Mtifuano Uchaguzi Uingereza

0
929

LONDON, UINGEREZA

GUMZO la Uchaguzi Mkuu wa Uingereza limeendelea kutawala ndani na nje ya nchi hiyo hususani katika vyombo mbalimbali vya habari vya kitaifa na kimataifa huku baadhi ya wachambuzi wa kisiasa, wakiona matokeo yake ni vigumu kutabirika kwa sasa.

Takwimu za utafiti wa hivi karibuni zinaonyesha chama cha Consevative cha Waziri Mkuu wa Uingereza, Boris Johnson kikiongoza na chama cha Labour kikiwa nyuma yao na chama cha Liberal Democrats.

Chama cha Nigel Farage cha Brexit, kiko chini katika kura na hivi sasa hakina uwakilishi katika Bunge la Uingereza.

Wakati baadhi ya wachambuzi wa kisiasa, wakiona matokeo ya uchaguzi huu hautabiriki, chama cha Farage nacho kimetajwa kuwa na uwezo wa kugawanya kura ya Brexit na kuwaacha chama cha Conservative bila ya wingi wa kura.

Rais wa Marekani, Donald Trump naye ameingia katika mjadala wa uchaguzi huo kutokana na kile ambacho baadhi wanaona kama jaribio la kutaka kumsaidia Waziri Mkuu, Johnson na zaidi akiwa nyuma ya agenda ya Uingereza kujitoa Ulaya ili Marekani iweze kufanya biashara nzuri na nchi hiyo.

Tuhuma za jaribio la kuingilia kati uchaguzi wa nchi nyingine zinaelekezwa dhidi ya Rais Trump baada ya kufanya mazungumzo ya simu na radio moja ya Uingereza Alhamisi.

Wakati wa mazungumzo hayo akiwa hewani na kiongozi wa Chama cha Brexit Nigel Farage, Trump alimpongeza Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson kuwa ni mtu barabara ambaye “ndiye mtu sahihi kwa nyakati hizi.”

Trump alimtaka Farage kushirikiana na Johnson, kiongozi wa Chama cha Conservative, katika kipindi hiki cha kuelekea kwenye uchaguzi mkuu utakaofanyika Disemba 12, ambapo suala nyeti ni Brexit.

“Iwapo yeye na wewe mtashirikiana, unajua kuwa ni nguvu isiyoweza kuzuilika katika uchaguzi,” Trump alitamka hilo kupitia Radia LBC.

Farage, ambaye alifanya kampeni kwa ajili ya kuwepo kura ya maoni mwaka 2016 kutaka msimamo wa wananchi iwapo Uingereza ijitoe Umoja wa Ulaya, ni mgombea katika uchaguzi ulioitishwa mapema.

Mahojiano ya Rais wa Marekani Alhmaisi na Farage, yalikwenda mbali zaidi na hata kumkosoa kiongozi wa chama cha Labour, akisema Jeremy Corbyn atakuwa “siyo mtu barabara kwa nchi yako” iwapo atachaguliwa kuwa waziri mkuu.

Corbyn naye mara moja alituma ujumbe wa Tweet akimshutumu Trump kwa “ kujaribu kuingilia kati uchaguzi wa Uingereza kumsaidia rafiki yake Boris Johnson kushinda uchaguzi.”

Mwandishi wa kisiasa wa gazeti la The Guardian, Andrew Sparrow, pia alisema Trump alitumia mahojiano hayo na Farage “kuingilia kati uchaguzi wa Uingereza.”

Boris Johnson aliahidi kuitoa Uingereza katika Umoja wa Ulaya “kwa njia yoyote ile” hadi Oktoba 31, akisema “afadhali afe chini ya shimo”.

Baada ya kuomba kuahirishwa kwa mchakato huo, Umoja wa Ulaya (EU) umekubali Jumatatu wiki hii kuchelewesha kwa muda wa miezi mitatu Uingereza kujitoa kutoka Umoja huo hadi Januari 31.

Pamoja na hayo mchakato wa Brexit bado haujulikani mwelekeo wake wakati wanasiasa wa Uingereza wakionekana wazi kutokuwa karibu kufikia muafaka juu ya vipi, lini na hata iwapo hatua ya kuachana na Umoja wa Ulaya itawezekana.

Mataifa 27 ya Umoja wa Ulaya Jumatatu wiki iliyopita yalifikia makubaliano kuchelewesha Brexit hadi Januari 31, pamoja na uwezekano wa Uingereza kujitoa mapema iwapo bunge la Uingereza litaidhinisha makubaliano ya kujitoa.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here