Na ELIYA MBONEA-ARUSHA
MAGEUZI yanayoendelea ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) yametajwa kuwa ni dawa chungu kwa viongozi, lakini ni nzuri.
Kauli hiyo ilitolewa mjini hapa jana na Katibu wa Itikadi na Uenezi Taifa, Humphrey Polepole alipokuwa akizungumza na viongozi wa ngazi mbalimbali wa chama hicho kutoka wilaya ya Arusha.
Akizungumzia mageuzi hayo, Polepole aliyetembelea pia Wilaya ya Longido alisema, CCM kwa sasa inataka kuwa na viongozi waadilifu kisiasa wasio na mwenendo wa kutiliwa shaka katika kuwatumikia watu.
“Tunataka viongozi ambao hata asipokuwa na mshahara au umechelewa fedha za chama ziendelee kuwa salama, tunataka viongozi wanaochukizwa na ubadhirifu wa mali za chama na Serikali,” alisema Polepole na kuongeza:
“Mageuzi ndani ya CCM ni dawa na kwa viongozi ni dawa chungu sana, lakini ni dawa. Kwa wanachama ni dawa tamu zaidi, kwa sababu wanaotuvuruga wakati mwingine ni viongozi hawa hawa,” alisema.
Katika mkutano huo uliohudhuriwa na viongozi wa CCM wilaya na Mkoa wa Arusha Polepole alitumia fursa hiyo pia kuonya wanachama wenye mchezo wa kupanga safu za watu wanaotaka kugombee uongozi wakati wa uchaguzi.
Alisema kwa muda mrefu sasa kumekuwapo na watu wanaoweka au kupanga viongozi na mabalozi ndani ya chama kwa ajili tu ya maslahi yao binafsi.
“Hatutakubali kuwa na kiongozi mbinafsi au yule anayetaka kupanga wenzake au wanaopanga safu na makundi yao hakika hatutakuwa na msalia mtume. Tukikubaini tutakula kichwa chako (kuondolewa),” alisema
Kuhusu wilaya ya Arusha, Polepole alifafanua kwamba nongwa ndani ya chama hususan wakati wa uchaguzi zinaweza kuathiri uchaguzi na hivyo aliwaomba viongozi hao kuwa kitu kimoja.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Arusha, Lekule Laizer alitumia mkutano huo kuomba radhi kwa kile kilichotokea katika Uchaguzi Mkuu wa 2015 baada ya wilaya hiyo ya Arusha kuambulia diwani mmoja tu wa chama hicho.