Hadija Omary -Lindi
MAGARI saba,nyumba tatu, zahanati moja na ofisi ya kata, vimechomwa moto maeneo tofauti mkoani Lindi.
Kutokana na hali hiyo, jeshi la polisi linawashikilia watu kadhaa kwa kuhusika na tukio hilo
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jana, Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Godfrey Zambi alisema uhalifu huo umefanyika wakati wa uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 28, mwaka huu.
Alisema katika Wilaya ya Liwale, uhalibifu huo umefanywa kwa mbunge mteule wa jimbo, Zuberi Kuchauka ambapo nyumba zake mbili na magari matatu yamechomwa na moto.
Alisema mgombea udiwani Kata ya Liwale Mjini ambaye alishinda nyumba yake imechomwa moto na zahanati yake, imevunjwa vioo vyote na kuharibiwa baadhi ya vifaa vya maabara.
Alisema pamoja na mali nyingine ambazo wanaendelea kuzitathmini magari hayo saba yaliyochomwa moto, yalikuwamo ya Serikali yakiwamo yaliyopelekwa kwa ajili ya uchaguzi.
Alisema watu hao ambao baadhi yao wamekamatwa pia walikusudia kuchoma moto nyumba ya askari mmoja ambaye alikuwa akishiriki zoezo la kusimamia upigaji kura,lakini walishindwa, badala yake wakaishia kuvunja vioo vyote vya nyumba hiyo.
Alisema hali aliyoikuta baada ya kutembelea maeneo yaliyoathiriwa, inaacha maswali mengi kama vurugu zote hizo ni kwa sababu ya uchaguzi tu au kuna jamnbo jingine nyuma yake?
“Kwa sababu vurugu zile zilianza kufanyika mapema kabla ya matokeo kutolewa, zilianza kufanywa saa mbili usiku hadi saa nne,wakati huo matokeo yalikjuwa bado…”alisema.
Alisema katika mji wa Nachingwea kumefanyika mambo aloyoyaita yasiyo ya kiungwana wala kibinadamu.
Alisema gari la Serikali liilichomwa moto pamoja na aliyekuwa Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Ahmad Makoroganya na nyumba yake kuvunjwa vioo vyote. Makoroganya alikuwa mgombea udiwani kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), alishinda uchaguzi huo.
Alisema pia ofisi ya Serikali ya Kata ya Mpiruka pia ilichomwa moto.
Akizungumza watu waliokamatwa kutokana na vitendo hivyo wilayani Nachingwea, Zambi alisema kundi la watu lilikuwa limejificha nyumbani kwa aliyekuwa mgombea ubunge wa wa Chadema likiwa na lita zaidi ya 40 za petroli, vinyago vya kuziba uso(mask), fomu namba 3 za polisi, pamoja na vitambulisho vya kupigia kura zaidi ya 60.
Kuhusu Jimbo la Mtama, Zambi alisema ofisi maendeleo ya jamii ilichomwa moto imeanguka haifai tena kwa matumizi, huku akisema jaribio kama hilo lilifanyika Kijiji cha Nyangamara.
Kuhusu Kilwa Kusini,alisema kulikuwa na jaribio la kuchoma ofisin ya kata ambapo petroli ilikwishamwagwa eneo hilo, lakini hivyo wasamaria wema waliwahi na kuidhibiti.
Alisema hadi sasa haijajulikana dhamkira ya watu wanaofanya huhalifu huo ni kina hadi, huku wakijiapiza kuwa wataua.
Aliyataja maeneo ambayo kauli hizo zimekuwa zikisemwa, kuwa ni Nachingwea, Liwale, baadhi ya maeneo ya Mtama na Kivinje.