Na DAMIAN MASYENENE–SHINYANGA
HALMASHAURI ya Wilaya ya Shinyanga mkoani hapa, imetoa kadi 5,568 za matibabu bure kwa wazee, huku nyingine 7,859 zikiendelea kutengenezwa kwa ajili ya kundi hilo maalum ili kuliondolea usumbufu wanaopata wakienda kupata huduma za matibabu.
Hayo yamebainishwa na Katibu wa Baraza la Wazee Wilaya ya Shinyanga, Boniface Boaz, katika risala ya baraza hilo iliyosomwa kwenye maadhimisho ya siku ya Wazee Duniani yaliyoadhimishwa kiwilaya katika Kitongoji cha Kiloleni Kata ya Masengwa wilayani Shinyanga yakibebwa na kaulimbiu ya ‘familia na jamii tuwajibike kuwatunza wazee’.
Alisema wilaya hiyo ina wazee 13,176 wakiwemo wanaume 6,283 na wanawake 6,893, huku kukiwa kumeanzishwa mabaraza ya wazee katika kata zote 26 za halmashauri hiyo ambayo yameunganishwa kwenye mfumo wa wizara.
Boaz alisema changamoto zinazokabili wazee wa wilaya hiyo ni pamoja na ukosefu wa maji safi na barabara zinazopitika wakati wote na bei ya nishati ya umeme kuwa juu.
Alisema pia wanahitaji kuthaminiwa kwa kuwekewa ulinzi, kupatiwa mikopo katika halmashauri inayotokana na makusanyo ya ndani, kupewa pensheni kila mwezi kupata fedha za kujikimu na kupatiwa vitambulisho vya matibabu bure.
“Bado matendo ya mauaji kwa wazee wenye macho mekundu yapo, hivyo elimu ya kulindwa kwa wazee iendelee kutolewa,”alisema.
Kwa upande wake Katibu Tawala Wilaya ya Shinyanga, Boniphace Chambi, alisema mauaji ya wazee yanayotokea nchini hususan katika jamii ya Wasukuma, chanzo huanzia kwenye familia, hivyo akatoa wito kwa jamii kuwajibika kuwatunza wazee na kubadili mawazo potofu.
“Tunashukuru kwa sasa matukio haya yamepungua, hivyo tuwajibike kuwatunza wazee wetu na tubadilishe mawazo kabisa na tuache hiyo kasumba kwa sababu uzee siyo uchawi bali ni baraka,” alisema.
Takwimu za Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto za mwaka 2020 zinaeleza kuwa tangu kuanza kutekelezwa kwa mkakati wa kitaifa wa kutokomeza mauaji dhidi ya wazee uliozinduliwa mwaka 2014, mauaji yamepungua kutoka 557 mwaka hadi 74 mwaka 2019, ambapo hadi mwaka huu idadi ya waliouliwa ni wazee 10 kwa mwaka.
Naye Mratibu shirika linalojihusisha na kutetea haki za wazee mkoani Shinyanga (TAWLAE), Eliasenya Nnko, alisema moja ya changamoto iliyopo sasa ni wazee kutoshirikishwa katika vyombo vya utoaji maamuzi na kutokupata mikopo licha ya uwezo wao wa kipato na uzalishaji mali kupungua.
“Maadhimisho ya mwaka huu kwa wilaya yetu ya Shinyanga yamepata mwitikio mkubwa kutoka makundi yote kwenye jamii, kwa sasa hatuwazii sana kuwatenga wazee na familia kwa sababu kuwaweka kwenye vituo ni kuzidi kuwatenganisha na familia na kuwafanya wakose upendo, muhimu hapa ni jamii kuwajali na kuwatunza,” alisema.