27.1 C
Dar es Salaam
Thursday, January 2, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

Magonjwa ya moyo tishio zaidi ya Ukimwi duniani 

VERONICA ROMWALD – DAR ES SALAAM



MAGONJWA ya moyo yanazidi kuwa tishio duniani, Shirika la Afya Duniani (WHO) linaeleza vifo vitokanavyo na magonjwa hayo duniani ni vingi ikilinganishwa na vile vinavyotokana na ugonjwa wa Ukimwi.

WHO linaeleza magonjwa ya moyo husababisha takribani vifo vya watu milioni 18 kila mwaka idadi hiyo ni sawa na asilimia 31.

Shirika hilo linaeleza idadi hiyo ni mara tatu zaidi ya idadi ya vifo vitokanavyo na ugonjwa wa Ukimwi ambao unakadiriwa kusababisha vifo milioni tano kila mwaka.

Kulingana na Shirika hilo asilimia 75 ya vifo vinavyotokana na magonjwa ya moyo hutokea Barani Afrika na kwamba idadi kubwa ya vifo hutokea huko Latin Amerika na sehemu za Bara la Asia.

 

Hali ilivyo nchini

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), Profesa Mohammed Janabi anasema viashiria vinaonesha kuna ongezeko la idadi ya wagonjwa wa moyo.

“Takwimu za Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) zinaonesha matatizo yanayoongoza kwa idadi kubwa ya wagonjwa wanaopokewa hapa hospitalini namba moja ni ajali ikifuatiwa na magonjwa ya moyo.

“Takwimu zetu hapa JKCI zinaonesha idadi ya wagonjwa inaonekana kuongezeka mwaka hadi mwaka, katika mwaka 2015 tulipoanza rasmi tuliona wagonjwa wa nje (Outpatient) 23,000, mwaka 2016 tuliona wagonjwa wa nje 53,000, mwaka 2017 tuliona wagonjwa zaidi ya 60,000 na mwaka 2018 ambao bado haujaisha tumeona wagonjwa 76,365.

“Ukijumlisha hii miaka mitatu tumeshahudumia wagonjwa wa nje zaidi ya 200,000, tumelaza (inpatient) wagojwa zaidi ya 11,000, tumefanya upasuaji wa kufungua kifua kwa kusimamisha moyo (kufungua kifua)  wagonjwa 800 na tumeshawafanyia upasuaji kwa tundu dogo wagonjwa 2,056, kiujumla tumhudumia wagonjwa  zaidi ya 250,000,” anasema.

Anaongeza “Hii maana yake ni nini?… tumeeleza huko nyuma tatizo ni nini? Moja labda uelewa wa watu umeongezeka na kuchukua hatua kuja hospitalini kwa uchunguzi, huenda ni kwa sababu wametambua sasa kuna taasisi kubwa (JKCI) ambayo inatibu magonjwa hayo.

Sababu za ongezeko

“Miaka ya hivi karibuni, imeelezwa kwa sababu ya mabadiliko chanya ya kiuchumi, umri wa wananchi kuishi nao umeongezeka (life expectancy), kadri umri unavyoongezeka na haya matatizo sugu ya moyo kama vile shinikizo la damu, moyo kuwa mkubwa nayo yanaongezeka.

“Lakini pia tumeeleza siku za nyuma pia kwamba hivi sasa mfumo wetu wa maisha si kama ule wa enzi za mababu na mabibi zetu, ulaji wetu si mzuri vyakula, tunakula vyenye mafuta mengi, wanga mwingi, uzito unazidi kuongezeka, hatua tabia ya kupima afya mara kwa mara na hatufanyi mazoezi.

“Tukijumlisha yote haya tumeongeza tatizo la moyo kuwa kubwa zaidi, ndiyo maana tunawashauri wananchi kuwa makini na ulaji, kufanya mazoezi, kupima afya mara kwa mara, kuepuka uvutaji wa sigara na unywaji pombe,” anasema.

Anaongeza “Kwa sababu swali kubwa tunajiuliza, kwanini watu wanaumwa sana sasa hivi wakati tukilinganisha na miaka 50 iliyopita, leo hii tuna hospitali, barabara, shule, elimu bora zaidi lakini nini kimetokea, kwanini magonjwa yamekuwa mengi.

“Tunaamini tiba imekuwa nzuri zaidi, teknolojia na madawa zaidi, magonjwa ya moyo, kisukari na saratani ni baadhi ya magonjwa yaliyo katika kundi la magonjwa yasiyo ya kuambukiza,” anabainisha.

 

Kuhusu saratani

Anasema saratani ni miongoni mwa magonjwa yasiyo ya kuambukiza na kwamba kuna changamoto ambazo wagonjwa hao huwa wanakabiliana nazo.“Wanakabiliwa na changamoto sita, mgonjwa anaweza kuwa na mojawapo ama zote kwa pamoja, huwa hawapati  vyema choo, sasa mtu akifunga choo maana yake ni kwamba ile sumu anayotakiwa kuitoa nje ya mwili inaendelea kubakia mwilini.

“Wagonjwa hawa pia hulalamika kupata tatizo la ‘acid’, vidonda vya tumbo, kwa kawaida wale wadudu wa saratani hukua katika mazingira hayo ya acid,” anasema.

Profesa Janabi anasema kutokana na hali hiyo, wagonjwa wengi hulalamika kukosa usingizi.

“Kibaiolojia mtu anapolala usingizi kuna homoni (kichocheo) ambacho mwili wake hukitoa, kichocheo hicho ni ‘anti cancer’, ikiwa mtu hapati usingizi maana yake kiwango cha kichocheo hicho huwa chini na hivyo saratani itaendelea ‘kumla’ zaidi,” anasema.

Anasema wagonjwa wa saratani hupata msongo wa mawazo kutokana na changamoto mbalimbali wanazopitia kila siku katika maisha yao.

“Kwa mfano unakuta mtu ameachwa na mumewe, mkewe… ametengwa, uchumi wake umeharibika, mwili wake hurusha homoni nyingi sana kuliko inavyopaswa kuwa,” anasema.

Anasema kitendo cha mtu kutokufanya mazoezi huchangia kupata magonjwa yasiyo ya kuambukiza ikiwamo saratani, moyo, kisukari na mengineyo.

“Mtu asipofanya mazoezi mwili wake huongezeka uzito kuliko kawaida, hali hiyo huweza kusababisha apate msongo wa mawazo, kutokunywa maji ya kutosha husababisha apate ‘acidit’, wagonjwa wa saratani huwa hawapati choo vizuri.

“Ni muhimu watu kuzingatia ulaji unaofaa, waepuke ulaji wa  vyakula vya wanga kwa wingi, vyakula vyenye mafuta mengi, chumvi nyingi, uvutaji sigara,unywaji wa pombe, kupima afya na kufanya mazoezi mara kwa mara ili kuepuka magonjwa haya,” anatoa rai.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles