Oscar Assenga -Tanga
MADIWANI wanane waliokuwa wa Chama cha Wananchi (CUF), ambao walitangaza kujiunga na CCM katika ziara Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk. Bashiru Ally wamehudhuria kikao cha bajeti cha Halmashauri ya Jiji la Tanga na kupitia bajeti ya mwaka 2020/21/
Hatua hiyo ilizua maswali huku baadhi ya wanasiasa na wananchi wakihoji uhalali wa kikao hicho kwa kuhudhuriwa na wajumbe ambao hawakutakiwa kwa mujibu wa sheria.
Katika kikao hicho halmashauri ya katika mpango wake wa bajeti ya mwaka 2020/21 imepitisha mapendekezo ya kukusanya Sh bilioni 66.1 kutoka katika vyanzo vya ndani, ruzuku ya Serikali Kuu na wahisani mbalimbali.
Akizungumza wakati wa kikao hicho Mkurugenzi wa Jiji la Tanga Daudi Mayeji wakati wa kikao maalumu cha kujadili mapendekezo ya mpango wa bajeti ya halmashauri hiyo kwa mwaka 2020/21.
Alisema kwamba upande wa vyanzo vya ndani halmashauri hiyo inakadiriwa kukusanya kiasi cha Sh bilioni 15.3 na fedha kutoka Serikali Kuu na wahisani zinakadiriwa kiasi cha Sh bilioni 49.8ambapo ruzuku ya mshahara ni Sh bilioni 40.7.
Mkurugenzi huyo alisema kwa upande wa ruzuku ya miradi ya maendeleo ni Tsh Bilioni 7.8 na matumizi mengineyo (OC) ni Bilioni 1.3 huku akieleza nguvu za wananchi katika kuchangia miradi ya maendeleo zinakadiriwa kuwa zaidi ya Tsh.Milioni 984.
Akizungumzia ubatili huo wa bajeti hiyo ikiwemo matumizi mabaya ya fedha za umma, Katibu wa Chama cha ACT Wazalendo Mkoa wa Tanga, Abdulrahman Lugone alisema madiwani hao hawakutakiwa kushiriki vikao hivyo na kupokea posho wala marupurupu kwa kuwa si wajumbe halali wa kikao hicho.