PATRICIA KIMELEMETA
MAELFU ya wananchi wa Dar es Salaam na wengine kutoka nje ya mkoa huo, wamefurika kupata matibabu ya bure kwenye meli ya Jeshi la China yenye hospitali ndani, huku wengine wakidai wamelazimika kulala nje karibu na Kituo Kikuu cha Polisi ili wawahi kupata matibabu.
Meli hiyo iliyowasili juzi, inatarajiwa kukaa kwenye Bandari ya Dar es Salaam kwa siku saba, na tano kati ya hizo, madaktari bingwa 381 wa China, watatoa tiba kwa wananchi watakaojitokeza.
Wakati utoaji huduma hizo ukianza jana, gazeti hili lilizungumza na baadhi ya wagonjwa waliojitokeza hapo, huku wengine wakisema wametoka kwenye nchi za Kenya na Uganda, kufuata matibabu hayo.
“Nimefika jana (juzi) saa tatu usiku kwa ajili ya kuwahi foleni, lakini hadi sasa sijapata namba, badala yake idadi ya watu inaongezeka kila wakati hali iliyosababisha kujitokeza kwa msongamano,” alisema Juma Mohamed (47) mkazi wa Temeke anayesumbuliwa na maradhi ya kisukari.
Alisema Serikali ilipaswa kutangaza utaratibu wa wagonjwa wote kujiandikisha kwenye hospitali zao na kupewa namba ili madaktari wanapofika iwe kazi rahisi ya kuratibu zoezi la kuwapeleka.
Mohamed alisema kutokana na hali hiyo, dalili zinaonyesha wazi kuwa kuna baadhi ya wagonjwa wataondoka bila ya kupata matibabu.
Naye Fatuma Mohamed kutoka mkoani Tanga, alisema anasumbuliwa na maradhi ya tumbo kwa muda mrefu, hali iliyomfanya kutoka mkoani kwake na kuja kuwaelezea madaktari hao.
“Nimetoka Tanga juzi nimefikia kwa ndugu zangu ili niweze kupata matibabu ya tumbo yanayonisumbua kwa muda mrefu,” alisema Fatuma.
Alisema ameenda kwenye hospitali mbalimbali mkoani humo, lakini hadi sasa bado anasumbuliwa na maradhi hayo, hali ambayo imemfanya akate tamaa ya kupona.
Naye Theresia Joseph aliyesema anatoka Uganda, alisema kuwa amefika kwenye eneo hilo kujiandikisha ili aweze kupatiwa matibabu ya nyonga yanayomsumbua kwa muda mrefu, huku mtoto wake akisumbuliwa na maradhi ya tumbo.
Alisema kuwa alipopata taarifa ya kuwapo kwa madaktari hao, amelazimika kufunga safari yeye na mumewe ili waweze kujiandikisha na kupata matibabu, jambo ambalo linaweza kuwasaidia kupona.
Mosses Norman aliyesema anatoka Kenya, alisema anasumbuliwa na maradhi ya miguu kwa muda mrefu.
Alisema alipopata taarifa amelazimika kuja nchini ili aweze kuonana na madaktari hao ambao anaamini wanaweza kumsaidia ili aweze kupona.
“Nasumbuliwa na maradhi ya miguu kwa muda mrefu, kuna wakati nashindwa kutembea, niliamini kuwa, nikionana na madaktari wa kichina wanaweza kunisaidia ili nipone,” alisema Mosses.
Hata hivyo, baadhi ya wananchi wamesema kuwa mazingira ya uandikishaji katika eneo hilo ni hatarishi kwa sababu ni barabarani ambako magari yaendayo katikati ya jiji yanapita.
“Utaratibu uliotumika sasa hivi ni mbovu na kwamba unaweza kuhatarisha maisha ya watu, kwa sababu wagonjwa wanaandikishwa barabarani kwenye eneo finyu ambalo kila wakati magari yanapita, jambo ambalo linaweza kusababisha hatari.
“Ni bora wangeandikishwa katika viwanja vya mnazi mmoja na kubebwa na mabasi ya jeshi hadi bandarini kwa ajili ya kupatiwa matibabu, kuliko kuandikishwa barabarani,” alisema Omary Khamis mkazi wa Dar es Salaam.
Ili wagonjwa waweze kwenda kwenye meli kupata matibabu, walilazimika kupitia Kituo Kikuu cha Polisi, ambako kulikuwa na eneo lililotengwa kujiandikisha kisha kupakiwa kwenye magari ya jeshi kwenda kwenye matibabu.
Mkuu wa Mkoa, Paul Makonda, aliwataka wagonjwa kufika kwenye eneo hilo kujiandikisha ili waweze kupatiwa huduma za matibabu katika meli hiyo.
“Ninawaomba wakazi wa Dar es Salaam wale wenye matatizo kujitokeza na kujiandikisha ili waweze kupata huduma za matibabu bure kutoka kwa madaktari bingwa,” alisema Makonda.
Alisema ndani ya meli hiyo kuna vifaa tiba vya kisasa, vyumba 8 vya upasuaji, kuwalaza wagonjwa mahututi (ICU), wodi za wagonjwa, vyumba vya madaktari, mitambo ya kisasa, mahabara na sehemu ya wagonjwa kupumzika.
Makonda alisema meli hiyo pia ina helikopa kwa ajili ya wagonjwa na mfumo maalumu wa mawasiliano kati ya meli na taifa la China pale inapotokea ugonjwa umeshindikana.
Alisema lengo ni kuhakikisha kuwa wagonjwa wanapatiwa huduma za matibabu kulingana na matatizo waliyonayo.
“Meli hii ina madaktari bingwa ambao watatoa huduma za afya kwa wagonjwa wote watakaobahatika kupata matibabu, mkakati wa Serikali ni kuhakikisha kuwa watakaojiandikisha wanapata huduma za matibabu,” alisema.