25.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 18, 2024

Contact us: [email protected]

MAFURIKO YAUA MMOJA CHEMBA

Na RAMADHAN HASSAN -DODOMA

MKAZI wa Kijiji cha Mwaikisabe Kata ya Kimaha wilayani Chemba, TEO Sekali (35) mkoani Dodoma amefariki dunia, huku watu wengine zaidi ya 2000 wakiwa hawana mahali pa kuishi baada ya nyumba zao kuzingirwa na maji kutokana na mvua kubwa inayoendelea kunyesha wilayani humo.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Gilles Muroto alithibitisha kifo hicho jana akisema athari za mvua hiyo zimejitokeza katika vijiji vya Olboloti, Kaloleni na Mrijo Chini Kata ya Mrijo na Mwaikisabe Kata ya Kimaha wilayani Chemba.

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk. Binilith Mahenge alifika katika vijiji hivyo na kumwagiza Mkuu wa Wilaya ya Chemba, Simon Odunga kuwahamisha wakazi wa vijiji vya Olboloti na Kaloleni ambao wameathirika zaidi na mvua hiyo kwa vile walikuwa wamejenga mabondeni.

Pia amemwagiza DC kuwatafutia viwanja maeneo mengine wananchi hao.

Dk. Mahenge alisema athari ya mvua hiyo ni kubwa kwa sababu  zaidi ya watu 2000 hawana mahala pa kuishi.

“Wale ambao hawana sehemu za kuishi ni jukumu letu kuhakikisha mnapata sehemu za kuishi na mimi nipo hapa nitasimamia hili kwa kushirikiana na kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa na wilaya,” alisema.

Wakizungumza na waandishi wa habari jana, waathirika wa mvua hiyo walisema athari hiyo  imetokana na mvua  iliyonyesha juzi jioni   hadi jana.

Fatina Bato, mkazi wa Kaloleni alisema mvua hiyo imesababisha umaskini mkubwa kutokana na nyumba yake kuzolewa na maji.

“Kikubwa tunaomba msaada hali zetu ni ngumu hatujui tutaishije kwa sababu  hatuna nyumba, hatuna chakula, hatuna kila kitu, tuomba tusaidiwe,” alisema.

Naye Gudluck John, mkazi wa Olboloti, aliiomba Serikali iwasaidie kutokana na kutokuwa na sehemu ya kuishi huku wengi wakiwa wana watoto wadogo.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Olboloti, Abdalah Suti alisema  mvua iliyonyesha katika maeneo yao ni kubwa na kwamba haijawahi kutokea tangu miaka ya 1960.

Naye Amiry Issa ambaye ni  Mkuu wa Zimamoto Kituo cha Dodoma, alisema   kikosi kinaendelea na shughuli za uokozi kuzunguka vijiji hivyo huku akiwataka wananchi kutosogelea maeneo hatarishi.

Mkuu wa Wilaya hiyo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya, Simon Odunga alisema eneo wanaloishi wananchi hao ni  hatarishi ikizingatiwa  wanazungukwa na milima.

Aliwataka waaliojenga mabondeni kuhama mara moja.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles