26.9 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

ODINGA AJICHIMBIA ZANZIBAR, KENYATTA AJIANDAA KUAPISHWA

Na Mwandishi wetu

WAKATI Mahakama ya Juu ya Kenya ikitoa hukumu iliyobariki ushindi wa Rais Uhuru Kenyatta, mpinzani wake Raila Odinga, ameonekana visiwani Zanzibar, huku ikiwa haijulikani kama yupo kwenye ziara ya kikazi ama amekuja mapumzikoni.

Raila alionekana jana kwenye mgahawa wa Lukman, uliopo Mji Mkongwe, akiwa na msaidizi wake mmoja na mlinzi mmoja.

Mmoja wa wananchi walioshuhudia Raila akiwa eneo hilo, alisema: “Sijajua kama amekuja kwenye mapumziko ama ziara ya kikazi, lakini nilichoona tu ni kuwa alikuwa yeye na msaidizi wake na mlinzi wakaingia kwenye mgahawa huo kwa ajili ya chakula cha mchana.”

Kwa mujibu wa gazeti la Daily Nation, wafuasi wa Raila ambaye ni kiongozi wa muungano wa Nasa, waliandamana ili kuonyesha kutoridhishwa kwao na uamuzi ya Mahakama ya Juu uliobariki ushindi wa Kenyatta.

Maandamano hayo yalibadilika na kuwa ya ghasia katika maeneo kadhaa ya Nyanza, nyumbani kwa Odinga na maeneo ya Kibira na Mathare jijini Nairobi.

Pia vijana wengine walifunga barabara zinazoelekea mjini Kisumu kwa kuchoma magurudumu ya gari na kuweka mawe barabarani.

Gazeti hilo pia lilinukuu taarifa ya Odinga  iliyotolewa na mshauri wake, Salim Lone, akisema Serikali ya Jubilee si halali na kwamba uamuzi wa Mahakama ya Juu ulifanywa kupitia shinikizo.

”Sisi watu wa Nasa tayari tulikuwa tumeamua kabla ya uamuzi wa mahakama kwamba hatuitambui Serikali ya Uhuru Kenyatta.

”Uamuzi huo haujabadilishwa na uamuzi wa Mahakama ya Juu ambao haukutushangaza. Ni uamuzi uliotolewa chini ya shinikizo kubwa, hatushutumu mahakama, tunaihurumia,” alisema Lone.

Ushindi wa  Kenyatta wa Oktoba 26 uliidhinishwa na mahakama hiyo kupitia uamuzi wa pamoja wa majaji sita wa Mahakama ya Juu.

Kulingana na gazeti hilo, Lone amedai kwamba mahakama ilikutana chini ya shinikizo kubwa, baada ya kushindwa kukutana kutokana na wasiwasi mkubwa wa kiusalama kufuatia kupigwa risasi na kujeruhiwa kwa dereva wa Naibu Jaji Mkuu kabla ya kusikilizwa kwa kesi ya uchaguzi wa Oktoba 26.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles