22.5 C
Dar es Salaam
Saturday, May 11, 2024

Contact us: [email protected]

Magufuli aifumua Muhimbili

04-IMG_7712*Amng’oa mkurugenzi mkuu, avunja bodi

*Asononeshwa wagonjwa kulala chini

 

NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM

RAIS John Magufuli, amemng’oa Kaimu Mkurugenzi wa Hopitali ya Taifa Muhimbili, Dk. Hussen Kindato pamoja na kuvunja bodi ya wakurugenzi wa hospitali hiyo.

Hatua hiyo ameichukua jana baada ya kufanya ziara ya kushtukiza katika hospitali hiyo, ambapo alipofika alikagua maeneo yote, kutembelea wodi na kushuhudia idadi kubwa ya wagonjwa wakiwa wamelala chini kwa kukosa vitanda.

Taarifa iliyotolewa jana na Katibu Mkuu Kiongozi Ikulu, Balozi Ombeni Sefue, ilisema kuwa Rais Dk. Magufuli amesikitishwa na hatua ya wagonjwa kukosa huduma hospitalini hapo, ikiwamo ya mashine za MRI na CT Scan kwa ajili ya uchunguzi wa maradhi ambazo zimeharibika kwa zaidi ya miezi mwili.

Balozi Sefue, alisema hali hiyo imemkasirisha Rais Magufuli kwa kuwa huduma hiyo inatolewa katika hospitali binafsi, huku wagonjwa wakielezwa kwenda huko.

“Lakini wakati huu mashine kama hizo zinafanya kazi katika  hospitali binafsi na wagonjwa wanaelekezwa kwenda huko, jambo hilo limemkasirisha sana Rais Magufuli na amechukua maamuzi kadhaa ikiwamo kuvunja Bodi ya Hospitali ya Taifa Muhimbili.

“Pia hatua nyingine ni kumwondoa Mkurugenzi wa hospitali hiyo, Dk. Hussein Kindato ambaye amepelekwa Wizara ya Afya kwa ajili ya kupangiwa kazi nyingine. Hivyo amemteua Profesa Lawrence Mseru ambaye zamani alikuwa akiongoza MOI kuwa kaimu mkurugenzi hadi hapo atakapoamua vinginevyo.

“Vilevile ameuagiza uongozi mpya wa Hospitali ya Taifa Muhimbili katika kipindi cha wiki moja, kwa vyovyote si zaidi ya wiki mbili, kuhakikisha mashine zote za uchunguzi wa magonjwa zinafanya kazi kama inavyopaswa na wakati wote kuhakikisha zinahudumiwa ili ziweze kutoa huduma wakati wote,” alisema Balozi Sefue.

Alisema pamoja na hali hiyo Wizara ya Fedha jana imetoa kiasi cha Sh bilioni tatu kwa ajili ya kulipa madeni na gharama za kutengeneza mashine hizo za Hospitali ya Taifa Muhimbili na hospitali nyinyine nchini.

“Kuanzia sasa kila hospitali itenge bajeti ya fedha kwa ajili ya kuhudumia mashine hizo kila wakati na madeni ya ukarabati yasilimbikizwe.

“Mashine hizo zifanye kazi wakati wote kama ilivyo kwa hospitali binafsi. Nitumie nafasi hii kuwakumbusha watumishi wa umma na viongozi wote sehemu za umma, kwamba anachosema Rais Magufuli kwamba awamu yake ya sasa ni kazi tu si utani, ni lazima watu wafanye kazi kwani humjui lini mtatembelewa,” alisema Balozi Sefue.

Alisema katika taarifa yake iliyotumwa kwa vyombo vya habari na Ikulu kuwa ni jambo la muhimu zaidi watu kufanya kazi si kwa kuogopa kwa ajili ya rais atakuja kukagua, ila wafanye kazi kwani wao ni watumishi wa umma na wapo kwa ajili ya kuwahudumia wananchi.

“Na tufanye kazi wakati wote,” alisema Balozi Sefue.

 

NAMNA ALIVYOFIKA MUHIMBILI

Rais Magufuli alifika Muhimbili saa 7:30 mchana ambapo alisema ziara hiyo ililenga kujifunza adha na matatizo wanayokumbana nayo wagonjwa wanaofika kutibiwa hapo.

Akiwa hospitalini hapo, Rais Magufuli alipata fursa ya kumsalimia na kumpa pole aliyekuwa Mbunge wa Kilindi mkoani Tanga, Beatrice Shelukindo (CCM), ambaye amelazwa baada ya kuvunjika mguu.

“Nimefanya ziara hii ya kushtukiza kwa lengo la kujifunza na ili kujionea hali halisi na matatizo wanayokumbana nayo wagonjwa wanaofika hapa kupatiwa matibabu… kwahiyo nimejifunza mengi na nimeshuhudia jinsi wodi zilivyojaa hadi wengine wamelala chini,” alisema.

Mbali na kumtembelea Shelukindo, Rais Magufuli pia alipata fursa ya kuwatembelea wagonjwa wengine waliolazwa hospitalini hapo katika wodi ya wanawake ya Mwaisela pamoja na wodi namba 17 ya Sewahaji.

Rais Magufuli amewasisitiza wahudumu wa afya katika hospitali hiyo kuendelea kufanya kazi ya kuwahudumia wagonjwa kwa bidii na moyo licha ya kwamba wanakabiliwa na changamoto mbalimbali.

 

AMJULIA HALI DK. BISIMBA

Kabla ya kufika Hospitali ya Muhimbili, Rais Magufuli alimtembelea Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk. Hellen Kijo-Bisimba aliyelazwa katika Hospitali ya Agha Khan kwa matibabu baada ya kupata ajali iliyosababisha kuvunjika kwa mfupa wa paja.

Bisimba alipata ajali hiyo juzi katika barabara ya Ali Hassan Mwinyi wakati alipokuwa kwenye gari yake yenye namba za usajili T 159 ATY ambayo iligongwa ubavuni na kupoteza mwelekeo jambo ambalo lilisababisha kupinduka mara nne.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa Tiba wa Hospitali ya Agha Khan, Dk. Mustafa Bapumia, alisema kuwa Bisimba amelazwa kwenye chumba cha wagonjwa walio katika uangalizi maalumu (ICU) huku akisubiri kufanyiwa upasuaji kwenye mfupa wa paja.

Alisema kwa sasa hali yake inaendelea vizuri, na kwamba jopo la madaktari linaendelea na matibabu ili aweze kufanyiwa upasuaji huo jambo ambalo linaweza kusaidia kurudia katika hali ya kawaida.

Dk. Bapumia alisema awali madaktari walitaka kumfanyia upasuaji jana, lakini walishindwa baada ya sukari na moyo kupanda ghafla kutokana na ajali aliyopata.

Hii ni mara ya pili kwa Rais Magufuli kufanya ziara ya ghafla ambapo mwishoni mwa wiki jana alifanya ziara kama hiyo katika Wizara ya Fedha na kukuta maofisa wengi wakiwa hawapo ofisini.

Rais Magufuli alifika katika ofisi hizo muda mfupi baada ya kumwapisha Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju, Ikulu.

Katika ziara hiyo, Rais Magufuli alitoka Ikulu kwa mguu na kuingia wizarani hapo kwa lengo la kujionea utendaji kazi wa watumishi katika wizara hiyo ambapo alipokewa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Dk. Servacius Likwelile na kisha kutia saini kitabu cha wageni.

Baada ya kufanya hivyo, katika hali isiyotegemewa, Rais Magufuli alitembelea ofisi moja baada ya nyingine na kujionea maajabu ambapo katika baadhi ya ofisi alikuta watendaji, wakiwamo maofisa waandamizi hawapo.

Rais Magufuli kila alipohoji waliko maofisa hao, hakupata majibu ya moja kwa moja huku akijibiwa kwamba walikwenda kunywa chai.

Alipomaliza kutembelea ofisi hizo, alipata fursa ya kuzungumza na maofisa waandamizi na maofisa wakuu wa wizara.

Jambo kubwa alilozungumza na viongozi na watumishi hao waandamizi ni kuhakikisha wanaziba mianya ya ukwepaji kodi ili kuiwezesha Serikali kukusanya mapato mengi.

Sambamba na hilo, aliiagiza Wizara ya Fedha kuhakikisha ukusanyaji wa kodi unaongezwa kwa kasi ili kuiwezesha Serikali kupata mapato ambayo pamoja na mambo mengine, yatawezesha kutimiza azma yake ya kutoa elimu bure hadi kidato cha nne.

Rais Magufuli pia aliwataka wataalamu wa Wizara ya Fedha na wale wa TRA kusimamia ipasavyo uingiaji na utoaji mizigo katika Bandari ya Dar es Salaam ili kudhibiti ukwepaji wa kodi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles