Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
Madiwani wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wa Kata ya Makurumla Manispaa ya Ubungo, Bakari Kimwanga na mwenzake wa Mzimuni Manispaa ya Kinondoni, Manfred Lyoto wamebaini uchafuzi wa mazingira katika mfereji wa mpaka unaotenganisha kata zao.
Katika ziara yao walioifanya leo Alhamis Januari 28, madiwani hao wakiwa wameambatana na wenyeviti wa mitaa ya Mtambani, Abdullah Kitumbi na Ibrahim Mselemu wa Kimamba, walikagua mfereji huo ambao walibaini nyumba nyingi za zilizopo kando ya mfereji huo, zimeunganisha mabomba ya maji machafu ikiwamo kutiririsha maji taka.
Akizungumzia hali hiyo Diwani Kimwanga, amesema kuwa katika kipindi hiki ambacho mvua zipo jirani ni lazima mrefeji huo usafishwe kwa kuwashirikisha wananchi.
“Ni aibu kwani yapo mambo ambayo wenyeviti wa mitaa mnatakiwa kuuangalia badala ya kukaa ofisini. Hivyo leo tumeona namna baadhi ya wananchi wameunganisha mabomba ya maji taka jambo ambalo ni hatari kwa afya zao.
“Tunachoomba wenyeviti kutaneni haraka mpange kikao cha pamoja ambacho kitashirikisha wananchi wa pande mbili na hiki kikao mtuarifu mapema mimi na mwenzangu (Lyoto) tutahudhuria,” amesema Kimwanga
Kwa upande wake Diwani Lyoto, amesema kuwa ipo haja kusafishwa kwa mfereji huo ikiwamo kuomba nguvu ya pamoja kwa Manispaa ya Ubungo na Kinondoni.
“Yapo maeneo yanahitaji nguvu Kazi ya wananchi na mengine ni lazima tusafishe mfereji kwa kutumia burudoza,” amesema Lyoto.