23.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, September 28, 2021

VODACOM YAONGEZA MTAJI SOKO LA HISA

Na JOHANES RESPICHIUS-DAR ES SALAAM


MTAJI wa Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) unatarajiwa kuongezeka kwa Sh bilioni 500, mara baada ya Kampuni ya Simu ya Vodacom kujiorodhesha sokoni hapo.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam juzi, Meneja Masoko wa DSE, Patrick Mususa, alisema wanategemea baada ya mchakato wa mauzo ya awali ya hisa za Vodacom na kujiorodhesha rasmi DSE, ukubwa wa mtaji utaongezeka maradufu.

Alisema uuzwaji wa hisa hizo bado upo chini ya Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA), ambapo baada ya hapo ndipo itajiorodhesha rasmi DSE ili kuingizwa rasmi sokoni.

“Kwa uhalisia, DSE haina utaratibu wa kubaini ushiriki wa uuzwaji wa hisa za awali, labda CMSA mpaka pale kampuni inapojiorodhesha kwenye soko. Tunatarajia ukubwa wa mtaji wa soko kuongezeka kwa takribani Sh bilioni 500 baada ya hisa za Vodacom kuingia sokoni.

“Licha ya faida hiyo, soko litakuwa limefanikisha kuongeza idadi ya makampuni yaliyojiorodhesha kwa sababu itakuwa imeingiza kampuni mpya kutoka Sekta ya Mawasiliano,” alisema Mususa.  

Hata hivyo, Mususa alisema thamani ya mauzo ya hisa wiki hii imeongezeka hadi kufikia Sh bilioni 4 kutoka Sh milioni 462, baada ya idadi ya hisa zilizouzwa na kununuliwa kuongezeka kutoka hisa 390,000 hadi milioni 7.

Alisema kutokana na kupungua kwa bei ya hisa za ACACIA kwa asilimia 13.5, KCB asilimia 9.2 na Jubilee Holdings asilimia 6.4, kumepelekea ukubwa wa mtaji wa kampuni zilizoorodheshwa  sokoni hapo kushuka kwa Sh trilioni 1.2 kutoka Sh trilioni 20.5 hadi Sh trilioni 19.3.

“Mtaji wa kampuni za ndani nao umepungua kwa Sh bilioni 200 hadi kufikia Sh trilioni 7.3 kutoka Sh trilioni 7.3, ikichangiwa na kupungua kwa bei ya hisa za DSE asilimia 6.3 na TBL asilimia 5.8, huku TBL ikiongoza kwa mauzo ya hisa zake kwa asilimia 67.4, ikifuatiwa na CRDB kwa asilimia 30.5 na DSE asilimia 1.2.

“Kiashiria cha kampuni zilizoorodheshwa, yaani DSEI kimepungua kwa pointi 138 kutoka pointi 2,359 hadi 2,221, baada ya hisa za makampuni kupungua, huku pointi 99 za kampuni za ndani (TSI) zikipungua hadi kufikia pointi 3,475 kutoka 3,574,” alisema Mususa.

Alisema sekta ya viwanda ilipungua pointi 183 kutoka pointi 4,620 hadi 4,437 baada ya hisa za TBL kupungua bei, hivyo hivyo kwa sekta ya huduma za kibenki na kifedha ambayo yenyewe ilishuka kwa pointi 2 kutoka pointi 2,548 hadi 2,546, ilichangiwa na kushuka kwa bei ya hisa za DSE wakati sekta ya huduma za kibiashara ikibaki kwenye kiwango cha awali cha pointi 3,137.

Mususa alisema mauzo ya hati fungani yalipungua kutoka Sh bilioni 23.1 hadi Sh bilioni 4.5 kutokana na kuuzwa kwa hati fungani sita za Serikali zenye thamani ya Sh bilioni 6.3 kwa gharama ya Sh bilioni 4.5.

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
158,460FollowersFollow
519,000SubscribersSubscribe

Latest Articles