CARACAS, VENEZUELA
MAELFU ya waandamanaji nchini Venezuela, wameingia katika siku nyingine ya maandamano, baada ya Rais Nicolas Maduro, kumweka kizuizini, Edgar Zambrano, ambaye ni naibu spika wa Juan Guaido katika bunge linalodhibitiwa na upinzani nchini humo.
Kwa mujibu wa mahakama kuu, Zambrano, anashikiliwa kwa makosa ya uasi dhidi ya Serikali na kuihujumu nchi. Zambrano alikamatwa na idara ya ujasusi SEBIN Jumatano iliyopita kwa kuunga mkono uasi wa Aprili 30, mwaka huu kutaka kumwondoa madarakani Maduro, uliopangwa na kiongozi wa upinzani Guaido ambaye anaungwa mkono na Marekani.
Rais Maduro anamtuhumu pia mkuu wake wa zamani wa ujasusi, Jenerali Christopher Figuera, kufanya kazi na Shirika la Upelelezi la Marekani, CIA. Venezuela imeingia katika mgogoro wa kisiasa tangu Januari mwaka huu, baada ya kiongozi wa upinzani Guaido kujitangaza kuwa Rais halali wa nchi hiyo.