24.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 19, 2024

Contact us: [email protected]

Magari ya Serikali yaua 20 miezi mitatu

Na MWANDISHI WETU


AJALI ya gari la Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) iliyosababisha vifo vya watu saba usiku wa kuamkia jana, inafanya jumla ya magari ya Serikali yaliyokumbwa na dhahama hiyo kufikia manne katika kipindi kisichopungua miezi mitatu.

Katika ajali hizo ambazo zimetokea kwa nyakati tofauti, kumbukumbu zinaonesha watu 20 wamepoteza maisha.

Ajali zote hizo zimetokea ndani ya miezi mitatu na siku mbili tangu Kangi Lugola alipoteuliwa kuongoza Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.

Ikumbukwe kwamba miongoni mwa mambo ambayo Rais Dk. John Magufuli alimwagiza Lugola kufanyia kazi ni pamoja na kuhakikisha anadhibiti ajali za barabani nchini.

Lugola mwenyewe alipozungumza na MTANZANIA Jumapili jana kwa njia ya simu kuhusu taarifa za mara kwa mara za ajali hasa zile zinazohusu magari ya Serikali, alisema atatoa takwimu zote kuhusiana na suala hilo.

Alisema tayari ameshawaagiza maofisa wa wizara hiyo kukusanya taarifa hizo kwa umakini.

“Kwa sasa natafuta takwimu zote za ajali za barabarani zinazotokana na magari ya Serikali, nikishazipata nitaitisha mkutano na waandishi wa habari kati ya kesho (leo) au kesho kutwa (kesho) nitafanya mkutano huu siku yoyote kuanzia kesho (leo) na mtapata taarifa rasmi kuhusu ajali za magari ya Serikali,” alisema.

Wakati Lugola akitoa msimamo huo, taarifa zilizokusanywa na MTANZANIA Jumapili zinaonesha kuwa magari ya Serikali yaliyoripotiwa kwenye vyombo vya habari kupata ajali ndani ya uongozi wa Lugola ni manne.

Ajali hizo ni pamoja na ile iliyotokea Julai 29 mwaka huu ikihusisha gari la Wizara ya Viwanda na Uwekezaji ambayo iligharimu maisha ya watu wawili huko mkoani Geita.

Nyingine ni ile iliyotokea Agosti 4, mwaka huu mkoani Manyara ambako gari ya Serikali iliyokuwa imembeba Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla ilipata ajali na kusababisha kifo cha mtu mmoja.

Mwezi uliopita ajali nyingine ya gari la Serikali ilitokea mkoani Singida ambako wafanyakazi watano wa Wizara ya Kilimo walifariki dunia. 

AJALI YA JANA

Katika tukio la ajali iliyotokea usiku wa kuamkia jana, watu saba wameripotiwa kufariki dunia huku wengine watatu wakijeruhiwa.

Ajali hiyo ilihusisha magari mawili ya Serikali katika eneo la Mbande, Kongwa mkoani Dodoma.

Akizungumzia tukio hilo jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Gilles Muroto, alisema ajali hiyo ilihusisha gari yenye namba za usajili STL 6250 mali ya CAG iliyokuwa ikitokea wilayani Chato kuelekea Dar es Salaam.

Alisema gari hilo lilikuwa likiendeshwa na Dickson Kitanda ambaye ni mtumishi wa ofisi ya CAG.

“Gari hilo liligongana uso kwa uso na gari lenye namba za usajili SU 41173 linalomilikiwa na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii wa PSSSF, ambalo lilikuwa likitokea Dar es Salaam kwenda Dodoma na lilikuwa ikiendeshwa na Peter Wilson,” alisema Kamanda Muroto.

Alisema chanzo cha ajali hiyo ni lori lililokuwa limeegeshwa barabarani bila kiashiria cha alama za kuonesha limeharibika.

Muroto alisema katika mazingira hayo gari hilo la ofisi ya CAG lililigonga lori hilo na kupoteza uelekeo, hivyo kwenda kugongana uso kwa uso na gari la PSSSF. 

CAG ANENA

Akizungumzia ajali hiyo, Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad alisema gari hilo lilikuwa limebeba ndugu wa msaidizi wake aliyemtaja kwa jina la Benjamin Mashauri ambao walikuwa wakitoka msibani huko Chato.

“Katika ile ajali mfanyakazi wangu ni mmoja tu ambaye ni dereva, waliobaki walikuwa ni ndugu wa msaidizi wangu anaitwa Benjamin Mashauri na walikuwa wakitokea Chato kwenye msiba,” alisema Profesa Assad.

TAARIFA YA MGANGA MFAWIDHI

Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma, Dk. Ibenzi Ernest alithibitisha kupokea miili saba ya marehemu wa ajali hiyo na majeruhi watatu ambao wamelazwa hospitalini hapo.

Dk. Ernest aliwataja waliofariki kuwa ni Dickson Kitanda (33), Grace Masato (42), Jofrey Samson (28), Andrew Lucas (24), Nehemia Wilfred (45), George Zakayo (52) na mwingine aliyemtaja kwa jina moja tu la Magai (58).

Aliwataja majeruhu kuwa ni Victoria Moshi, Abubakari Ndwata na Eliad Mndeme.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles