AVELINE KITOMARY-DAR ES SALAAM
MKUU wa Kitengo cha Macho Hospitali ya CCBRT, Dar es Salaam, Dk. Crispin Ntomoka, amesema matatizo ya afya ya macho yamekuwa yakichangia ajali za barabarani kutokana na madereva wengi kutopima macho.
Akizungumza na MTANZANIA katika mahojiano maalumu, Dk. Ntomoka ambaye pia ni daktari bingwa wa magonjwa ya macho, alisema kwa siku kati ya wagonjwa 10 wanaofika katika kliniki yake wakiendesha gari, watatu wana tatizo la afya ya macho.
“Mtu mwingine anakuja akiwa na uoni hafifu, lakini anaendesha gari na ana leseni, wengine wanakuja wakiendesha gari, ukiwapima unagundua wana uono ambao kimsingi hauruhusiwi kuendesha chombo cha moto.
“Zamani tulikuwa tunasema matatizo ya macho hayaui, Serikali wakaweka nguvu kwenye magonjwa yanayoua sana kama Ukimwi, afya ya mama na mtoto kwenye macho ikasahaulika, sasa watu wengi huku wanaendelea kupata madhara,” alisema.
Dk. Ntomoka alisema hata ajali zinapotokea, mamlaka husika huwa haziendi kupima uono wa dereva, kitu ambacho si sahihi kwani hata uono hafifu unaweza kusababisha ajali.
“Ulishawahi kuona ajali ikitokea polisi wakawahi kumpima dereva macho? Mara nyingi wanakimbilia kupima ulevi, lakini hawapimi afya ya macho, hawajui kama hata afya ya macho inachangia kusababisha ajali barabarani kwa sababu kuna watu hawaelewi, wanaendesha gari hawaoni vizuri na utakuta mtu kama huyo alishawahi kupima sehemu akaambiwa avae miwani, baadaye akaacha kuvaa.
“Kati ya wagonjwa ninaowaona, watatu kati ya 10 wana shida inayotibiwa na miwani, lakini wanatembea barabarani na wanakwambia wanaona, lakini kitaalamu uono wao ni hafifu, ni sheria kupima macho kabla ya kupata leseni ila wapo wengine wanafoji vipimo kwa wahudumu wa afya wasio waaminifu.
“Wengine wanafanya kwa sababu hawajui umuhimu wa kupima afya ya macho, waamke wafanye vitu kwa usahihi, dereva usikubali kuendesha chombo cha moto bila kuhakikisha unapima afya ya macho ili kuzuia ajali barabarani.
“Nawaambia hii ni hatari kwa watumiaji wa barabara, vyombo husika vifuatilie kwa undani kuhakikisha afya ya macho ni namba moja katika vipimo, wawe na uhakika kuwa wanaoendesha magari wamefanyiwa uchunguzi na madaktari wa macho, kuna watu ambao macho yao yana shida ya kutofautisha rangi pia,” alisema Dk. Ntomoka.
Alisema sababu ya matatizo ya macho ni pamoja na umri mkubwa, matatizo ya mtoto wa jicho, magonjwa ya kurithi na ugonjwa unaotibiwa kwa miwani.
“Watu wazima karibu asilimia 75 ulemavu wa macho unasababishwa na matatizo yanayozuilika na asilimia 40 inasababishwa na mtoto wa jicho, sababu nyingine ni umri mkubwa kama miaka 60, pia kuna magonjwa yanayoathiri jicho kama kisukari, wengine ni kuumia na matatizo ya yanayotibiwa na miwani, hili tatizo linatokana na maumbile ya jicho,” alisema.
MATATIZO YA MACHO KWA WATOTO
Dk. Ntomoka alisema kwa mwaka huu watoto 200 wamefanyiwa upasuaji kutokana na magonjwa mbalimbali ya macho.
“Kuna sababu ambazo zinasababisha watoto wazaliwe na matatizo ya macho, ambazo ni pamoja na maumbile, mfano presha ya macho kwa mtoto iko kama anavyozaliwa na kilema ndivyo ilivyo, kuna ugonjwa wa mtoto wa jicho, kuna ya magonjwa ya kurithi kama yale ya tumboni kwa mama. Kama mama ana ugonjwa wa rubella, kaswemde, HIV na mengine.
“Wengine wanakuja wakiwa na shida ya mtoto wa jicho, kwa mwaka huu mpaka sasa wamefikia watoto 200 na kati yao asilimia 40 walikuwa na tatizo la mtoto wa jicho, mengine ni makengeza, aleji hii inatokea pale mazingira yanapomkataa mtoto.
“Wapo wanaotibiwa kwa dawa na wengine kwa upasuaji. Mtoto anatakiwa atibiwe mapema kwani akiwa mdogo mfumo wa jicho unakuwa haujakomaa, hivyo ni vizuri wakawahi kupata matibabu,” alieleza Dk. Ntomoka.
KOMPYUTA/SIMU HATARI
Kwa mujibu wa Dk. Ntomoka, matumizi ya vifaa vyenye mwanga mkali vinaumiza macho, ni hatari pia kwa afya ya macho.
Alisema vinasababisha uteute unaolainisha macho kukauka na macho yakiwa makavu yanaweza kuwasha, kutoa machozi, kuumia na wakati mwingine kuwa mekundu.
“Hii tunaita Computer Vision Syndromes, ni mkusanyiko wa usumbufu ambao mtu anapata kwa matumizi ya vifaa vyenye mwanga mkali.
“Ni changamoto sana, sasa hivi maofisini watu wengi wanakuja wanalalamika, ni muhimu watu wakajua kuwa matumizi ya muda mrefu ya kompyuta, simu na vifaa vingine vyenye mwanga mkali ni hatari kwa macho,” alifafanua Dk. Ntomoka.
Alieleza katika kliniki yake anawaona wagonjwa watano hadi 10 kwa siku, ambao wamepata madhara ya macho kutokana na vitu vyenye mwanga mkali.
“Madhara yanaweza yasionekane kwa sasa ila baada ya miaka kadhaa ukaanza kuumwa macho, katika kliniki yangu napata watu wengi wenye tatizo hilo, kila siku nikikaa klinini kati ya watu 40, watano hadi 10 matatizo yao yanatokana na vitu vyenye mwanga,” alifafanua.
Dk. Ntomoka aliwataka watu kufuata ushauri wa matumizi sahihi ya vifaa vyenye mwanga kama kupunguza mwanga na kupumzisha macho kwa dakika 20 kila baada ya saa moja.
“Watu wapate ufahamu juu ya matumizi sahihi ya kompyuta ili wasiweze kupata matatizo ya macho, wafuate ushauri wa kutumia smart phone (simu janja), kompyuta, televisheni na vitu vingine kama hivyo, kama watu wanahitaji ushauri waende kwa madaktari wa macho ili waweze kushauriwa.
“Pia ni muhimu kupumzisha macho kwa kila baada ya dakika 20 mpaka 30 au kuvaa miwani inayochuja kiasi cha mwanga,” alishauri Dk. Ntomoka.