31.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Dk. Bashiru kwa vijana hana sura mbili

Na LEONARD MANG’OHA

NI mwaka mmoja sasa tangu Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Dk. Bashiru Ally, alipopitishwa na chama hicho kushika wadhifa huo ulikuwa ukishikiliwa na Abdulrahman Kinana.

Kwa kipindi chote hicho Dk. Bashiru amejitofautisha na wanasiasa wengi kwa kutokuwa na tabia ya ukigeugeu, badala yake amekuwa katika sura na mtazamo mmoja na mara zote amesimama imara katika kile anachokiamini bila kuyumba.

Yapo mambo mengi ambayo Dk. Bashiru amejipambanua wazi katika ukosoaji bila kujali umaarufu au ukubwa wa cheo cha mtu ndani na nje ya chama anachokiongoza.

Hivi karibuni katika sura ile ile ameonyesha wazi wazi kukerwa na utendaji kazi wa baadhi ya viongozi wenye umri mdogo, huku akidai kuwa wamepewa dhamana ya uongozi pasipo kuandaliwa vema.

Tukianza na tukio la hivi karibuni lililomhusisha Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, wakati wa shughuli za mazishi ya aliyekuwa Mwenyekiti wa Kampuni za IPP, Dk. Reginald Mengi, yaliyofanyika mkoani Kilimanjaro, bila kujali atamuathiri nani au Chama chake Dk. Bashiru, hakuificha sura yake aliuthibitishia umati wa watu waliofurika kuaga mwili wa Dk. Mengi kuwa yeye ni mtu wa kunyoosha mambo na si kupindisha.

Itakumbukwa kuwa baada ya kutokea kifo cha Dk. Mengi viongozi mbalimbali wa vyama na Serikali walimzungumzia mengi aliyoyatenda, miongoni mwao ni Makonda ambaye katika maelezo yake alitaja kabila la wachaga na kuibua mjadala mpana.

Katika kuweka mambo sawa Dk. Bashiru Ally alilazimika kutumia madhabahu kumuombea msamaha Makonda kwa kauli yake.

Wakati akimwombea msahama Dk Bashiru amesema hayo ni matunda ya kutoandaa vijana wao kuwa viongozi bora jambo ambalo matunda yake yameanza kuonekana.

Dk. Bashiru anasema “Naomba nitumie fursa hii kumuombea msamaha kijana wangu Makonda mimi namfahamu na hii ni mara yangu ya pili namsema hadharani,”

“Mara yangu ya kwanza nilimsema kule Simiyu akaja analia ofisini nikasema ubadilike na kwa kweli ameanza kubadilika, bado ni kijana mzuri, shupavu lakini tunahitaji kuwasaidia vijana wetu,”

“Kuhusu uongozi na umuhimu wa kuwaandaa vijana wetu kuwa viongozi bora, Baba Askofu (Dk Fredrick Shoo)kazi hiyo hatujaifanya, na kwa sababu hatujaifanya, tunaanza kuvuna matunda ya kutowaandaa vijana wetu kuwa viongozi bora, watiifu, wakweli, wanyenyekevu na wenye heshima,” amesema Dk. Bashiru 

Kumbukumbu zinaonyesha kuwa si mara ya kanza kutoa kauli za aina hiyo Aprili 27, mwaka jana katika mahojiano maalumu na kituo kimoja cha televisheni alitoa kauli inayofanana na hiyo akidai kuwa licha ya mchango mkubwa alioutoa kwa chama chao, Mbunge wa Mtama, Nape Nnauye, anahitaji kupikwa, kusikilizwa, kuaminiwa na kusimamiwa.

Mwingine aliyemtaja ni Mbunge wa Nzega Mjini Hussein Bashe, amwelezea kuwa ni miongoni mwa vijana waliopitia katika Umoja wa Vijana wa chama hicho (UVCCM) wakati mfumo wa kuandaa viongozi ukiwa umekufa.

Dk. Bashiru amekuwa na mtazamo tofauti kabisa kuhusu wabunge hao ambao baadhi ya wana-CCM wamekuwa wakiwataja kuwa ni wabunge wakorofi ndani ya CCM, kutokana na hoja mbalimbali ambazo wamekuwa wakiziibua katika vikao mbalimbali vya Bunge na kuwanyima usingizi mawaziri.

Katibu Mkuu huyo amekuwa akilitazama hilo kwa hali ya utofauti na kila mara ameonesha kusimamia msimamo wake huo, bila kupindisha maneno na madai anayoyatoa ni kukosekana kwa mfumo rasmi wa chama wa kuwaandaa vijana kuwa viongozi wa baadaye.

Dk. Bashiru amepata kueleza kuwa kati ya mambo ambayo CCM haiyafanyi kwa muda mrefu ni pamoja na kuwaandaa viongozi wao, huku akirejea historia kwa kusema awali chama hicho kilikuwa na vyuo vya kuwaandaa makada na viongozi kabla ya kurejeshwa serikalini.

“Sasa Umoja wa Vijana (UVCCM) ambao ulikuwa ndiyo tanuru la vijana, likakosa hiyo faida ya vijana kuandaliwa. Sasa kina Bashe na Nape wametokea umoja wa vijana kipindi ambacho maandalizi yao yalikuwa yanasuasua, kipindi ambacho umoja wa vijana ukageuzwa chombo cha wagombea kujipima umaarufu wao, hasa wagombea urais.

“Bahati mbaya chama kikawa mbali na vijana wale na bahati mbaya vijana ni watukutu, wakati wote akili inachemka. Ndivyo Bashe na Nape walivyopatikana, walitokea Umoja wa Vijana, wakaaminiwa, wakapewa nafasi za uongozi wakaenda wakawa wabunge kwa hiyo ule udadisi wao ukaonekana una usumbufu fulani,” amesema Dk Bashiru.

Anaongeza kusema; “Nape Nnauye amekuwa mwenezi wetu jasiri kabisa wa kutetea chama, lakini kwa kweli anahitaji kupikwa. Kwa hiyo nilipokuwa nasema si kwamba nilikuwa nakubaliana nao kila kitu. Kwa hali ilivyo kwa kweli ni kati ya watu kwa maoni yangu wana mchango mkubwa,” anasema Dk Bashiru.

Kwa kuonyesha kuwa si mtu wa kuyumbishwa Julai mwaka jana alirudia kauli hiyo kwenye kikao cha Halmashauri Kuu ya chama wilayani Kakonko Mkoani Kigoma na baadaye wilayani Nzega mkoani Tabora akidai kuwa Bashe na Nape si wakorofi kama inavyodaiwa bali ni wadadisi.

 “Kupitia kwenu ningependa kufafanua kwamba Hussein Bashe si mwanachama mkorofi katika chama, lakini ni miongoni mwa wabunge wadadisi. Kuna tofauti kubwa kati ya mkorofi na mdadisi na kwa udadisi wake anasababisha tetesi zisizokuwa na ukweli.

“Nape kidogo ana joto zaidi kuliko Bashe, lakini wote nawafahamu kwa hiyo msikubali kudanganywa kuwa Nape na Bashe ni watukutu kwa hulka zao. Si watukutu, ni wadadisi,” anasema Dk Bashiru

Huu ndiyo ukweli ambao ni nadra kuusikia ukisemwa na viongozi wengi katika CCM ukweli mchungu wa kuthubutu kuukubali ukweli na hasa kuonyesha kuwa kuna sehemu chama kinakosea, aidha kwa woga wa kutotaka kuonekana ni msaliti wa chama ama kwa kuhofia, kuchukiwa na wanachama wengine.

Hali hii imejionesha hata katika masuala ovu yanayotendwa na makada wa chama hicho ikiwamo kuhodhi maeneo makubwa huku wananchi wakikosa maeneo ya kufanyia shughuli za maendeleo.

Wakati fulani Serikali ilianzisha utaratibu wa kuwapoka baadhi wa watu wanaomiliki maeneo makubwa bila kuyaendeleza huku wananchi wakikosa ardhi kwa ajili ya shughuli za kilimo. Awali  hakuna kiongozi yeyote ndani ya Chama aliyepata kuwataja viongozi waliohodhi maeneo hayo.

Badala yake tuliishia kuona wanaonyang’anywa maeneo ni wananchi wa kawaida, wafanyabiashara, viongozi wa upinzani na baadhi ya waliokuwa wana-CCM kabla ya kukihama chama hicho.

Maana yake ni kwamba viongozi wanaogopana wanalindana, tabia hiyo ya unafiki Dk. Bashiru anaonekana kutoikumbatia.

Hivi karibuni Dk. Bashiru ameeleza kushangazwa na baadhi ya wana-CCM walioanza kuugua ugonjwa wa kusaka urais na kuibua makundi ndani ya chama na kudai kuwa wanawajua na wameanza kuwafuatilia.

Tena anadai kuwa kuna watu tayari wameanza kupanga safu za urais wa mwakani na ule wa 2025 hasa wale wanaotaka urais wa Zanzibar baada ya kumalizika kwa muhula wa pili wa Dk. Mohamed Shein.

Kama tunakumbuka Dk. Bashiru aliwahi kutoa onyo kama hilo Agosti 18, mwaka jana wakati wa ziara yake visiwani humo ambapo aliwataka baadhi ya wana-CCM walioanza kampeni kabla ya muda na kuwataka kuzingatia kanuni na katiba ya chama na kudai kuwa chama hicho kina taratibu zake za kupata viongozi kwani hata Rais aliyepo madarakani atapaswa kuomba ridhaa ya wana CCM ili ateuliwe tena.

Kauli kama hiyo amewahi kuitoa kwa wakuu wa mkoa wanaousaka ubunge akiwataka waache kuvuruga chama na kueleza kuwa atawapeleka kwa aliyewateua amwambie awatafutie kazi nyingine.

Dk Bashiru amekuwa akieleza kuwa chama hicho kimejipanga kuanza kuchukua hatua dhidi ya mwanachama au makundi yenye tabia ya kukidhoofisha kwa kukisema vibaya kinyume na uhalisia.

Si msimamo mgeni kwake kwa sababu hata alipokuwa nje ya chama alifahamika hivyo hakuwahi kuwa vuguvugu mar azote yeye amechagua aidha kuwa wa moto au baridi.

Tutaikumbuka misimamo yake kuhusu Katiba mpya ambayo kwake anaamini kuwa haiepukiki na ni lazima ipatikane ili kuhakikisha ustawi wa demokrasia nchini, japo kwa sasa anakiri kuwa namna ya kudai Katiba hiyo imebadilika kwa sababu tayari yeye ni Katibu Mkuu wa chama chenye Serikali.

Naamini anapaswa kuwa kiongozi wa mfano asiyekuwa na woga dhidi ya watu wote hata kama ni wale wa chama chake, kwa sababu woga huzaa unafiki na matokeo ya unafiki mara zote husababisha kujipendekeza.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles