27.1 C
Dar es Salaam
Wednesday, June 12, 2024

Contact us: [email protected]

Magufuli afichua siri ya majipu

John-Pombe-MagufuliNA ELIYA MBONEA, ARUSHA

RAIS Dk. John Magufuli  amesema analazimika kuwatumbua majipu baadhi ya watendaji na viongozi wa Serikali kwa kuwa ni wagumu na hawataki kubadilika.

Amesema   anapoamua kumsimamisha mtu au kumfukuza kazi si kwamba yeye ni katili bali analazimika kufanya hivyo kwa sababu wenye majipu ni makatili kwa Watanzania walio wengi.

Dk. Magufuli alitoa kauli hiyo mjini hapa jana   kwenye ibada iliyofanyika katika Parokia ya Tokeo la Bwana Burka, Jimbo Kuu Katoliki la Arusha. Ibada hiyo  iliongozwa na Paroko, Padri James Mailady.

Akizungumza na waumini waliohudhuria ibada hiyo, Rais Magufuli aliwasisitiza waumini kuendelea kumuombea.

“Kuongoza ni kazi kubwa na kuongoza Taifa   maskini kama Tanzania inahitaji mkono wa Mungu zaidi.

“Ndugu zangu ninapochukua hatua hizi nataka kuiweka Tanzania kwenye mstari ulionyooka… nawaomba muendelee kuniombea, ninafahamu jukumu hili ni kubwa.

“Nimejitoa sadaka, najua sadaka yangu itasimamiwa na Mwenyezi Mungu,” alisema Rais Magufuli huku akikatishwa na vigelegele na shangwe kutoka kwa waumini.

Katika maombi hayo, aliwataka Watanzania wamtangulize Mungu huku wakitambua siku moja kila mtu atakufa na hivyo ni vema wajitahidi kutenda matendo mema hasa kwa watu wanyonge.

“Watanzania wengi ambao ni wanyonge, wanapata shida na kunyanyaswa na watu wakubwa waliopewa madaraka.

“Kwa hiyo, siku zote tusimame tukimuomba Mungu kwa sababu  hivi vyeo ni vya muda, mwenye cheo kikubwa ni Mungu peke yake.

“Natoa wito kwa tuliopewa dhamana ya kuongoza hasa wenye madaraka makubwa, tuyatumie madaraka haya kwa ajili ya Watanzania waliotuchagua ambao kwa dhati na kwa muda mrefu, walikuwa wanateseka,” alisema.

Rais  aliwahakikishia waumini hao  kwamba hajabadilika katika misimamo yake, hivyo yale aliyoahidi atahakikisha anayatimiza ikiwamo kuondoa kero za wananchi.

“Kila siku nimekuwa nikizungumza uchaguzi umeisha, lengo letu sasa ni kuipeleka Tanzania mbele, shida za Watanzania ni nyingi kuliko vyama vya siasa, ndugu zangu tupeleke maslahi ya Watanzania mbele kuliko vyama vyetu.

“Nataka niahidi tena kwenu leo  kwamba nitajitahidi sana nisiwaangushe ndugu zangu ndiyo maana nachukua baadhi ya hatua,” alisema.

“Naahidi kwenu kwamba nimekubali kuwa mwanaparokia wenu na bahasha yangu ya zaka, nitajitahidi kuilipa  nisije nikatumbuliwa na paroko,” alisema.

Katika ibada hiyo  pia alitoa mchango wake wa Sh milioni moja kwa ajili ya kwaya ya kanisa hilo iweze kununua sare nyingine za kuimbia.

Naye Padri Germin Longio akihubiri kanisani hapo, alisema Rais Magufuli hakuliacha kanisa yatima na badala yake aliliachia msaidizi ambaye ni Roho Mtakatifu.

Alisema   kutokana na kuwa na kiongozi imara, kila muumini anatakiwa kufanya kazi kwa kuwa Yesu Kristo alisema asiyefanya kazi na asile.

Rais Magufuli  bado yupo  Arusha baada ya juzi kuwatunuku kamisheni maofisa wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).

Leo  anatarajia kuzindua majengo mawili ya mifuko ya jamii ya PPF na NSSF.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
588,000SubscribersSubscribe

Latest Articles