KWANZA naomba niwape pole nyingi Watanzania wenzangu kwa majonzi na hasira zilizotokana na kichapo ilichopata timu yetu ya Taifa, Taifa Stars katika mchezo wa kufuzu Fainali za Kombe la Mataifa Afrika (AFCON).
Kichapo hicho cha bao 1-0 kutoka kwa wenyeji Lesotho wakati wa mchezo uliofanyika kwenye Uwanja wa Setsoto mjini Maseru Jumapili iliyopita kilififisha matumaini makubwa tuliyokuwa nayo Watanzaniam kufuzu fainali hizo baada ya miaka zaidi ya 30.
Sidhani kama nitakosea nikiutumia msemo alilowahi kuutoa Rais Mstaafu wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi kwamba ‘Tumekuwa kichwa cha Mwendawazimu, kila mmoja anajifunzia kunyoa”
Ningependa kushauri mamlaka za michezo na Serikali kuwa timu hii tuliyo nayo sasa haiwezi kutufikisha popote, zaidi ya kupoteza muda na fedha bure pamoja na kuwapa Watanzania matumaini hewa.
Tunahitaji kuivunja mara moja na kuacha kushiriki mashindano ya kimataifa yanayoihusisha timu yetu hii ya Taifa kwa muda ili kutoa nafasi ya kujiandaa hadi tutakapokuwa tayari kwa mashindano hayo.
Na wakati huo huo tutafakari kama Taifa wapi tulikosea na kujifunza kwa wenzetu, ambao pengine walipitia njia tuliyomo sasa na baada ya kujipa muda wa kutafakari badala ya kulazimisha vitu visivyowezekana.
Hata hivyo, si makusudio yangu katika makala haya kuzama katika suala hilo la michezo, bali kujikita katika jambo lingine, ambalo naona ni muhimu linalolikabili Taifa kwa sasa-zao la korosho.
Ni baada ya uhakiki wa majina ya wakulima wa korosho pamoja na mambo mengine kufichua madudu ikiwamo uwapo wa majina hewa kama vile mwenza wa karani wa chama cha msingi cha Makonga wilayani Newala.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mkuu wa Wilaya ya Newala, Aziza Mangosongo, majina hayo yalibainika baada ya kupata taarifa kutoka kwa wananchi. Katika utafiti huo ilibainika kuwa kilo 200 zilikuwa zimeandikiwa malipo hewa.
Hali hii yenye lengo la kukandamiza jasho la mkulima inachukiza na haileti picha nzuri kwa taswira ya Taifa.
Hali haiko hivyo pekee, kuna utaratibu usio rasmi wa baadhi ya watu kujihusisha na ununuzi wa korosho kutoka kwa wakulima unaoitwa ‘Kangomba’, ambao baadhi ya matajiri hutuma fedha vijijini na wenyeji kununua korosho, lakini wanapokamatwa huwataja hao matajiri hao kuwa ndio waliowatuma.
Hii michezo yote niliyoitaja hapo juu yenye lengo la kumkandamiza mkulima haikuanza kama unavyoota uyoga bali inaonekana imeota mizizi baada ya kufumbiwa macho na wahusika wakiwamo viongozi wa maeneo yote hayo.
Tatizo kubwa la Watanzania linalotukabili ni kufumbia macho hujuma zinazofanyika kwenye sekta mbalimbali, hali inayozifanya siwe sehemu ya utaratibu wa kawaida na matokeo yake kuathiri kizazi kizima.
Yawezekana kabisa matatizo kama haya hayapo kwenye zao la korosho pekee bali mazao yote ya biashara lakini kama kawaida yakiwa yamefumbiwa macho.
Tumeanza na korosho kwa sasa naamini bila shaka tukija kwenye pamba nako yataonekana madudu ambayo yataushangaza umma.
Nitoe rai kwa viongozi wenye dhamana hasa wanaosimamia kazi yote ya ukusanyaji wa korosho hivi sasa kusimama kidete kuhakikisha wanapata taarifa zote zilizo na taswira mbaya ya kumkandamiza mkulima wa Korosho.
Kwa miaka nenda rudi mkulima ameendelea kuwa maskini huku jasho lake likiwanufaisha watu wachache wenye lengo la kujitajirisha wao na familia zao.
Kazi wanayoifanya ni ya manufaa kwa Taifa, huo ndio uzalendo unaotakiwa na hawapaswi kukubali kuwapa nafasi wahujumu uchumi kujiona wameshinda vita hii.
Tunapaswa kumuunga mkono Rais wetu Dk. John Pombe Magufuli kuhakikisha jasho la mnyonge linalipwa inavyostahili.
Wananchi tulio nje ya mikoa inayolima zao la korosho tunaungana na timu nzima ya viongozi iliyopewa jukumu la kusimamia kazi ya kuhakiki, ukusanyaji na usambazaji kwenye maghala kuhakikisha haki inatendeka.
Naamini kazi inayofanywa haina lengo la kumkomoa mtu, kikundi au watu fulani bali kuhakikisha jasho la mkulima ambalo limekuwa likipotea linalipwa kulingana na kazi aliyoifanya.
Naiomba Serikali kuziba masikio kwani yatasemwa mengi wakati kazi hii yenye tija ikiendelea, mara nyingi watu wasioitakia mema nchi hawakosi la kusema au kulaumu, lakini hayo yasiwe chanzo cha kurudisha nyuma moyo na ari waliyoianza.
Ni kwa sababu kila linapofanyika jambo lenye na tija kwa wananchi lazima kitatokea kikundi cha watu wachache watakaojitokeza kulaumu. Lakini huu si wakati wa kusikiliza maneno ya pembeni, kwani wananchi walio wengi wanaiunga mkono Serikali yao tukufu.