26.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

Ocean Road waanza kutibu kisasa saratani ya koo

NA VERONICA ROMWALD – DAR ES SALAAM


WAGONJWA wa saratani ya koo wanaotibiwa katika Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI), sasa wameanza kupatiwa tiba ya kisasa kwa kutumia mionzi ya ndani.

Akizungumza na gazeti hili ofisini kwake jana, Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Saratani wa ORCI, Dk. Jerry Ndumbaro, alisema huduma hiyo kitaalamu inaitwa Oesophageal Brachytherapy na imeanza kutolewa hospitalini hapo tangu Oktoba 30, mwaka huu.

“ORCI ni kati ya taasisi chache zinazotoa huduma hii katika ukanda huu wa Afrika Mashariki na Kati.

“Aina hii ya tiba awali hapa ORCI tulikuwa tunaitoa kwa wagonjwa wa saratani ya kizazi pekee, lakini kuanzia Oktoba 30, mwaka huu tumeanza rasmi kutoa tiba hii pia kwa wagonjwa wa saratani ya koo,” alisema.

Pia alisema tiba hiyo ya mionzi ya ndani ni nzuri zaidi ya mionzi ya nje kwa kuwa inampa mgonjwa nafuu mapema.

Dk. Ndumbaro alisema inaweza kutumika peke yake au kwa kuongezea na tiba ya mionzi ya nje.

Alisema tiba ya mionzi ya ndani kwa kutumia kifaa maalumu cha oesophageal applicators inawawezesha wataalamu kutibu ugonjwa moja kwa moja katika eneo lililoathirika.

“Kifaa hicho huingizwa kupitia mdomoni na kupelekwa moja kwa moja kwenye sehemu yenye ugonjwa, tunaweza kupima kama kimefika eneo husika kwa kutumia mashine maalumu.

“Hivyo tunatibu ugonjwa kwa haraka zaidi na mgonjwa anapata nafuu haraka zaidi ikilinganishwa na tiba ya mionzi ya nje pekee, ikizingatiwa kwamba wagonjwa wa saratani ya koo hushindwa kumeza, akipatiwa tiba hii humsaidia kupata nafuu mapema,” alisema.

Dk. Ndumbaro alisema saratani ya koo inashika namba nne kwa wingi wa idadi ya wagonjwa wanaohudumiwa katika taasisi hiyo.

“Huathiri zaidi wanaume zaidi ya wanawake katika uwiano wa wanne kwa mmoja, dalili zake kuu ni kushindwa kumeza chakula na kupungua uzito,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles