27.5 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

Msajili ataka vyama kufuata sheria kuepuka migogoro

Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam

MSAJILI wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi, amewataka viongozi wa vyama vya siasa na wadau wote kuheshimu sheria na taratibu za Uchaguzi kama zilivyoainishwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), ili kuepuka migogoro isiyo ya lazima. 

Alisema hayo alipokuwa akizungumza jijini Dar es Salaam katika kikao na viongozi wa vyama vya siasa ambacho kililenga kutathimi mwelekeo wa kampeni za Uchaguzi Mkuu 2020 zinazoendelea.

“Hiki si kikao cha kuja kusutana ila ni kikao cha kuja kuongea na kuangalia mwelekeo unavyokwenda kwenye kampeni, pia nafasi ya Msajili kama mlezi, nikaona nisiwanyime hiyo nafasi ya kukutana nanyi na kuwapa maneno mawili ya kuwakumbusha wajibu wenu” alisema Jaji Mutungi.

Jaji Mutungi aliwaomba wagombea na wadau wa vyama vya siasa kuimarisha demokrasia ya nchi kwa kufanya siasa za kistaarabu ambapo amewataka wagombea washindane kwa ustaarabu huku wakifuata sheria na taratibu za nchi.

 Alisema mtu yoyote atakayeonekana kwenda kinyume na maelekezo na taratibu za uchaguzi atachukuliwa hatua kulingana na taratibu zilizowekwa.

“Tuachane na ile dhana ya kwamba mtu anasema wakiniacha wananiogopa, wakinishughulikia wananionea, sasa huu ujumbe ninaousema uende pande zote, na sisi taasisi ambazo zimepewa mamlaka ya kusimamia utekelezaji wa hii sheria, tuisimamie kwa haki kwa sababu tusipofanya hivyo tunaweza sababisha tafarani,” alisema Jaji Mutungi. 

Naye, Mwenyekiti wa Women Fund Tanzania, Profesa Ruth Meena aliwataka wagombea wote nchini wachukue wajibu wa kuzifahamu sheria na maadili ya uchaguzi ili waweze kuzijua haki zao, kutengeneza hoja za msingi na kuepuka kutumia lugha za matusi katika kampeni zao 

“Wagombea ni lazima wachukue wajibu wa kuzielewa sheria, waelewe maadili ya uchaguzi hasa yale yanayohusu haki za wanawake na vijana katika kushiriki kikamilifu,”alisema Profesa Meena.

 Aliongeza kuwa wagombea wanawajibu mkubwa wa kujenga mazingira yatakayowezesha kutumia nguvu za hoja na si matusi wawapo katika kampeni zao ili kuweza kujenga mazingira ya amani.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles