Anna Potinus
Rais Dk. John Magufuli amesema amepata fundisho lililomfanya aachane na tabia ya kuwapongeza wateule wake wanaofanya kazi nzuri akihofia wasije wakapatwa na mambo mabaya ambayo yanaweza yakawapelekea kupoteza maisha akitolea mfano wa tukio lililowahi kumtokea baada ya yeye kupongezwa na Rais Mstaafu, Benjamini Mkapa alipofanya vizuri.
Ametoa kauli hiyo leo Jumanne Novemba 12, alipokuwa akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa kitabu cha historia ya maisha ya Rais Mstaafu, Benjamin Mkapa ambapo amesema kuwa kitendo cha yeye kupongezwa kilimletea matatizo na kufanya achukiwe na baadhi ya mawaziri hadi kufikia hatua ya kunyweshwa sumu.
“Nakumbuka Mzee Mkapa pale tulipofanya kazi vizuri alifurahi na baadae akatamka mimi kuwa askari wake wa mwamvuli namba moja kwa kufanya kazi nzuri ya barabara, siwezi kusahahu suala hilo maishani mwangu kwasababu licha ya dhamira yake njema liliniletea mimi matatizo nilianza kuaona dalili za baadhi ya mawaziri tena wengine wa ngazi za juu kabisa kuanza kunichukia na baada ya hapo nikanyweshwa sumu Dodoma ambayo alimanusura iondoe uhai wangu lakini kwa neema za Mwenyezi Mungu nikakiepuka kifo.
“Baada ya tukio la kunusurika kifo nilimwendea Mzee Mkapa kumuelezea dhamira yangu ya kutaka kujiuzulu nakumbuka siku hiyo aliniangalia kwa jicho la baba na mwana akinihurumia na pia kunipa ujasiri na baada ya dakika chache aliniambia nanukuu “John kafanye kazi ukimtanguliza Mungu” na baada ya hapo nikapewa ulinzi nikaendelea kuchapa kazi,” amesema Rais Magufuli.
Amesema tukio hilo lilimfanya amuone Mzee mkapa ni mtu anayewapa watu moyo hata kama wamekata tamaa lakini pia amejifunza kutokuwasifu wateule wake hata kama wanafanya mazuri mengi ili yasije yakawapata yaliyompata yeye.