelea kufanywa na pongezi za kimataifa tunazozipata kutokana na kupambana na rushwa.
“Nilipigiwa simu na watu fulani wakaniambia wanaombwa rushwa na vongozi wa CCM nikamtafuta mtu wa Takukuru nikamwambia awashike tena wakiwa wamevaa nguo za kijani kwa hiyo rushwa haina chama hata ndani ya CCM kuna rushwa pia hivyo Takukuru ninawapongeza kwa kuwakamata kwa haraka,” amesema.
Aidha, amemtaka Balozi Mlowola kwenda kwenye kituo chake cha kufanyia kazi haraka iwezekanavyo na kuachana na tabia wanayoifanya baadhi ya mabalozi ya kuaga kila ofisi baada ya kuapishwa.
“Balozi usichelewe kuondoka ukawa unaaga aga, nilishasema nikishakuteua wala usije kuniaga nenda kwenye kituo chako na mke wako kama ni mfanyakazi wa serikali Waziri ampangie kazi huko huko ndiyo atakuwa msaidizi wako anakula mshahara na wewe unakula mshara hiyo ndio faida tena itasaidia kutunza siri za serikali,” amesema